Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiinua juu na kunyesha Kitabu cha
Rasimu ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwa ni
ishara ya uzinduzi rasmi wa rasimu hiyo uliofanyika leo Juni 03, 2013
katika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam. Kulia ni Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda, (kushoto) ni Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
Mpya, Joseph Sinde Warioba.
TUME ya Mabadiliko ya Katiba jana ilitoa rasimu ya mapendekezo
ya katiba mpya ambayo imesheheni masuala mazito ambayo kama
yatapitishwa, yataleta mabadiliko makubwa ambayo yamekuwa yakipiganiwa
kwa zaidi ya miaka 20.
Miongoni mwa mambo makuu yaliyoingizwa katika rasimu hiyo ni mfumo
mpya wa Muungano wa serikali tatu; serikali ndogo ya mawaziri 15; Tume
Huru ya Uchaguzi; spika na naibu wake wasio wabunge wala viongozi wa
vyama vya siasa.
Mengine yaliyoingizwa ni kumnyang’anya rais madaraka ya kuteua peke
yake viongozi wa ngazi za juu. Tume inapendekeza kwamba rais adhibitiwe
katika kuteua mawaziri na manaibu wao, majaji na manaibu wao, wakuu wa
vyombo vya ulinzi na usalama na makatibu wakuu na manaibu wao.
Imependekeza rais asaidiwe na vyombo kadhaa katika uteuzi huo.
Mawaziri watakaoteuliwa na rais hawatashika nyadhifa zao hadi
waidhinishwe na Bunge. Vile vile, rais atateua majaji kutoka miongoni
mwa majina yatakayopendekezwa kwake na Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Tume imependekeza liundwe Baraza la Ulinzi na Usalama litakalomshauri
rais kuhusu uteuzi wa wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Zaidi ya hayo, kinga ya rais kutoshitakiwa imependekezwa ibaki pale
pale, ingawa Bunge lina mamlaka ya kumshitaki kama ilivyo sasa.
Rasimu pia imependekeza umri wa mgombea urais ubaki miaka 40 ya sasa.
Katika uchaguzi, rais atatangazwa mshindi iwapo atakuwa amepata zaidi ya
asilimia 50 ya kura zote; na matokeo yake yatahojiwa mahakamani ndani
ya mwezi mmoja tangu yalipotangazwa.
Mbali na kurejeshwa kwa taifa la Tanganyika, tume imependekeza pia
mgombea binafsi aruhusiwe katika ngazi zote, kuanzia kitongoji hadi
Ikulu.
Akisitiza umakini uliotumika kuchakata mapendekezo yaliyokusanywa kwa
wananchi tangu Aprili mwaka jana, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Jospeh
Warioba alisema wamezingatia maslahi ya taifa na mahitaji ya wakati
katika kila eneo.
Rasimu ya katiba mpya ina ibara 240. Katiba ya sasa ina ibara 152.
Mwanzoni kabisa, rasimu inapendekeza tunu za taifa ziwe sehemu ya
katiba. Zilizopendekezwa ni utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi,
uwajibikaji na lugha ya taifa - Kiswahili.
Misingi mikuu ya taifa iliyopendekezwa itajwe na katiba ni uhuru,
haki, udugu, usawa, umoja, amani na mshikamano. Misingi ya awali katika
katiba ya sasa ni uhuru, haki, udugu na amani.
Muungano
“Haikuwa kazi rahisi katika suala la Muungano, tulipata maoni mengi…
ilituchukua muda mrefu sana, wapo waliotaka tuuvunje na waliotaka
serikali nne.
“…Wote walikuwa na hoja za msingi, baada ya uchambuzi wa kina tumekuja
na mapendekezo ya serikali tatu ambazo ni Serikali ya Zanzibar,
Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Muungano,” alisema Jaji Warioba.
Aidha, rasimu imepunguza idadi ya masuala ya Muungano kutoka 22 ya
awali hadi saba ambayo ni Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Ulinzi na Usalama, Uraia na Uhamiaji, Sarafu na Benki Kuu,
Usajili wa Vyama vya Siasa, Mambo ya Nje na ushuru wa bidhaa na mapato
yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya Muungano.
Rasimu hiyo ya katiba imependekeza kuwepo kwa mgombea binafsi kwa
ngazi zote, wagombea urais wawe na miaka kuanzia 40, pia imeshauri
matokeo ya uchaguzi wa rais yanaweza kulalamikiwa mahakamani ambapo kesi
hiyo itamalizika ndani ya siku 30.
“Sio kila mtu anaweza kufungua kesi, wanaoweza kufanya hivyo ni
waliogombea urais,” alisema mwenyekiti huyo na kuongeza kwamba rais
aliyeshinda ataapishwa siku 30 baada ya kutangazwa.
Kuhusu madaraka ya rais tume hiyo imependekeza kuwa rais aendelee
kuwateua viongozi wa ngazi za juu ambao ni mawaziri na manaibu wao kisha
watathibitishwa na Bunge.
Aidha, uteuzi wa Jaji Mkuu na naibu wake utafanywa na rais kutokana na
majina yatakayopendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama halafu Bunge
litayathibitisha.
“Kuhusu makatibu wakuu na manaibu wao watateuliwa na rais kutokana na mapendekezo ya Tume ya Utumishi wa Umma.
“Tumependekeza pia rais aunde serikali ndogo iliyo na mawaziri
wasiozidi 15, pia mawaziri hao si wabunge, hivyo hawatahudhuria vikao
vya Bunge isipokuwa kama watahitajika kutoa ufafanuzi kwenye kamati za
Bunge,” alisema.
Kuhusu Bunge
Rasimu hiyo imependekeza kuwepo na wabunge wa kuchaguliwa na wachache
wa kuteuliwa na rais kuwakilisha watu wenye ulemavu huku ikifuta uwepo
wa viti maalumu.
Aidha, imependekeza pia ukomo wa ubunge uwe vipindi vitatu vya miaka
mitano na kwamba wananchi wanaweza kumwondoa mbunge wao madarakani.
Rasimu hiyo imebainisha kuwa mbunge akifukuzwa chama ataendelea na
wadhifa huo isipokua atakapohama chama ndipo atakapopoteza ubunge wake.
Jaji Warioba alisema tume yake imependekeza kutokuwepo kwa chaguzi
ndogo badala yake chama kilichopoteza mbunge kwa namna yoyote kitamweka
mtu mwingine.
“Tume yetu imependekeza Spika wa Bunge na naibu wake wasitokane na
wabunge, pia wasiwe viongozi wa vyama vya siasa,” alieleza na kuongeza
kwamba walifanya kazi kwa kuzingatia hadidu za rejea.
Tume ya Uchaguzi
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, tume yake imependekeza kuwapo kwa Tume
Huru ya Uchaguzi ambayo sifa za wajumbe wake zitaainishwa kwenye katiba
mpya.
Aidha, wajumbe hao wataomba na majina yao yatachambuliwa kwenye Kamati
ya Uteuzi itakayoongozwa na majaji wakuu wa nchi washirika wa Muungano
ikiwa na wajumbe sita.
Wajumbe hao ni Spika wa Bunge la Muungano, Spika wa Baraza la
Wawakilishi, Spika wa Bunge la Tanganyika na Mwenyekiti wa Tume ya Haki
za Binadamu na Utawala Bora.
“Kamati hiyo itapeleka kwa rais majina ya watu wanaofaa kuwemo kwenye
Tume Huru ya Uchaguzi, hivyo rais atateua mwenyekiti, makamu na wajumbe
wake kutoka kwenye majina hayo….
“Tume hiyo itasimamia masuala ya uchaguzi, kura ya maoni na usajili wa vyama vya siasa,” alisema Jaji Warioba.
Mahakama
Rasimu ya katiba mpya imependekeza kuwepo kwa Mahakama ya Juu
(Supreme Court) ambapo majaji wa juu wa Mahakama ya Rufani watateuliwa
na rais baada ya kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Mambo ambayo hayakuingizwa
Miongoni mwa mambo ambayo hayakuingizwa katika rasimu ni serikali za
majimbo, mahakama ya kadhi, wakuu wa mikoa na wilaya, serikali za mitaa,
na uraia wa nchi mbili.
Akifafanua kuhusu kuachwa kwa masuala hayo, Jaji Warioba alitoa sababu
kadhaa, ambazo hata hivyo zitaendelea kujadiliwa katika mabaraza ya
katiba, kabla ya kuhitimisha kama yaingizwe au yaachwe kabisa.
Kuhusu serikali za majimbo, alisema tume ilizingatia suala la ukubwa
wa gharama, hasa kwa kuwa tayari imeshakubali serikali tatu.
Alisema sababu nyingine ni hisia za ubaguzi wa kidini, kikabila na kikanda ambazo zimeanza kujitokeza.
Akizungumzia mahakama ya kadhi, alisema si suala la Muungano, bali
nchi washirika; na kwamba kama Tanganyika ikitaka inaweza kujifunza
kutoka Zanzibar ambako wamekuwa na mahakama hiyo ikifanya vizuri bila
kuiingiza kwenye katiba.
Alisema masuala ya wakuu wa mikoa na wilaya na serikali za mitaa
yatashughulikiwa na serikali husika, Bara au Zanzibar, kwani si ya
Muungano.
Kuhusu uraia wa nchi moja au mbili, alisema waliliacha suala hilo kwa
maana kuwa linaweza kuwekwa kwenye sheria ya uraia badala ya kuingizwa
kwenye katiba.
Mengi ya yaliyoingizwa kwenye rasimu ni yale ambayo wanasiasa na
wanaharakati wamekuwa wakipigania kwa miaka zaidi ya 20 tangu kuruhusiwa
kwa demokrasia ya vyama vingi.
0 comments:
Post a Comment