KUCHAFUKA kwa Tanzania kimataifa ikituhumiwa kuwa ‘lango’ la
kusafirisha dawa za kulevya kumewalazimisha wanasiasa kumtaka Rais
Jakaya Kikwete kuwakamata haraka vigogo wanaohusika na biashara hiyo.
Mmoja wa wanasiasa hao, Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, Vincent
Nyerere (CHADEMA), amelazimika jana kutoa taarifa kwa vyombo vya habari
nchini akimwomba Rais Kikwete kuchukua hatua za kisheria dhidi ya
wahusika ambao aliwahi kudai anawajua kwa majina.
Nyerere ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani, katika taarifa
yake alisema Rais Kikwete ndiye aliyeutangazia umma kuwajua wahusika wa
biashara hiyo, lakini ameshindwa kuwataja, badala yake kumekuwa na
ongezeko kubwa la watu wanaojihusisha na biashara hiyo kiasi cha
kuchafua jina la nchi katika ngazi za kimataifa.
Alisema kushamiri kwa biashara hiyo haramu kiasi cha kuilazimu
serikali kutangaza kuwa janga la taifa kunatoa picha kwamba imezidiwa
nguvu na vigogo wanaoendesha biashara hiyo.
“Rais Kikwete alisema anawafahamu wafanyabiashara wa madawa ya kulevya
na alipiga hatua kubwa zaidi na kusema wamo pia viongozi wa dini,
lakini nashangaa kuona sasa hajafanya hivyo, licha ya maaskofu kumtaka
awataje hadharani,” alisema Nyerere.
Mbunge huyo alisema ukimya wa rais, huku hali ikizidi kuwa mbaya
kutokana na kuwapo kwa madai ya kukamatwa kwa wasichana wawili
Watanzania nchini Afrika Kusini wakiwa na kilo 150 za madawa ya kulevya
yenye thamani ya sh bilioni sita, kunazidi kuzua maswali mengi.
“Ukimya wa rais unaweza kuchukuliwa kuwa serikali yake haina tena
ubavu wa kupambana na wauza unga, jambo ambalo ni hatari kwa vijana
wetu,” alisema.
Mbali na kutaka rais kuchukua hatua, Nyerere pia aliwataka Waziri wa
Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said
Mwema, kuwaeleza Watanzania kulikoni hadi Tanzania inakuwa uchochoro wa
kupitisha dawa za kulevya katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.
Mbunge huyo alimtaka pia Kamishina wa Tume ya Dawa za Kulevya
kujieleza, iweje kiasi kikubwa cha dawa za kulevya katika tukio la hivi
karibuni la kukamatwa kwa wasichana hao nje ya nchi kiliweza kupitishwa
katika uwanja wa ndege bila kujulikana.
Watu wengine maarufu waliowahi kuzungumzia hatari ya biashara hiyo na
tuhuma za kuhusisha watu wazito nchini ni pamoja na Mwenyekiti wa
makampuni ya IPP, Reginald Mengi na Mbunge wa Jimbo la Mwibara, Kangi
Lugola (CCM).
Ripoti iliyotolewa mwaka jana na Tume ya Kupambana na Dawa za Kulevya
ilibainisha kuwa kati ya mwaka 2008 na 2012, watuhumiwa 10,799
walikamatwa na dawa za kulevya hapa nchini, wengine 240 wakikamatwa na
dawa hizo katika nchi za Brazil, Pakistan, China na Afrika Kusini, jambo
ambalo limetia dosari kubwa katika jumuiya ya kimataifa.
Via Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment