Waziri Mkuu, Mizengo Pinda

TOZO ya sh 1,000 kwa mwezi ya laini za simu (simu card) iliyopitishwa na Bunge hivi karibuni inaitafuna serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo viongozi wake wamelazimika kuwa na ndimi mbili katika jambo walilolipanga wao, Tanzania Daima Jumapili limebaini.
Tozo hiyo haikuwa bahati mbaya bali ilipangwa na kupata baraka za vikao vya juu vya CCM na Baraza la Mawaziri kabla ya bajeti hiyo kusomwa bungeni na kupitishwa kwa kishindo na wabunge wote wa chama hicho.

Tanzania Daima Jumapili limebaini kuwa kauli za Rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu wake, Mizengo Pinda na viongozi wengine wa CCM akiwAmo Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, ni za kujaribu kupunguza jazba za wananchi na wadau mbalimbali waliopaza sauti zao kuipinga.

Katika kuthibitisha kuwa CCM walifahamu mapema tozo hiyo ni mwiba kwao, siku ya kusomwa kwa bajeti kuu ya serikali, Waziri wa Fedha na Uchumi, William Mgimwa, alilazimika kufuta pendekezo la awali katika kifungu (C ) (viii) cha marekebisho ya sheria ya ushuru wa bidhaa, sura 147, akisema kimefanyiwa marekebisho.

Kabla ya marekebisho hayo kipengele hicho kilisomeka kuwa serikali ilikuwa inapendekeza kuanzisha ushuru wa bidhaa kwa kadi za simu (simu card) kwa kiwango cha sh 1,450 kwa kadi ya simu kwa mwezi, ambapo ushuru huo utakusanywa na kampuni za simu.

Hata hivyo, Waziri Mgimwa hakusema kuwa fedha hiyo itakayokusanywa itapelekwa kwenye mfuko wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini kama Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, anavyojitetea sasa.

Mbali na tozo hiyo kwenye laini za simu, serikali pia inatoza ushuru wa bidhaa wa asilimia 14.5 kwenye huduma zote za simu za kiganjani badala ya muda wa maongezi.
Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha na Uchumi katika ushuru huo asilimia 2.5 zinatumika kugharamia elimu nchini.

Suala ambalo wananchi wengi hawajagundua ni kodi ya zuio ya asilimia 10 ya kamisheni ya usafirishaji wa fedha kwa njia ya simu za mikononi, yaani M-Pesa, Tigo-Pesa, Aitel Money na Easy Pesa.

Licha ya Waziri Mgimwa kusema ushuru wa bidhaa kwenye simu hautatozwa kwenye huduma za kutuma na kupokea fedha, tayari makali hayo yameelekezwa kwa watumiaji, kwani kampuni hizo zimeongeza tozo kwenye huduma hizo za kutuma na kupokea fedha.

Kwa mkanganyiko huo wa kauli za Rais Kikwete, Waziri Mkuu, Pinda na Nape ni wazi kuwa uamuzi huo wa kubariki tozo hizo haukuwa shirikishi kwa serikali ya CCM.

Wakati Nape akisema kuwa CCM inataka serikali ifute kodi hiyo kwa madai kuwa ni mzigo kwa walalahoi, Pinda anadai fedha hizo zitakazokusanywa zilipangwa kuingizwa REA ili kusambaza umeme vijijini.

Kauli ya Pinda inakinzana na maelezo ya Waziri wa Fedha bungeni, ambapo alisema kuwa fedha zitakazopelekwa REA ni zile za tozo mpya ya mafuta ya petroli (petroleum levy) ya sh 50 kwa lita, ambayo itakusanywa na TRA.

Mkanganyiko huu wa kauli umekuja baada ya wamiliki wa kampuni za simu kutikisa kiberiti wakiipinga kodi hiyo kuwa inawaumiza watumiaji wa simu.

Waziri Mgimwa aliibuka wa kwanza akisema kuwa watakaa na wadau hao kuona jinsi watakavyoweza kumaliza sakata hilo ambalo wanasiasa wa upinzani wamelibebea bango wakitaka lirudishwe upya bungeni.

Naye,Pinda, akiwa ziarani mkoani Ruvuma aliwaeleza wananchi kuwa kama wanasiasa wataendelea kuipinga dhamira njema ya serikali, itabidi serikali ipunguze idadi ya vijiji vilivyokuwa vimeingizwa kwenye orodha ya kupatiwa umeme na REA.

Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, ambayo Kamati Kuu yake ndiyo iliishauri serikali katika kuandaa bajeti hiyo, aliitisha mkutano na viongozi wa Wizara ya Fedha, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na wawakilishi wa kampuni za simu.

Katika mazungumzo hayo aliwapa mtihani mgumu wa kupendekeza jinsi gani ya kuziba pengo la sh bilioni 178 ambazo zitapotea katika bajeti iwapo kodi hiyo itafutwa.

Wakati Rais Jakaya Kikwete akisema kodi hiyo haiwezi kufutwa moja kwa moja bila kutafuta njia nyingine za kupata fedha za kujaza pengo hilo la sh bilioni 178 zilizolengwa kupatikana, hoja kadhaa zimeibuliwa kwa serikali na CCM.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kiuchumi wameweka bayana kuwa kauli ya Rais Kikwete inaonesha serikali haikuwa tayari kuifuta kodi hiyo licha ya kukabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wananchi.

Wanasema kuwa viongozi wa kampuni za simu hawana uwezo wa kupendekeza namna ya kuziba pengo litakalopatikana baada ya serikali kufuta kodi hiyo kwa sababu wao hawajui rasilimali zote ilizonazo serikali na utendaji wake hivyo ni kuwaweka njia panda.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye ni mtaalamu ya uchumi, alisema utaratibu wa tozo la laini za simu ni wa kuwakatisha tamaa wananchi na kuwaumiza.

Lipumba alisema haoni sababu kwa serikali kuanzisha kodi hiyo kwa kuwa imekuwa ikikusanya kodi kutoka katika kampuni za simu, hivyo kuanzisha tozo la laini ni kuwazuia watu kuwa na zaidi ya moja.

Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema kuwa katika suala hilo kuna haja ya kusikiliza kilio cha Watanzania kwa kuwa si kila sheria ni sahihi.

Dk. Bana alisema kuwa ni muhimu wanaoanzisha sheria hizo wakafanya kwanza utafiti ili kuweza kufahamu nchi nyingine zinafanyaje katika suala la mawasiliano.

Alisema kuwa si kweli kuwa kila kodi inayopatikana inaelekezwa katika mambo yanayoamuliwa, kwa kuwa kuna maeneo mengi ambayo kodi yake haifanyi kazi inayopaswa.

“Wanaposema kodi hiyo itapelekwa kuzalisha umeme vijijini si wakweli, kwa kuwa kuna maeneo mengi ambayo kodi yake haielekezwi kule kunakopaswa,” alisema.

Wakati mjadala wa tozo hizo ukiwa mkali, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Andrew Chenge, alisema licha ya idadi kubwa ya watu kupinga tozo hiyo hawakubahatisha kutoa pendekezo hilo bali walifanya utafiti wa kina na kujiridhisha kuwa ni sahihi likaanzishwa.

Matamshi ya viongozi hao yamezidi kuchochea mvurugano, mpasuko baina ya wananchi, viongozi wa serikali na makada wa CCM wanaoona kodi hiyo itachangia kukipunguzia kura chama chao katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2015.

Hata hivyo wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kiuchumi wamelidokeza Tanzania Daima Jumapili kuwa mgawanyiko huo unaonyesha mpasuko mkubwa uliopo ndani ya chama tawala, ambapo zamani waliweza kuwa na kauli moja tofauti na ilivyo hivi sasa.

Wakati hali ya mambo ikionekana kuiendea kombo CCM, mwanasiasa mkongwe wa chama hicho, Chrisant Mzindakaya, juzi aliponda malumbano ya baadhi ya viongozi wa sasa na wastaafu, akisema ni dalili ya taifa kupata viongozi wavivu siku zijazo.

Mzindakaya ambaye ni mbunge wa zamani wa Kwera, alitoa angalizo hilo wakati wa ufunguzi wa mdahalo wa changamoto za kuongoza mabadiliko ulioandaliwa na Taasisi ya Uongozi, ambapo pia alisema viongozi wamekuwa na tabia ya kuwakumbatia wageni na kuwasahau raia wao.
Chanzo: Tanzania Daima
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top