Sehemu ya umati wa wananchi walioshiriki kumsikiliza Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe mjini Songea jana.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) taifa, Freeman Mbowe amesema kuwa msajili wa vyama vya siasa hapa nchini, John Tendwa hana mamlaka ya aina yoyote ya kuifuta CHADEMA kwa vile kufanya hivyo ni sawa na kuwataka wananchi wadai haki zao nje ya utaratibu rasmi jambo ambalo ni la hatari kwa ustawi wa taifa hili.

Mbowe ameyasema hayo jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Stendi ya maroli iliyopo katika eneo la Majengo mjini Songea ambapo mamia ya wakazi wa Manispaa ya Songea na wengine kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara walifika kushuhudia uzinduzi wa Kanda ya Kusini ya chama hicho inayoundwa na mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi.

Alisema kuwa binadamu yoyote pale anapodai haki yake hapaswi kuzuiliwa katika mazingira tatanishi hivyo wanachama wa CHADEMA wana haki ya msingi ya kujiwekea ulinzi wao (RED BRIGADE) kama wanachama wa Chama Cha Mapinduzi walivyojiwekea ulinzi wao kupitia vikundi vya Green Guard na sio vinginevyo.

Alisema kuwa suala la Red Brigade sio geni na wala halijaanzishwa na Mbowe bali limewekwa bayana kwenye katiba ya CHADEMA tangu mwaka 2006 ambapo linasema chama kitajiwekea ulinzi wa mali na viongozi wake hivyo kuifuta CHADEMA, kama anavyodai msajili wa vyama vya siasa nchini John Tendwa, ni kutafuta machafuko ndani ya nchi.

Alimtaka msajili wa vyama vya siasa kuona umhimu wa kuweka miundombinu ya kuwa na amani kwa kusimamia kikamilifu haki kwa vyama vyote vya siasa vilivyopo hapa nchini badala ya kuwa na upendeleo wa chama cha CCM ambacho kinaonekana kuwa na propaganda nyingi za kisiasa ambazo ni kandamizi.

Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Mbowe ameeleza kuwa kuanzia sasa CHADEMA itahakikisha kuwa inakuwa na ulinzi mkali kwa kuweka vikundi vya RED BRIGADE ambavyo vitakuwepo katika ngazi za serikali za mitaa, vijiji, tarafa, wilaya mkoa na Taifa, mbapo vitalinda usalama wa mali za chama pamoja na viongozi wao.

Alifafanua zaidi kuwa RED BRIGADE ilikuwepo tangu awali isipokuwa kwa hivi sasa kilichofanyika ni kuiongezea uwezo ambao umevifanya vyombo vya dola vishituke na kuanza kuipigia CHADEMA kelele ingawa majukumu yake ni yaleyale na yanaelekeana na vikundi vya GREEN GUARD vya CCM.

"Hivi tunaposema vijana wetu wafanye mazoezi ya ukakamavu kunakuwa na tatizo gani, mbona Green Guard wanafanya hayo lakini hawahojiwi?" alihoji Mbowe.

Vilevile Mbowe alisema kuwa vikundi vya  Green Guard vya CCM vimekuwa vikifanya matukio mengi ya kiharifu lakini jeshi la polisi limekuwa likiyafumbia macho ambapo alitoa mfano wa matukio ya uharifu ya vikundi vya Green Guard ambayo hakutaka kuyataja kuwa waharifu walikamatwa lakini wakatoroshwa katika mazingira tatanishi.

Kuhusu rasimu ya katiba amewahimiza wananchi kuwa makini wakati wanapoijadili akidai kuwa CCM inataka kuweka taratibu inazozitaka wakati Tume ya Katiba ilifanya kazi yake vizuri jambo lililoifanya CHADEMA nayo iwe na mpango wa kuwa na tume yake ya kuijadili rasimu hiyo kwa kuwaelimisha wananchi mambo halisi yanayopaswa kuwepo katika katiba mpya kwa msalahi ya taifa.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top