Na Gideon Mwakanosya-Songea
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda amewataka wakulima wa Mkoa wa Ruvuma kuona
umuhimu wa kujipanga kikamilifu katika uzalishaji wa mazao ya chakula na
biashara yatakayoweza kuboresha uchumi wao na taifa kwa ujumla kwa kulitumia
soko la kimataifa lililopo katika kitongoji
cha Mkenda kilichopo katika kijiji cha Nakawale (Mhukuru) kilichopo
mpakani mwa Tanzania na Msumbiji linalotarajiwa kuanza wakati wowote mara baada
ya kukamilika kwa ujenzi wa soko hilo.
Waziri Mkuu Pinda ameyasema hayo
hapo jana wakati alipokuwa akiweka jiwe la msingi la soko la kimataifa la
mpakani Mkenda lililopo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji ambalo linajengwa kwa
fedha zilizotolewa na mfuko wa Umoja wa Ulaya (EU) lenye thamani ya shilingi
169,239,746/= kwa kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara soko ambalo litatoa
fursa kubwa kwa wakulima na wafanyabiashara wakubwa na wadogo watakaotumia
vyema nafasi hiyo.
Alieleza kuwa kwa hivi sasa eneo
hilo la kitongoji cha Mkenda linahitaji kuwepo miundombinu mizuri ambayo itaweza
kukidhi haja ya Watanzania hasa wanaoishi mpakani mwa Tanzania na Msumbiji
hivyo fursa zilizopo zinahitajika kuboreshwa zaidi ili kuwajengea wananchi
uweza wa kiuchumi ikizingatiwa kuwa eneo hilo halikuwa na fursa hizi.
Pinda amewahakikishia wananchi wa
maeneo ya mpakani mwa Tanzania na Msumbiji kuwa serikali ina mpango wa kuweka
miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami kutoka njipanda ya Likuyufusi hadi
Mkenda ili kuwaondolea adha ya usafiri wanayoipata hivi sasa na kwamba nia kubwa
ya serikali ni kuimarisha miundombinu ya barabara katika maeneo ya kutoka
Mbinga mjini hadi Mbambabay, kutoka Kitai kupitia Rwanda Lituhi hadi Mbambabay,
kutoka Namtumbo kupitia Tunduru hadi Mangaka Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara.
Alisema barabara zote hizo
zinatarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami na kwamba kwa hivi sasa serikali
imejitahidi kwa kujenga barabara kwa kiwango cha lami kutoka Songea mjini hadi
Mbinga mjini na kutoka Songea mjini kwenda Namtumbo ambazo kwa hivi sasa
zimekamiliza lakini yamebaki matengenezo madogomadogo jambo ambalo watanzania
tunahitaji kujipongeza.
Hata hivyo, Waziri Mkuu Pinda
amempongeza meneja wa wakala wa barabara (Tanroads) mkoani Ruvuma Eng. Abraham
Kissimbo kwa usimamizi mzuri alioufanya wakati miradi mikubwa ya ujenzi wa
barabara hizo ilipokuwa ikitekelezwa hivyo amemwagiza waziri wa ujenzi
kuhakikisha kuwa meneja huyo anakuwepo Ruvuma ili aweze kusimamia miradi ya
ujenzi labda kama itaelekezwa vinginevyo.
“Maendeleo ni hatua hivyo
nampongeza sana meneja wa Tanroads Ruvuma Eng. Abraham Kissimbo kwa kazi nzuri
aliyofanya kwa kipindi chote alichokuwepo kwani barabara za lami na za vumbi
nilizopita zimekuwa nadhifu hivyo ni vizuri akaendelea kubaki Ruvuma ili aweze kuboresha zaidi
miundombinu ya barabara”, alisema Waziri Mkuu Pinda.
Aidha, Waziri Mkuu Pinda amekubali
ombi la kuigawa wilaya ya Songea ambayo ni kubwa sana lililototewa na Mbunge wa
jimbo la Peramiho Jenista Mhagama ambaye alimwomba waziri Mkuu Pinda kuwa
Wilaya ya Songea ina eneo kubwa hivyo ni vyema akaona umhimu wa kukubaliana na
ombi la kuligawa.
Waziri Pinda alieleza kuwa
anakubalina na ombi la kutaka kuigawa Wilaya ya Songea lakini akaushauri
uongozi wa wilaya hiyo kuona namna ya kuanza mchakato ili taratibu zifuatwe na
yeye hana pingamizi ya aina yoyote lakini aliwataka wananchi wa wilaya hiyo
kujijengea uwezo zaidi katika sekta mbalimbali zikiwemo za elimu, afya na kilimo
ambazo zinahitajika sana kwenye maeneo mengi hapa nchini.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo
la Peramiho Jenista Mhagama mara tu baada ya kupewa nafasi ya kujitambulisha na
Mkuu wa mkoa ndugu Said Mwambungu alisema kuwa kwa niaba ya wananchi wa jimbo la
Peramiho anamshukuru waziri Mkuu Pinda kwa kukubali kutembelea kitongoji cha
Mkenda ambacho kiko mpakani mwa Tanzania na Msumbiji pia aliipongeza serikali
kwa kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara kuamua kujenga soko la kimataifa
kwenye eneo hilo ambalo lipo mbali sana na makao makuu ya wilaya na mkoa (KM
124) kisha akaipongeza serikali kwa kujenga daraja kubwa na zuri ambalo ni
kiungo kikubwa kati ya Tanzania na Msumbiji.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri
ya Wilaya ya Songea, Sigsbert Valentine akitoa taarifa ya ujenzi wa jenga la
soko hilo kwa Waziri Mkuu Pinda alisema kuwa ujenzi wake unaofadhiliwa na mfuko
wa Umoja wa Ulaya (EU) kwa kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara ukikamilika
utaweza kuwaletea wananchi wa Mkoa wa Ruvuma fursa nyingi zitakazotokana na
soko hilo ambapo alizitaja kuwa ni pamoja na taasisi za fedha, shule za msingi
na sekondari, hospitali, ofisi mbalimbali za serikali, maghala ya kuhifadhia
mazao au mizigo na nyumba za kulala wageni.
Alisema kuwa kwa sasa hivi halmashauri
yake tayari imepima viwanja 620 vye hadhi mbalimbali ambapo alivitaja kuwa ni
vya ujazo wa chini (Low density) viwanja 31, ujazo wa kati (Medium density)
viwanja 93 na ujazo wa juu (High density) viwanja 496 ambapo alieleza kuwa kati
ya viwanja hivyo 462 ni vya makazi ya watu, viwanja 121 ni vya makazi na
biashara na viwanja 37 ni vya biashara tu hivyo amewaomba watu wenye uwezo
wakiwemo wafanyabiashara wafike Mkenda kuwekeza.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment