Mbunge wa Jimbo la Arumeru, Joshua Nassari
 
Jeshi la Polisi mkoani Arusha, jana lilimshikilia Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari akituhumiwa kumshambulia kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hussein Warsama wakati wa uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Makuyuni, wilayani Monduli.
 
Nassari aliyefika Kituo Kikuu cha Polisi Arusha saa 2:30 asubuhi jana, alishikiliwa kwa saa tatu na nusu baada ya kuhojiwa, ambapo aliachiwa saa 6:02 mchana, baada ya kujidhamini mwenyewe.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Arusha (RCO) Diwan Nyanda, Nassari anadaiwa kumshambulia Warsama, Julai 16 mwaka huu, huko Makuyuni alipokuwa wakala mkuu wa mgombea udiwani kupitia Chadema, Japheth Sironga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Lebaratus Sabas hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo, baada ya simu zake zote mbili za kiganjani kuita bila kujibiwa, huku Nyanda ambaye Nassari aliripoti kwake akikataa kuzungumzia suala hilo na kutaka atafutwe RPC kwa maelezo kwamba ndiye msemaji wa polisi mkoa.
“Niko njiani naenda Dodoma, mtafute afande RPC, ndiye msemaji wa polisi mkoa,” alisema RCO Nyanda kwa njia ya simu jana.
Hata hivyo, habari za uhakika kutoka duru za polisi zinaeleza kuwa Jeshi la Polisi walianza kumsaka Nassari tangu Jumanne iliyopita kupitia kwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Arumeru.
Habari hizo zilizothibitishwa na Nassari mwenyewe zimeeleza kuwa Jumatano ya Julai 24 mwaka huu, Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai wa Jeshi la Polisi, Kamishna Isaya Mngulu alimpigia simu mbunge huyo kumtaka afike polisi, ndipo walipokubaliana kuwa aende jana.
Tuhuma zinazomkabili
“Nilipofika polisi na kuripoti kwa RCO, nikawekwa chini ya ulinzi na kutakiwa kutoa maelezo kuhusu madai ya kumshambulia mtu mmoja anayejulikana kwa jina la Husein Warsama siku ya uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Makuyuni,” alisema Nassari.
Mbunge huyo alisema kuwa baada ya kuwekwa chini ya ulinzi, RCO Nyanda alimkabidhi kwa ofisa mwingine wa polisi kwa ajili ya mahojiano, lakini alikataa kuandikisha maelezo yoyote kwa sababu hakuwa ameambatana na wakili wake.
Nassari alifafanua kuwa maelezo hayo yalionekana kuwaudhi polisi ndipo RCO aliagiza awekwe mahabusu hadi wakili wake, Tundu Lissu na Mabere Marando watakapofika, huku polisi kutoka wilayani Monduli wakiwa wamefika tayari kumchukua na kumpeleka huko kutokana tuhuma zinazomkabili kuwa zilifanyikia wilayani humo.
“Baada ya mimi kuwa tayari kuwekwa mahabusu na kuanza kukabidhi vifaa vyangu, RCO na maofisa wengine wa polisi waliokuwepo, walifanya majadiliano mafupi na baadaye kunikubalia kujidhamini mwenyewe, huku polisi wakiahidi kunipigia simu wakati wowote nitakapohitajika,” alisema Nassari.

Wakati polisi wakimshikilia Nassari kwa tuhuma hizo, mbunge huyo pia alitoa tuhuma ya kushambuliwa hadi kulazwa hospitali na watu aliodai kuwa makada wa CCM siku hiyohiyo ya uchaguzi mdogo. 

Nassari alilazwa katika Hospitali ya Seliani jijini Arusha, kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam.
 
Nassari adai kunusurika kutekwa na Warsama.
Wakati polisi wakimhoji kwa shambulio dhidi ya kada huyo wa CCM, Nassari naye amedai kuvamiwa na kunusurika kutekwa na makada wa CCM, aliodai waliongozwa na Warsama Julai 14, mwaka huu.
“Julai 14, mwaka nilivamiwa na watu wakiongozwa na Warsama huyu huyu anayedai nilimshambulia. Nilitoa taarifa polisi, lakini hadi sasa hakuna hatua iliyochukuliwa,” alisema Nassari.
Alisema ingawa hajajua aina ya makosa yanayomkabili, lakini ameshangazwa na hatua ya polisi kumweka chini ya ulinzi yeye aliyepigwa na kunusurika kuuawa na wafuasi wa CCM siku hiyo ya uchaguzi.
Kamanda wa Operesheni na Mafunzi wa Jeshi la Polisi, Kamishna Paul Chagonja, aliwahi kuwaeleza waandishi wa habari jijini Arusha kuwa jeshi hilo lilikuwa linamsubiri Nassari amalize kutibiwa na kutoka hospitali ili wamhoji kuhusu tuhuma za kumshambulia kada wa CCM.
Aliporejea Arusha akitokea Jijini Dar es Salaam baada ya kutoka hospitali, Nassari aliwaeleza waandishi wa habari kuwa yuko tayari kukamatwa na polisi kujibu tuhuma hizo. Via Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top