Serikali imesema msimamo
wa serikali kuanzisha tozo ya kodi
katika laini za simu hautabadilika kutokana na ulazima wa kupata fedha kwa
ajili ya kuunganisha umeme maeneo ya vijijini ambako bado watu wengi wanaishi
bila umeme.
Hayo yalisemwa jana na
Waziri Mkuu wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda
alipokuwa akihutubia wananchi na viongozi mbalimbali kwenye mkutano uliofanyika
katika viunga vya Halmashauri ya Manispaa ya Songea.
Mizengo Pinda alisema kuwa
kodi ya laini imewekwa mahususi ili kukusanya fedha ambazo zitatumika katika
kuunganisha umeme kwenye maeneo mengi hususani ya vijijini ambayo kwa sasa hayana umeme jambo ambalo alisema linakwamisha
jitihada za wananchi kujiletea maendeleo ambapo alisema kila mtumia laini ya
simu atapaswa kulipa kodi ya shilingi elfu moja kwa mwezi.
Aidha, Pinda aliwashangaa
watu wanaopinga tozo hii akidai kuwa ni ndogo kwa kuwa ni sawa na kutoza
shilingi therathini kwa siku kiasi ambacho kiko chini sana ikilinganishwa na
matumizi ya kawaida kama kuvuta sigara ambapo alisema kuwa suala la tozo katika
laini linatokana na shinikizo la wabunge kuitaka serikali itafute vyanzo vya
mapato vitakavyotumika kusambazia umeme maeneo ya vijijini.
“Serikali ilielekezwa
bungeni kuwa itafute vyanzo vyoyote vile kupata umeme vijijini…tukakaa tukaangalia
tukaona ni vema wananchi wachangie shilingi 1000 katika kila laini kiasi
ambacho kitaiwezesha serikali kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 160 kwa
ajili ya umeme vijijini”, alisema Pinda.
Hivyo, waziri Pinda
akasisitiza kuwa serikali itaendelea kukusanya kodi katika laini za simu hata kama
wananchi watalalamika lakini mwishoni lazima watalazimika kuelewa tu.
Awali Naibu waziri wa
Nishati na Madini Steven Maselle alipata wakati mgumu alipojaribu kuwaeleza
wananchi haja ya kukusanya kodi kwa kila laini ya simu ambapo wananchi waliguna
kwa nguvu kuashiria kuwa hawakubaliani na kauli hiyo jambo lililomfanya Waziri Pinda
alitolee ufafanuzi zaidi.
Uhusiano
wa Tanzania na Malawi.
Akizungumzia suala la
uhusiano wa Tanzania na Malawi Waziri Mkuu Pinda alisema kuwa kimsingi serikali
ya Tanzania haina nia wala sababu ya kuingia vitani na Serikali ya Malawi kwa
kuwa suala lililopo linaweza kupata ufumbuzi bila ya kuingia vitani ambapo
alisema kuwa kwa sasa suala hili limepelekwa katika Jumuiya ya Nchi za Kusini
Mwa Afrika (SADC) kwa usuluhishi ambako Marais wawili wastaafu wamepewa jukumu la
usuluhishi wa tatizo hili.
Kwa upande mwingine Waziri
Pinda alisema ikiwa SADC hawatafanikiwa kupata suluhisho na serikali ya Malawi
ikaamua kwenda katika mahakama za kimataifa Tanzania iko tayari kwenda
kujitetea kwa vile haioni wapi ilipoteleza.
“Hata wakipeleka suala
hili katika mahakama ya Kimataifa tuko tayari kupeleka wanasheria wetu waliobobea
tutakwenda kujieleza vizuri kwani hatuoni tulipokosea,” alisema Pinda.
Hata hivyo alionya
kuwa ikiwa atatokea mtu, kwa sababu zake mwenyewe, akaamua kuivamia Tanzania nchi
haitakuwa na budi kujitetea kwa kupambana naye kwa vile uwezo wa kupambana upo
ambapo alitolea mfano wa kilichomkuta Idd Amin wa Uganda.
Vilevile Mizengo Pinda
alisema kuwa kuna tatizo la miundombinu ya mawasiliano eneo la mwambao mwa ziwa
Nyasa ambako wananchi wanakosa taarifa za vyombo vya habari vya Tanzania na
badala yake wanapata kiurahisi zaidi taarifa za Malawi fursa ambayo Pinda alisema inaweza ikawa inatumika vibaya kwa
kuwapotosha wananchi wanaoishi pembezoni mwa ziwa Nyasa ambapo aliahidi
kulipatia ufumbuzi tatizo hili kwa kufunga mitambo itakayowezesha wananchi hawa
kupata taarifa za habari kama kawaida.
Suala
la Ujangili
Waziri Mkuu Mizengo Pinda
alisema kuwa serikali inasikitishwa na tabia ya watu kujihusisha na ujangili
katika mbuga za taifa ambapo alisema hayo yanafanyika zaidi mkoani Ruvuma katika mbuga ya wanyama ya Selous ambapo aliwashangaa watu wanaojua uwepo wa ujangili na wanawajua watu
wanaofanya ujangili lakini wanasema hakuna ujangili wakati wanyama wanazidi kuangamia.
Ndipo Pinda akasema kuwa
serikali imejipanga kuhakikisha kuwa majangili yanasakwa popote yalipo,
kunakamata na kufikishwa katika vyombo vya sheria ambapo alisema kuwa kwa sasa
serikali imeanzisha oparesheni uhai inayolenga kunusuru viumbe hai vyote na
inakusudia pia kupambana na majangili na ujangili nchini ingawa alikiri kuwa
hadi sasa oparesheni hii bado haijaanza kufanya kazi.
Vilevile Waziri Pinda
alikemea tabia ya vyombo vinavyohusika na kutoa silaha kwa wamiliki binafsi
ambapo alivitaka kuhakikisha kuwa silaha zinatolewa kwa sababu na idadi maalumu
ili kupunguza idadi ya watu wenye kumiliki silaha ambazo baadhi huishia
kutumika katika ujangili.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment