HARAKATI za Jeshi la Polisi kuishinikiza CHADEMA kuwasilisha
ushahidi unaolituhumu jeshi hilo kuhusika na mlipuko wa bomu mkoani
Arusha hivi karibuni na kuua watu wanne zimechukua sura mpya.
Jeshi hilo limemuamuru Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe,
kuwasilisha ushahidi unaohusu bomu lililolipuka katika mkutano wa chama
hicho uliofanyika viwanja vya Soweto, jijini Arusha Juni 15, mwaka huu.
Ingawa polisi imeendelea na harakati hizo, tayari CHADEMA walishakataa
kuutoa ushahidi huo kwa polisi bali wanataka Rais Jakaya Kikwete aunde
tume huru ya kijaji itakayosikiliza shauri hilo.
Tanzania Daima Jumapili limefanikiwa kupata nakala yake yenye kumbukumbu ya jalada, AR/IR/6223/2013 ya tarehe 17, Julai 2013.
Barua hiyo inamtaka Mbowe apeleke vielelezo kwa mujibu wa kifungu
namba 10 (2) na (2A) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.
Barua hiyo imesainiwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi, Hussein
Laisseri, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai.
“Kutokana na mahojiano uliyofanya na Polisi Mkoa wa Arusha mnamo Juni
20, 2013 kuhusu mauaji yaliyotokana na ulipuaji wa bomu huko Soweto,
Arusha ulidai kuwa unao ushihidi unaobainisha wahusika wa tukio hilo.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 10 (2) na (2A) cha sheria ya mwenendo wa
makosa ya jinai nchini, sura 20 kama ilivyorekebishwa mwaka 202,
unaamriwa kufika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai
tarehe 23 Julai, 2013 saa 8 mchana bila kukosa na ulete ushahidi huo,
unatahadharishwa kuwa kushindwa au kukataa kufika na kuleta ushahidi huo
ni kosa la jinai chini ya sheria iliyotajwa,” inaeleza sehemu ya barua
hiyo.
Tanzania Daima Jumapili liliwasiliana na baadhi ya wanasheria wa
CHADEMA ambao hawakutaka kutajwa majina yao, wamesema kitendo cha polisi
kumshinikiza Mbowe kupeleka ushahidi huo ni kuingilia mchakato mwingie
wa kisheria.
Walisema kuwa tayari CHADEMA wamepeleka maombi kwa Rais Jakaya Kikwete
ili aunde tume huru ya kijaji ambayo mpaka leo hajajibu ombi hilo.
Walibainisha kuwa jeshi hilo wamekosea utaratibu kisheria na kuingilia suala ambalo tayari lipo katika mchakato.
“Haiwezekani kuingilia mchakato mmoja wa kisheria kwa kutumia mchakato
mwingine wa kisheria, hii ni sub judice,” alisema mmoja wa mawakili.
Wakili huyo alisema hatua ya Jeshi la Polisi nchini kudai ushahidi wa
bomu la Arusha kwa nguvu ni ya kushangaza na hawajapata kuitumia
kushinikiza masuala mengine.
“Jeshi hilo halijawahi kumlazimisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kuwataja wauza dawa za kulevya, licha ya kusema majina anayo,
hadi sasa hajayaweka hadharani,” alisema.
Kauli ya Slaa
Barua hiyo inakuja siku chache baada ya Jeshi la Polisi kumuita na
kumhoji kwa maelezo ya onyo kuhusiana na uchochezi Mwenyekiti wa
CHADEMA, Freeman Mbowe.
Hata hivyo Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alipinga hatua
ya polisi kumhoji Mbowe kuhusu ushahidi wa Arusha kwa madai kuwa
alichokifanya mwenyekiti wao, huo si msimamo wake bali wa chama.
Dk. Slaa aliweka wazi kuwa kamati kuu ya chama hicho iliamua kuwa
ushahidi huo usiwasilishwe polisi kwa sababu ni watuhumiwa katika suala
hilo.
“Mbowe hajasema hatatoa ushahidi, atatoa lakini si kwa polisi,
tunataka tume huru ya kimahakama ya kijaji, ambayo inapaswa kuundwa na
rais, sasa rais hajasema hataunda, Jeshi la Polisi linapoanza
kulazimisha ninashindwa kuelewa uwezo wa polisi katika uelewa wa sheria.
“Tumewaeleza polisi kuwa hatutawasilisha ushahidi wetu kwao kwakuwa
kwanza sisi tunaamini kuwa wao ni watuhumiwa namba moja,” alikaririwa
Dk. Slaa.
Dk. Slaa aliongeza kuwa polisi hawakupaswa kumshika Mbowe bali kamati kuu iliyoamua kutoutoa ushahidi huo kwa polisi.
0 comments:
Post a Comment