Waziri wa mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi
MDAHALO wa kujadili mstakabali wa amani ya taifa ulioandaliwa na
Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA), umeibua
mambo mazito ambapo washiriki wameinyooshea kidole serikali wakidai
ndiye mchawi wa wananchi.
Mdahalo huo ambao kauli mbiu yake ilikuwa ni Mustakabali wa Amani na
Usalama wa Wananchi wa Taifa Letu kwa Miaka 50 Ijayo, ulifanyika jana
katika Ukumbi wa Nkrumah wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na
kuwashirikisha wanazuoni, wanasiasa, viongozi wa vyombo mbalimbali vya
ulinzi na serikali.
Wachokoza mada walikuwa ni mhadhiri wa sheria wa chuo hicho, Dk.
Onesmo Kyauke aliyegusia mfumo wa utendaji wa Jeshi la Polisi katika
kusimamia amani ya nchi, Profesa Benadetha Kiliani, mtaalam wa sayansi
ya siasa na utawala kwa umma na mwanahabari nguli na mhadhiri wa Shule
Kuu ya Uandishi wa Habari, Dk. Ayoub Rioba.
Katika mada yake, Dk. Kyauke aliliponda jeshi la polisi linavyokiuka
sheria katika kutekeleza majukumu yake kiasi cha kuruhusu kuingiliwa na
wanasiasa na kuelekezwa jambo la kufanya.
Bila kuuma maneno, mhadhiri huyo alimtaja wazi wazi Naibu Katibu Mkuu
wa CCM (Tanzania Bara), Mwigulu Nchemba, akidai kwa sasa analiendesha
jeshi hilo kwa kuingilia majukumu ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya
Jinai (DCI) na Mwendesha Mashataka Mkuu (DPP).
Alisema kuwa mwanasiasa huyo ambaye ni mbunge wa Iramba Magharibi,
amekuwa akiwatuhumu wanasiasa wa vyama vya upinzani kuwa ni magaidi na
polisi wamekuwa wakiwakamata na kuwafungulia mashtaka hayohayo anayosema
kada huyo bila hata kuwa na ushahidi.
Dk. Kyauke alitolea mfano wa matukio ambayo Nchemba amekuwa akiyafanya
kuwa ni pamoja na lile la kuonyesha ushiriki wa kupanga tukio la ugaidi
la Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo(CHADEMA), Wilfred Lwakatare.
Tukio lingine alisema ni wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa
udiwani jijini Arusha, ambapo kiongozi huyo aliwataka wananchi wa jiji
hilo kutochagua madiwani wa CHADEMA kwa kuwa ni chama cha ugaidi kwa
madai kwamba ndio waliohusika kummwagia tindikali kijana wa CCM kule
Igunga.
Kutokana na matamshi hayo, mhadhiri huyo alisema baadhi ya wanachama
wa CHADEMA waliweza kukamatwa kama njia mojawapo ya kuisaidia polisi;
jambo linalowafanya kama wasomi kujiuliza kuwa Mwigulu siku hizi kawa
DCI au DDP?
Kuhusu utendaji wa Jeshi la Polisi, alisema ndilo limekuwa chanzo
kikubwa cha uvunjifu wa amani kwa kupoka haki ya Kikatiba ya wananchi
kuandamana na kufanya mikutano huku akitolea mfano wa mauaji
yaliyofanywa na jeshi hilo ya mwandishi wa habari, Daudi Mwangosi,
kijijini Nyororo, mkoani Iringa, wakati wa kuzindua matawi ya CHADEMA.
Katika mauaji hayo, alisema ushahidi wa wazi umeonyesha namna gani
polisi walivyoshiriki na tume zote zilizoundwa zikamuelekezea kidole
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa na Msajili wa Vyama vya Siasa,
lakini hakuna hatua zilizochukuliwa hadi leo zaidi ya polisi mwenye cheo
kidogo akitolewa kafara huku mkubwa wake akiendelea kupandishwa cheo.
Pia alisema kumekuwepo na upendeleo wa jeshi hilo kwa kutetea chama
tawala ikiwemo enzi za IGP Omar Mahita kudai kuwashikilia wanachama wa
Chama cha Wananchi (CUF) na majambia ingawa hadi leo wamekosa
uthibitisho lakini kutokana na uongo huo wameshindwa kumchukulia hatua
kiongozi huyo.
Katika mapendekezo yake, Kyauke aliitaka polisi kubadili mfumo wake
wa kufanya kazi, na kuhoji kwa nini Tanzania ni dhambi kuandamana huku
akimtaka Waziri Mkuu kufuta kauli yake ya kutaka wananchi kupigwa tu na
jeshi hilo wanapokaidi amri.
Prof. Kilian kwa upande wake, alisema mpaka sasa bado kiini cha
uvunjifu wa amani hakijagundulika na badala yake pande zote zimekuwa
zikirushiana mpira ikiwemo serikali, wananchi na wanasiasa.
Alizitaja sababu zinazochangia matukio hayo kuwa ni pamoja na hali ya
upinzani kuja juu hivyo chama tawala kinajihami kutokana na mabadiliko
hayo, kuongezeka kwa kiwango cha umaskini na mfumo wa kiliberali ambao
umechangia matabaka na uhuru wa kutoa maoni tofauti na enzi za ujamaa.
Naye Dk. Rioba alisema suala la amani sio la kuombewa kanisani au
msikitini bali ni la kisayansi zaidi na kudai kwamba wanasiasa wamekuwa
wakijidanganya pale wanapowahimiza watu kuliombea taifa liwe na amani.
Pia Rioba alikanusha vyombo vya habari kuwa vimekuwa vikichangia
kuharibu amani na badala yake alivifananisha vyombo hivyo na bunduki
ambapo kama isipotumiwa kamwe haiwezi kuharibu amani.
Akifafanua hili alisema vyombo vya habari vitaharibu amani endapo tu
wanasiasa watavitumia na kuitaka jamii ielewe kwamba vyombo hivyo vina
dhima kubwa kama mlinzi wa taifa na ndio maana wakati mwingine
vinapendekezwa kuwa NGO’s ili viweze kufanya kazi kwa uhuru zaidi.
Katibu Mkuu wa CHADEMA Dk. Willibrod Slaa alisema mchawi wa hayo yote
ni serikali, huku akinukuu ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala
Bora iliyomtuhumu aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa,
Michael Kamuhanda, na Msajili wa Vyama vya Siasa. Akisema amani sio
suala la kuhubiriwa au kujadiliwa bali ni matokeo ya utekelezaji wa haki
mbalimbali.
Slaa pia alilalamikia vitendo vya ukatili vilivyofanywa Mtwara na
vyombo vya dola dhidi ya wananchi, huku akimnyooshea kidole Brigedia
Elia Athanas aliyekuwa amemwakilisha Mkuu wa Majeshi.
“Jeshi letu lilikuwa linaheshimika sana, lakini siku za hivi karibuni
linaelekea kupoteza heshima yake kwa jamii, tukirejea mfano katika
uchaguzi mkuu uliopita ambapo mnadhimu wa jeshi, Abdulrahman Shimbo,
alivyotoa kauli yenye utata, jeshi linaingiaje kwenye siasa wakati suala
la uchaguzi ni suala la kiraia?” alihoji.
Hoja ya Dk. Slaa kuhusu utendaji wa jeshi la wananchi mkoani Mtwara
ilipingwa kwa haraka na Brigedia Athanas akisema: “Naomba kuweka wazi
kuwa jeshi letu liko Mtwara, lina adabu na vitendo ambavyo vimekuwa
vikiripotiwa ni vya propaganda tu kama alivyosema Dk. Slaa.”
Licha ya kiongozi huyo kujitetea, mchangiaji aliyefuata, Julius
Mtatiro ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Tanzania Bara),
alithibitisha kuwa wanajeshi wanabaka na walitenda vitendo vya kikatili
dhidi ya raia na viongozi wa chama hicho akiwemo mkurugenzi wao, Shaweji
Mketo.
Mwakilishi wa NCCR Mageuzi, Faustine Sungura, alisema chama hicho
hakiko tayari kufanya maandamano bali kinapambana kwa nguvu ya hoja na
kwamba wataendelea kutumia nguvu ya hoja.
Akihitimisha kongamano hilo, Wazri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel
Nchimbi, alisema kuwa kati ya mambo ambayo yanampa changamoto ni amani
ya nchi hii.
“Tulirithi nchi ikiwa na amani, hivyo tuna deni la kurithisha nchi hii ikiwa ya amani katika kizazi kijacho.
Dk. Nchimbi alikemea suala la udini, akiwatahadharisha Watanzania kuwa
wasiingie katika vurugu na wasikubali kugawanywa kwa sababu ya dini
zao.
“Tukiingia katika vurugu za dini hatutapona, Wakristo na Waislam wote
tukatae kugawanywa kwa kutumia misingi ya udini kwa manufaa ya Tanzania
ya sasa na kizazi kijacho.
Waziri Nchimbi huku akimtambua Dk. Slaa, alisema wanasiasa wote wana
wajibu wa kuwatumikia wananchi, “Suala la amani sio suala la Chama cha
Mapinduzi peke yake, ni suala la wanasiasa wote wa chama tawala na
wapinzani kutambua kuwa wao ni watumishi wa umma, na kuvumiliana kisiasa ndiko kunaleta amani.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment