JAJI Steven Ihema na wakili mwandamizi, Bi.
Jesse Mguto wataongoza kamati muhimu za za maadili za Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) zilizoundwa baada ya kufanya mabadiliko kwenye katiba ya
Shirikisho hilo mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais wa TFF Leodegar C. Tenga
alitangaza jana.
Shirikisho hilo pia limemteua Jaji Bernard
Luanda kuongoza Kamati ya Rufaa za Uchaguzi wakati Profesa Mgongo Fimbo
ataendelea kuongoza Kamati ya Rufaa za Nidhamu na Kamanda Mstaafu, Alfred
Tibaigana akiendelea kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu.
Rais Tenga alisema hayo wakati alipoongea
na waandishi wa habari jana kwenye ukumbi wa mikutano wa Uwanja wa Taifa mara
baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Utendaji, ambacho kikatiba kina
jukumu la kuunda Kamati Ndogo za TFF na vyombo vya maamuzi.
“Tulitaka tuwe na watu solid (imara) na
makini ambao watatuhakikishia tunakwenda vyema,” alisema Tenga akizungumzia
uteuzi huo ambao unahitimisha mchakato wa mageuzi kwenye Shirikisho baada ya
Uchaguzi Mkuu wa TFF uliopangwa kufanyika mwezi Februari kusimamishwa kutokana
na baadhi ya wagombea kupinga kuenguliwa na baadaye kwenda FIFA.
Katika kumaliza tatizo hilo, FIFA ilituma
ujumbe wake kusikiliza walalamikaji na watu wengine na baadaye kuagiza kuundwa
kwa Kamati za Maadili na kufanyika kwa Mkutano Mkuu Maalum wa TFF kwa ajili ya
kuingiza vyombo hivyo kwenye katiba kabla ya kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa
TFF.
“Tumezingatia pia maoni ya wajumbe wa
Mkutano Mkuu ambao walitaka kamati ziwe na majaji... lakini si rahisi kupata seating
judges (majaji walio kazini) ndio maana tunawashukuru wale waliotuambia kuwa
wako tayari kutusaidia.
“Tumetafuta majaji na mawakili waandamizi
ambao tunaamini watatuhakikishia haki inatendeka na inaonekana inatendeka,”
alisema Tenga na kuongeza kuwa pia walizingatia maombi ya wajumbe wengine
watatu ambao walitaka kupumzika, akiwataja kuwa ni Deo Lyatto, Sylvester Faya
na Idd Mtiginjollah.
Alisema kutokana na mfumo huo mpya, mambo
yote yanayohusu masuala ya ndani ya uwanja sasa yatashughulikiwa na Kamati ya
Nidhamu, wakati yale ya nje ya uwanja, ambayo yanawahusu viongozi na
wanafamilia ya mpira wa miguu kwa ujumla, yatashughulikiwa na Kamati za
Maadili.
Tenga alisema mabadiliko hayo pia yamegusa
kamati nyingine mbili, yaani Kamati ya Nidhamu na Kamati ya Uchaguzi ambayo
sasa itaongozwa na Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Zanzibar, Hamidu Mbwezeleni
Jaji Ihema ataongoza Kamati ya Rufaa za
Maadili akisaidiwa na mwanasheria mwingine mwandamizi, Victoria Makani, huku Bi.
Mguto, ambaye anakuwa mwanamke wa kwanza kuongoza vyombo vya vya maamuzi
ataongoza Kamati ya Maadili akisaidiwa na makamu wake Francis Kabwe, ambaye
Msajili wa Mahakama Kuu.
Katika uteuzi huo, baadhi ya wajumbe
wamehamishwa kutoka kamati moja hadi nyingine. Mhe. Murtaza Mangungu, ambaye
awali alikuwa Kamati ya Rufaa za Uchaguzi, sasa ataingia kwenye Kamati ya Rufaa
za Maadili; Kamanda Mohamed Mpinga na Prof Madundo Mtambo wamehamishwa kutoka
Kamati ya Rufaa za Uchaguzi kwenda Kamati ya Maadili.
Wajumbe wapya kwenye Kamati hizo ni pamoja
na kocha wa zamani wa Taifa Stars na Reli ya Morogoro, Mshindo Msolla na
Kamanda Mstaafu Jamal Rwambow wanaingia kwenye Kamati ya Nidhamu; mwanasheria
maarufu Evodi Mmanda anaingia kwenye Kamati ya Maadili; mwanasheria mwandamizi
Mustapha Kambona ambaye anaingia kwenye Kamati ya Nidhamu; Mhe. Mohamed Misanga
ambaye anaingia kwenye Kamati ya Maadili na Kanali Iddi Kipingu, ambaye
anasifika kwa kuendesha soka la vijana, anaingia kwenye Kamati ya Rufaa za
Nidhamu.
Pia Mwanasheria Anne Steven Marealle
anakuwa mjumbe kwenye Kamati ya Rufaa za Uchaguzi; Yohane Masale (Rufaa za
Uchaguzi), Allen Kasamala (Rufaa za Uchaguzi); Francis Kiwanga ambaye pia aningia kwenye
Kamati ya Rufaa za Uchaguzi na mkufunzi wa FIFA, Henry Tandau ambaye anaingia
kwenye Kamati ya Rufaa za Maadili.
Kamati ya Utendaji pia imefanya mabadiliko
kwenye Kamati ya Waamuzi ambako mwenyekiti Said Nassoro na katibu Charles
Ndagala wa Chama cha Waamuzi wanaingia kwenye kamati hiyo kushika nafasi ya
Joan Minja na Riziki Majala.
Wajumbe wa Kamati hizo ni kama ifuatavyo:
Kamati ya Rufaa za Maadili ni Jaji Steven
Ihema (mwenyekiti), Victoria Makani (m/mwenyekiti), Mhe. Mohamed Misanga, Henry
Tandau na Mhe. Murtaza Mangungu.
Kamati ya Maadili: Bi Jesse Mguto
(mwenyekiti), Francis Kabwe (m/mwenyekiti), ACP Mohamed Mpinga, Prof. Madundo
Mtambo, na Evod mmanda.
Kamati ya Rufaa za Nidhamu: Prof. Mgongo
Fimbo, Ong’wanuhama Kibuta (m/mwenyekiti), Kanali Mstaafu Idd Kipingu, Dk.
Mshindo Msolla, ACP Jamal Rwambow.
Kamati ya Nidhamu: Kamanda Mstaafu Alfred
Tibaigana (mwenyekiti), Mustafa Kambona (m/mwenyekiti), Azzan Zungu, Yussu
Nzowa na Mohamed Msomali.
Kamati ya Rufaa za Uchaguzi: Jaji Bernard
Luanda (mwenyekiti), Francis Kiwanga (m/mwenyekiti), A. Steven Semu, Yohane
Masalla na Allen Kasamala.
Kamati ya Uchaguzi: Hamidu Mbwezeleni
(mwenyekiti), Moses Kaluwa (m/mwenyekiti), Mustafa Siani, Hassan Dyamwale na
Kitwana Manara.
Kamati ya Waamuzi: Kapteni Mstaafu Stanley
Lugenge (mwenyekiti), Omar Kasinde (m/mwenyekiti), Said Nassoro, Charles
Ndagala na Mohamed Nyama.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment