KAMA Watanzania wataridhia rasimu ya katiba mpya ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania iliyozinduliwa wiki iliyopita na Tume ya Mabadiliko
ya Katiba bila mabadiliko, itapiga marufuku Rais wa Tanzania
kujihusisha kwa namna yoyote na chama chochote cha siasa kikiwemo chama
chake, Tanzania Daima Jumapili limebaini.
Pendekezo hilo limo katika Ibara ya 69 ya rasimu hiyo inayobainisha
madaraka na majukumu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa
Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu.
Ibara ya 69(4) ya rasimu hiyo inabainisha kuwa: “Katika kutekeleza
majukumu yake kwa mujibu wa ibara hii, rais ataepuka kujinasibisha, kwa
namna yoyote ile, na chama chochote cha siasa au kundi lolote kwa namna
ambayo inaathiri umoja wa wananchi.”
Katika ibara inayotangulia, ya 68(2) Rais wa Jamhuri ya Muungano
ametajwa kuwa atakuwa Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi
Mkuu, na kwa mamlaka hayo kwanza atakuwa alama na taswira ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na watu wake, pili atakuwa alama ya umoja na uhuru
wa nchi na mamlaka yake na mwisho atakuwa na dhamana ya kukuza na
kuhifadhi umoja wa kitaifa.
Lengo la kuwekwa marufuku hiyo limebainishwa wazi na ibara yenyewe
kuwa ni kulinda umoja wa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
umoja wa kitaifa kwa ujumla.
Kama rasimu hiyo itapitishwa katika kura ya maoni mwakani, rais
hataruhusiwa kushiriki katika mikutano ya kawaida ya hadhara, katika
mikutano ya kampeni za uchaguzi au shughuli nyingine yoyote ya chama
chake, isipokuwa vikao vikuu vya maamuzi vya chama chake.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema kuwa kama kifungu hicho
kitakubaliwa kama kilivyo, litakuwa pigo kubwa kwa chama tawala nchini -
Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kimekuwa kikiwatumia wanachama wake
ambao ni viongozi wa serikali, akiwemo rais kujinufaisha kisiasa.
Kwa muda mrefu tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa
nchini, vyama vya upinzani vimekuwa vikiwalalamikia viongozi wa serikali
kutumia nafasi zao serikalini kufanya kazi za siasa za CCM, hususan
nyakati za uchaguzi.
Viongozi wa serikali ambao wamekuwa wakilalamikiwa ni pamoja na Rais
wa Jamhuri ya Muunagno wa Tanzania, mawaziri, wakuu wa mikoa na wakuu wa
wilaya ambao wamekuwa wakitumia nafasi zao serikalini kuifanyia kampeni
CCM kwa kutumia rasilimali za umma.
Aidha, kumekuwepo malalamiko kama hayo dhidi ya marais wastaafu,
akiwemo mwasisi na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ambaye katika
uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi wa mwaka 1995, alisimama
kumfanyia kampeni aliyekuwa mgombea urais wa CCM, rais mstaafu Benjamin
Mkapa.
Kilicholalamikiwa zaidi ni kauli yake kwamba; “siwezi kuiachia nchi
yangu ikichukuliwa na mbwa” iliyowakera viongozi wa upinzani kwa
kufananishwa na mbwa, hususan aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya
Chama cha NCCR-Mageuzi, Augustino Mrema aliyekuwa akipewa nafasi kubwa
ya kushinda.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema kwa kiasi kikubwa kauli hiyo
ya Mwalimu Nyerere iliathiri na kuteteresha heshima yake mbele ya umma
wa Watanzania.
0 comments:
Post a Comment