Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe.
HOFU kubwa ya kutokea tena kwa vurugu katika uchaguzi mdogo wa
madiwani kwenye kata nne imeugubika mji wa Arusha na vitongoji vyake.
Hofu hiyo inatokana na ugumu wa uchaguzi huo pamoja na mlipuko wa bomu
uliotokea mwezi uliopita mkoani humo katika mkutano wa kufunga kampeni
za udiwani kwa CHADEMA na kuua watu wanne na kujeruhi wengine 70.
Tanzania Daima imedokezwa kuwa uchaguzi huo utakuwa na mvutano mkubwa
kwa vyama vya CHADEMA na CCM ambavyo idadi ya madiwani wao inakaribiana
sana, na ndio utakaoamua nani ataiongoza Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, CCM ilikuwa na madiwani 10 wa
kata, viti maalumu watatu na wabunge watatu na jumla yao kuwa 16.
CHADEMA nao walipata madiwani wanane wa kata, viti maalumu watatu na
wabunge watatu, jumla 14, huku TLP wakiwa na madiwani wawili.
Baada ya matokeo hayo, ulifanyika uchaguzi wa meya na naibu wake,
ambao ulitawaliwa na vurugu kubwa, huku CHADEMA wakikataa kumtambua Meya
Gaudence Lyimo (CCM).
CHADEMA waliamua kufanya maandamano ya kupinga mchakato uliomuwezesha
meya huyo kuingia madarakani na kuzuka vurugu zilizosababisha polisi
kuwaua kwa risasi watu watatu.
Tangu wakati huo hadi sasa, mji wa Arusha na viunga vyake haujapata
utulivu wa kisiasa, huku CCM ikidaiwa kuendesha harakati za kuidhoofisha
CHADEMA na Mbunge wake, Godbless Lema, anayeonekana kuwa mwiba mkali.
Hata hivyo, CCM ilipata ahueni mwaka 2011 pale CHADEMA ilipoamua
kuwafukuza uanachama madiwani wake watano kwa tuhuma za utovu wa
nidhamu.
Madiwani wanne walikuwa wa kata na mmoja wa viti maalumu. Madiwani hao
ni Diwani wa Kimandolu, Estomih Mallah, Diwani wa Elirai, John Bayo,
Diwani wa Themi, Ruben Ngowi, Diwani wa Kaloleni, Charles Mpanda na
Diwani wa Viti Maalumu, Rehema Mohamed.
CCM nayo ilipata pigo mwaka jana baada ya diwani wake wa Daraja Mbili
kufariki dunia, huku diwani wa Sombetini, Alphone Mawazo, akiamua
kujiunga na CHADEMA, na hadi sasa kata yake haijatangazwa kuwa wazi kwa
sababu ambazo hazijawekwa wazi.
Kinachogembewa
CHADEMA na CCM ugomvi wao mkubwa kwa Jiji la Arusha ni kuongoza
halmashauri hiyo na kutoa meya, hivyo uchaguzi wa keshokutwa ndio
utaamua majaliwa ya nafasi ya meya aliyepo hivi sasa anayetoka chama
tawala.
Uchaguzi huo unatarajiwa kuwa mgumu zaidi kwa pande zote mbili
kutokana na kupungua kwa idadi ya madiwani, tofauti na ilivyokuwa mwaka
2010.
Safari hii CCM ina madiwani wanane wa kata, madiwani wa Viti Maalumu watatu na wabunge watatu ambapo jumla yao ni 14.
CHADEMA wenyewe wana madiwani watano wa kata, viti maalumu watatu na wabunge watatu, ambapo jumla yao ni 11.
Kama CHADEMA itafanikiwa kurejesha kata zake nne, itakuwa na madiwani
wa kata tisa, wabunge watatu na madiwani wa viti maalumu watatu, hivyo
kufanya idadi yao kuwa 15, hivyo kuwazidi CCM kwa diwani mmoja.
Idadi hiyo itawafanya wawe na uwezo wa kuongoza halmashauri hiyo na
kutoa meya wa jiji hilo, kwani wakiingia kwenye baraza la madiwani
wanaweza kumng’oa wa CCM na kumchagua wa kutoka chama chao.
CCM wanaweza kulingana na CHADEMA kama watafanikiwa kumshawishi Diwani
wa TLP, Michael Kivuyo, kuwaunga mkono kwenye kura za umeya, hivyo
pande hizo kila moja kuwa na madiwani 15.
Kama hali itakuwa hivyo, pande hizo mbili zitalazimika kukaa kwenye
meza ya mazungumzo kukubaliana utaratibu wa kuongoza halmashauri ya jiji
kwa kupokezana kwa kipindi fulani.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wamelidokeza Tanzania Daima kuwa
uchaguzi wa kesho kutwa utakuwa mgumu zaidi kuliko ilivyowahi kutokea
huko nyuma.
Tayari kuna taarifa kuwa idadi kubwa ya viongozi wa CCM wamepiga kambi
mkoani humo kuhakikisha wanapata walau kata moja au mbili ili kuendelea
kuiongoza halmashauri ya jiji hilo ambalo ni kivutio kikubwa cha
utalii.
Ugumu wa uchaguzi huo
Ugumu wa uchaguzi huo pia unachangiwa na mlipuko wa bomu uliotokea
mwezi uliopita kwenye mkutano wa kufunga kampeni wa CHADEMA, ambapo watu
wanne walifariki dunia na 70 kujeruhiwa.
Baadhi ya watu waliozungumza na Tanzania Daima walionesha wasiwasi wao
juu ya usalama siku ya uchaguzi huku wengine wakieleza kuwa wanahofia
kujitokeza siku ya kupiga kura.
Simon John, mkazi wa Kata ya Themi alisema bado ana hofu ya kujirudia
kwa matukio ya kupigwa mabomu kama yalivyojitokeza awali.
Joyce Tumaini, mkazi wa Kimandolu alisema mlipuko wa bomu uliotokea
mwezi uliopita unaweza ukasababisha watu wachache kujitokeza kupiga
kura.
Usalama safi
Mkurugezi wa Jiji la Arusha, Sipora Liana, amewataka wakazi wa jiji
hilo kujitokeza kwa wingi kuhitimisha uchaguzi mdogo wa kata nne
zilizosalia baada ya uchaguzi huo kuahirishwa awali kutokana na mlipuko
wa bomu uliotokea Juni 16 na kuua watu wanne na wengine 70 kujeruhiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Liana alisema
hali ya usalama imeimarishwa na hakuna hofu ya kutokea milipuko katika
uchaguzi huo aliosema utaanza saa 1 asubuhi hadi saa 10 jioni.
Alitaja kata zitakazochagua madiwani wao kuwa ni Kaloleni, Themi,
Kimandolu na Elerai, huku akiainisha kuwa vituo katika kata zote ni 136
na kila kituo kitakuwa na msimamizi mmoja.
Aliongeza kuwa wapiga kura waliojiandikisha ni 60,123 na kwamba
wamekubaliana na viongozi wa vyama vya siasa mkoani humo kuwataka
wafuasi wao kuondsoka katika maeneo ya kupigia kura baada ya zoezi hilo
kukamilika kwa kila mmoja.
0 comments:
Post a Comment