Naibu Waziri wa Ulimu na Ufundi, Philip Mulugo
MATOKEO mabaya waliyoyapata wanafunzi waliohitimu kidato cha nne
mwaka 2012 yamesababisha shule za sekondari za serikali kukosa
wanafunzi 10,000 waliopaswa kuanza masomo Julai 29, mwaka huu.
Kutokana na upungufu huo serikali imeamua kusitisha usajili wa shule
za sekondari za serikali na imewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote
nchini kuboresha shule zilizopo kwa kuhakikisha zinakuwa na miundombinu
bora kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo, ndiye
aliyetangaza upungufu huo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa
taarifa ya uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na kidato cha tano katika
shule za sekondari za serikali na vyuo vya ufundi.
“Mwaka jana tulisajili shule mbili za kidato cha tano na sita, ambazo
ni Miono iliyopo Bagamoyo na Tandahimba ya Mtwara… tumekubaliana mwaka
huu hatutaongeza shule nyingine, tuboreshe zilizopo kwanza,” alisema
Mulugo.
Mulugo alisema kutokana na uchache huo wa wanafunzi wenye sifa za
kujiunga na kidato cha tano, hasa wa masomo ya Sayansi ya Jamii,
serikali imeamua kutoongeza idadi ya shule za sekondari kama inavyofanya
kila mara kulingana na idadi ya wanafunzi wenye sifa za kujiunga na
shule husika.
Mulugo alisema watahiniwa 34,213 kati ya 431,650 waliofanya mtihani wa
kidato cha nne mwaka 2012 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha tano na
watakaokwenda kwenye shule 207 zilizopo hapa nchini.
Mulugo alisema idadi ya waliofaulu inajumuisha wanaokwenda kwenye vyuo
vya ufundi na Taasisi ya Menejimenti ya Maendeleo ya Maji.
Kwa mujibu wa Mulugo, watahiniwa binafsi 193 walifaulu na kati yao
watahiniwa 76 waliokuwa na sifa za kwenda kidato cha tano
hawakuchaguliwa, kwa sababu mbalimbali, ikiwamo umri zaidi ya miaka 25
huku mmoja wao akiwa si raia.
“Waliochaguliwa ni 34,213, kati yao wanaokwenda kidato cha tano ni
33,683 na ufundi ni 530, ufaulu huo ni ongezeko la asilimia 8.9
ikilinganishwa na wanafunzi 31,423 waliochaguliwa mwaka 2012.
“Kati ya hao wanaokwenda sekondari wasichana ni 10,300 na wavulana ni
23,383, hiyo ni sawa na ongezeko la wanafunzi 2,824, sawa na asilimia
9.15 ikilinganishwa na wanafunzi 30,859 waliochaguliwa mwaka 2012,”
alisema Mulugo.
Kuhusu ufaulu wa masomo ya sayansi, naibu waziri huyo alisema wavulana
wameongezeka, ambapo kati ya 23,383 waliochukua masomo ya sayansi ni
13,708 sawa na asilimia 58.62 wakati waliobaki walichaguliwa kwenye
msomo ya sayansi ya jamii.
Mulugo alisema kati ya wasichana 10,300 waliochaguliwa kujiunga na
kidato cha tano, wasichana 5,038 sawa na asilimia 48.91 walichaguliwa
kwenye masomo ya sayansi huku 5,262 sawa na asilimia 51.09 wakipelekwa
kwenye masomo ya sayansi ya jamii.
Kwa upande wa vyuo vya ufundi, Mulugo alisema waliofaulu ni 530, kati
yao wavulana ni 416 na wasichana ni 114, na kusema idadi ya wasichana
imeongezeka kutoka 47 mwaka jana, sawa na asilimia 142.55.
Akifafanua zaidi, alisema kuanzia mwaka huu wamerejesha utaratibu wa
wanafunzi wanaoingia kidato cha tano wataanza masomo wiki ya tatu ya
Julai, badala ya Aprili kama ilivyokuwa miaka minne iliyopita.
0 comments:
Post a Comment