Mwenyekiti wa kampuni za IPP, Reginald Mengi.
MWENYEKITI wa kampuni za IPP, Reginald Mengi ametoboa siri kuwa
hakuna mfanyabiashara wa Tanzania aliyefanikiwa katika biashara kubwa
kwa kusaidiwa na serikali bila ya kutoa rushwa.
Mfanyabiashara huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa
Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), alisema yeye aligoma kutoa rushwa
kwa watendaji wa serikali jambo lililosababisha kupoteza fursa nyingi
ambazo zingemfanya awe na maendeleo zaidi ya aliyonayo hivi sasa.
Kauli hiyo aliitoa jana jijini Dar es Salaam wakati akichangia mada
katika uzinduzi wa ripoti ya uchumi na maendeleo barani Afrika kwa
mwaka 2013, uzinduzi uliofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Diplomasia.
Alisema kutokana na kukithiri huko kwa rushwa, maendeleo ya
kibiashara na kijamii hapa nchini hayawezi kufikiwa kama jitihada za
kupambana na nayo zitapuuzwa.
“Ili ufanikiwe ni lazima uione fursa iliyopo, lakini tatizo liko wapi
mnajua… ni kwa hawa waliopewa dhamana ya kutoa vibali kuendekeza
rushwa,” alisema Mengi.
Alisema ni vigumu katika nchi iliyojaa rushwa kuzungumzia suala la
amani wakati wananchi wanapata huduma mbovu kutokana na watendaji wa
serikali, taasisi na idara zake kuendekeza rushwa.
Alibainisha kuwa idara nyingi za serikali hivi sasa zimegubikwa kwa
rushwa kiasi cha kuathiri huduma mbalimbali zitolewazo huku akitolea
mfano wa matumizi ya bajeti ya serikali ya sh trilioni 18
yaliyoidhinishwa na Bunge hivi karibuni.
“Tunaweza kuangalia dhamira nzuri ya serikali hasa katika bajeti ya
trilioni 18, manunuzi ya umma ni asilimia 80. Kati ya hizo asilimia 20
-30 zinaweza kuishia katika mianya ya wizi na rushwa, na mambo haya
yanaweza kufanywa na watu wachache huku wengi wakiangamia kwa kukosa
huduma muhimu,” alisema.
Alisema mbali na fedha zinazopotea katika manunuzi ya umma, maeneo
mengine yanayofanya madudu kwa kiasi kikubwa ni sekta ya bandari,
TANESCO na reli ambako alibainisha kuwa wajanja wachache wanatumia
fursa walizonazo kujitengenezea mianya ya kufaidi rushwa ya maeneo
hayo.
Aliongeza kuwa mianya ya rushwa isipodhibitiwa Mtanzania wa kipato
cha chini ataendelea kuumia hata kama kipato chake kitaongezeka.
Alisisitiza kuwa tatizo jingine linalochangia rushwa nchini ni
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kutokutambuliwa
katika katiba pamoja na kunyimwa uwezo wa kuwashitaki watoaji na
wapokeaji wakubwa wa rushwa.
Alisema katika kupambana na rushwa nguvu ya TAKUKURU inaishia katika
kuwashitaki watuhumiwa wadogo, huku wakubwa wakisubiri uamuzi wa
Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP).
Mengi alisema ana wasiwasi kuwa kwa hali ilivyo sasa kwenye sekta ya
madini nchini hakuna Mtanzania atakayebaki miaka michache ijayo iwapo
mambo hayatabadilishwa.
Alibainisha kuwa sera na kauli zinazotolewa midomoni mwa viongozi
zinaelekeza kumuwezesha Mtanzania katika fursa mbalimbali wakati
uhalisia wa matendo yao hauendani.
“Viongozi wanasema mdomoni kuwa wanataka kuwawezesha Watanzania,
lakini ukweli ni kwamba kuna mkakati wa kuwarudisha nyuma kwa kasi
kubwa,” alisema Mengi.
Awali, Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Felix Mosha
akiwasilisha ripoti ya uchumi na maendeleo 2013 kwa bara la Afrika
ambapo alisema ukosefu wa miundombinu bora katika bara hilo unachangia kwa
kiasi kikubwa wawekezaji kushindwa kuwekeza katika maeneo yatakayoweza
kumkwamua mwananchi wa kawaida.
Alisema nchi imefanya makosa makubwa kupuuzia kilimo cha kisasa na
kukimbilia kuwekeza katika sekta nyingine huku ikiwaacha watu takribani
asilimia 80 katika mbio za kuelekea katika mafanikio.
“Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 duniani na katika Afrika ni kati ya
tano bora ambayo uchumi wake unaokua kwa kasi kubwa, lakini wananchi
wake wanaendelea kuwa katika hali duni. Hii ni kwa kuwa uwekezaji
unafanywa katika maeneo yasiyowanufaisha wananchi moja kwa moja,”
alisema Mosha.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment