Tume ya Mabadiliko ya Katiba jana katika tukio la kihistoria ilizindua rasimu ya Katiba Mpya itakayojadiliwa na Mabaraza ya Katiba kabla ya wananchi kupiga kura ya maoni kuikataa au kuikubali rasimu hiyo. 

Iwapo wananchi watapitisha rasimu hiyo, Bunge la Katiba litakaloundwa na wabunge wa Bunge la Muungano, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wajumbe watakaoteuliwa na Rais wa Jamhuri litakaa na kupitisha Katiba Mpya.
Rasimu hiyo ya Katiba Mpya iliyozinduliwa jana na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji mstaafu Joseph Warioba ilizingatia maoni yaliyotolewa na wananchi wakati wa mchakato wa kukusanya maoni. 

Kazi kubwa ya wajumbe wa Tume hiyo ilikuwa ni kuzunguka nchi nzima, ambapo maoni ya watu 1,015,564 yalikusanywa kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na waliohudhuria mikutano ya moja kwa moja, waliotuma ujumbe mfupi wa simu (sms), barua pepe na kutumia mitandao ya kijamii.
Rasimu hiyo ina mapendekezo ya Tume kuhusu masuala mbalimbali ambayo wananchi walitaka yaingizwe katika Katiba Mpya. Kama tulivyosema hapo juu, rasimu hiyo imepatikana baada ya Tume hiyo kuchambua kwa kina maoni hayo yaliyotolewa na wananchi kwa njia mbalimbali. 

Bila shaka haikuwa rahisi kwa Tume kufanya uchambuzi wa maoni hayo kutokana na ukweli kwamba baadhi ya maoni kuhusu masuala nyeti ya kitaifa yalikuwa yakikinzana, hivyo Tume ilibidi ifanye uamuzi mgumu wa kuainisha maoni hayo na kutoa mapendekezo kwa kuzingatia wakati tuliomo, uzoefu wa mataifa mbalimbali na masilahi ya taifa letu.
Hatua inayofuata sasa ni mijadala ya rasimu hiyo katika Mabaraza ya Katiba itakayojadili mapendekezo ya tume hiyo, ambayo sisi wa Mwananchi tunadhani ni mapendekezo mazuri yatakayoipatia nchi yetu Katiba bora. 

Tangu kuanza kwa mchakato wa kupata Katiba Mpya tumekuwa tukiwaomba wananchi kupitia safu hii kutoa ushirikiano kwa Tume hiyo, tukisisitiza kwamba Tume hiyo imeundwa na wajumbe wenye uadilifu mkubwa na wenye rekodi ya utumishi uliotukuka. Tulisema wajumbe hao wako juu ya udini na itikadi za kisiasa, hivyo wangezingatia tu matakwa na masilahi ya taifa katika kufanya kazi yao.
Tulifarijika jana kuona Tume hiyo ikizindua rasimu yenye mapendekezo ya kuleta utengamano badala ya utengano katika taifa letu. Ni mapendekezo ya kuboresha hali ya Muungano, umoja, amani, haki za binadamu, demokrasia, utawala bora na kadhalika.
Ni mapendekezo yanayoruhusu mabadiliko katika mfumo wa utawala, muundo wa Muungano, Bunge, Serikali, Mahakama na ushiriki wa wananchi katika uongozi wa nchi, ikiwa ni pamoja na haki ya kila mtu kugombea nafasi ya uongozi kuanzia ngazi ya chini hadi urais. Kwa maneno mengine, mgombea binafsi sasa ruksa.
Tume pia imependekeza kuwapo serikali tatu. Madaraka ya rais yapunguzwe kama ilivyo kwa mambo yanayohusu Muungano ambayo sasa imependekezwa yabakie saba tu. Imependekezwa uwepo ukomo wa ubunge na Viti Maalumu vifutwe. Yapo pia mapendekezo kuhusu muundo wa Tume ya Uchaguzi, Msajili wa Vyama vya Siasa, mawaziri kutokuwa wabunge na mapendekezo mengine mengi.
Ni matumaini yetu kwamba Mabaraza ya Katiba yataepuka udini na itikadi za kisiasa katika kujadili mapendekezo hayo. Ni matumaini yetu pia kwamba katika mchakato mzima wa kupata Katiba Mpya hakuna mwananchi atakayepoteza, wananchi wote wataibuka washindi. 
Mwananchi 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top