Askari wa M23
Afisa mmoja wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo ametiwa nguvuni baada ya kuchafua maiti za wapiganaji wa waasi
nchini humo.
Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa DRC,
Lambert Mende, ameiambia BBC kwamba Luteni Solomo Bangala alizuiliwa
juzi Alhamisi na maafisa wa kijeshi baada ya mapigano kuzuka kati ya
jeshi na waasi wa M23 katika eneo la mashariki karibu na mji wa Goma.
Kukamatwa kwa afisa huyo kunajiri
muda mfupi tu baada ya katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki Moon
kuzungumzia madai ya kuwepo dhuluma na mateso dhidi ya wafungwa kutoka
makundi ya waasi pamoja na wale waliouwawa zinazotekelezwa na wanajeshi
wa Kikongomani.
Kikosi cha kulinda amani cha umoja wa mataifa
kinatathmini upya hatua yake ya kuunga mkono vikosi vya serikali ya DRC
kufuatia shutuma hizo.
Mapigano kati ya jeshi la DRC na waasi wa M23 yalianza siku ya Jumapili karibu na mji wa Goma.
Mwandishi wa BBC Maud Jullien aliyepo katika mji
wa Goma anasema uwanja wa mapigano ulikuwa takriban kilomita 7 katika
vilima kutoka mji huo.
Hapajakuwa na mapigano yoyote katika kipindi cha
siku mbili zilizopita na jeshi limesema limefanikiwa kuwafukuza waasi
yapata kilomita 6, anasema mwandishi wetu.
Mwezi Novemba, wanamgambo wa M23 waliuteka kwa
kipindi kifupi mji wa Goma, kisha wakaondoka baada ya kutimizia msururu
wa ahadi ikiwemo kuanzisha mazungumzo na serikali.
Waasi wa M23, ambao kwa wingi wanatoka kabila la
Watutsi walijiondoa katika jeshi la serikali mwezi Aprili mwaka 2012,
na kuanzisha mapigano yaliyowaacha takrikaban watu 800,000 bila makao
katika eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa madini.
Mazungumzo ya amani yaliyofanyika nchini Uganda mwaka huu ili kushughulikia malalamishi ya waasi hao yamekwama.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment