Mwendesha mashtaka mkuu wa Misri, ameagiza kukamatwa kwa kiongozi mkuu wa kundi la Muslim Brotherhood Mohammed Badie. Kiongozi huyo amelaumiwa kwa kuchochea ghasia zilizotokea mjini Cairo ambapo watu 51 waliuawa.
Amri ya kuwakamata viongozi wengine wapatao 100
wa kundi la Brotherhood imetolewa. Baadhi wamewekwa kizuizini. Agizo la
sasa linajiri wakati Waziri Mkuu mteule yuko mbioni kuteua serikali mpya
baada ya kuondolewa madarakani kwa Mohammed Morsi.
Kundi
la Muslim Brotherhood anakotokea Morsi limelaani muingilio wa jeshi la
kutaja kitendo hicho kama mapinduzi. Wafuasi wake wamekua wakiandamana
kila siku nje ya msikiti wa Rabaa Al-Adawiya wakitaka Morsi arejeshwe
madarakani.
Chama cha kisiasa cha vuguvugu hilo, Freedom and
Justice Party kimesema hakitajiunga na utawala wa mpito na kimekataa
wadhifa wa uwaziri kilichotengewa na Waziri MKuu Hazem al-Beblawi.
Msemaji wa Muslim Brotherhood Gehad El- Haddad
ameambia vyombo vya habari kwamba amri ya kumkamata Badie ni njama za
jeshi kuzima maandamano. Kundi hilo limelaumu jeshi kwa kuwafyatulia
risasi waandamanaji wakati wakifanya maombi nje ya kambi kuu ya jeshi.
Kwa upande wake, jeshi limesema lilikua likijibu
shambulio kutoka kwa waandamanaji waliokuwa na silaha. Makabiliano ya
Jumatatu yalipelekea kuawa kwa zaidi ya wafuasi 50 wa Muslim
Brotherhood.Kaimu Rais wa Misri, Adly Mansour ametangaza ratiba inayotoa
muelekeo wa uchaguzi mpya nchi hio.
Hii ni pamoja na kufanyia marekebisho katiba
iliyosimamishwa na jeshi na uchaguzi mkuu kufanyika mapema mwakani.
Kwanza itaanza kura ya maoni dhidi ya rasimu ya katiba, uchaguzi wa
bunge na baadaye uchaguzi wa Rais mpya mapema mwaka 2014.
Muungano wa upinzani wa National Salvation Front
(NSF) ambao ulioongoza maandamano yaliyomuondoa madarakani Mohammed
Morsi umepinga mpango wa sasa na kusema haukushauriwa. Muslim
Brotherhood imepinga mpango wowote wa kuweka utawala mpya kando ya Bw
Morsi.
Chanzo: BBC Swahili
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment