LICHA ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kutangaza msimamo wa
kukataa serikali tatu, Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete,
amewataka wake wajiandae kisaikolojia kwa mabadiliko yoyote
yatakayotokea kinyume na matakwa yao.
Kwa mujibu wa chanzo kimoja kutoka ndani ya kikao cha Baraza la
Kikatiba la Halimashauri Kuu ya CCM ambalo linapitia vifungu vya rasimu
ya Katiba Mpya, Rais Kikwete aliwataka makada wenzake kujiandaa kwa
lolote kama ilivyotokea mwaka 1992.
Rais Kikwete alisema mwaka 1992 idadi kubwa ya wanachama wa CCM walikataa mfumo wa vyama vingi lakini mfumo huo ulipita.
Kiongozi huyo alisema katika kikao hicho cha mwaka 1992 ilikubalika kuwa ‘wengi wapewe wachache wasikilizwe’.
Katika kikao cha jana Kikwete aliwataka wana CCM wajiandae
kisaikolojia kwa jambo lolote litakaloamriwa na wananchi watakaopiga
kura juu ya rasimu ya Katiba mpya.
Kwa mujibu wa chanzo cha Tanzania Daima, Katibu wa Halmashauri Kuu ya
Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Dk. Asha Rose Migiro, aliwasilisha na
kuchambua upungufu uliopo kwenye rasimu ya Katiba Mpya iliyotolewa hivi
karibuni na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Kutokana na upungufu huo hasa katika mfumo wa serikali idadi kubwa ya
makada wa chama hicho ilikubaliana kuendelea na msimamo wao wa serikali
mbili.
Mara baada ya Migiro kumaliza, walisimama wajumbe kadhaa na Kikwete
kumpa nafasi mmoja wao ambaye alitaka wasiendelee na suala la Katiba
mpya liahirishwe mpaka baada ya mwaka 2015.
Inaelezwa kuwa mjumbe huyo kutoka Zanzibar, alijenga hoja kuwa suala
la Katiba mpya halikuwa kwenye ilani ya uchaguzi wa chama hicho ya mwaka
2010.
Mjumbe huyo alisema ilani ya chama hicho ilitoa ahadi za ujenzi wa
madaraja, barabara, ununuaji wa meli na nyinginezo nyingi ambazo mpaka
sasa bado.
Alisema ni busara CCM ikaachana na hoja hiyo mpaka baada ya uchaguzi wa mwaka 2015.
Hata hivyo baada ya mjumbe huyo kutoa hoja hiyo, Kikwete aliwataka
wajumbe wajadili mantiki ya rasimu ya Katiba mpya badala ya kufoka au
kubishana.
Rais Kikwete alisema mazingira ndiyo huamua jambo fulani hivyo hakuna sababu hoja hiyo ya Katiba kutojadiliwa hivi sasa.
Inaelezwa kuwa Rais alisema licha ya asilimia 80 ya Watanzania
kutoukubali mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 hoja hiyo ilipita kutokana
na mazingira.
Alisema licha ya hofu ya Watanzania juu ya mfumo wa vyama vingi bado
mfumo huo umendelea kuwepo mpaka hivi sasa na umeonyesha maendeleo.
Baada ya kauli hiyo wajumbe walianza kupitia kifungu kwa kifungu
Rasimu ya Katiba mpya ambapo wengi walipinga muundo wa serikali tatu
uliopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Msimamo wa CCM
Chama hicho tawala tangu kutoka kwa Rasimu ya Katiba kimekuwa
kikisisitiza msimamo wa kutambua serikali mbili na si tatu kama
ilivyotolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu
Joseph Warioba.
Kamati Kuu (CC) iliyoketi Juni mwaka huu iliamua kuipeleka rasimu hiyo
kwa wananchi wake kuanzia ngazi ya matawi na kutaka yaundwe mabaraza ya
Katiba ya chama hicho.
Hata hivyo CCM ilishaweka wazi msimamo wake kuwa haitokubali muundo wa serikali tatu.
Akizungumza na Tanzania Daima, kabla ya kuingia katika kikao jana
jioni, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema suala la Katiba
limewachukua nafasi kubwa.
Alisema suala hilo limechukua muda mwingi kutokana na kupitia kifungu
kwa kifungu na mpaka jana saa 10, walikuwa wamepitia vifungu 140.
“Tumeshindwa kuanza kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) kama
tulivyotarajia kutokana na majadiliano hayo lakini nina imani tutamaliza
vizuri.”
Nape alisema suala la kuingizwa kwa uraia wa nchi mbili katika Katiba Mpya nalo liliteka zaidi mjadala.
0 comments:
Post a Comment