Mbunge wa Mtwara Mjini, Hasnain Murji akichangia hoja bungeni. Mbunge huyo anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kuchochea vurugu za gesi Mtwara.
  
Jeshi la Polisi mkoani Mtwara limemkamata mbunge wa Mtwara Mjini (CCM), Hasnain Murji likimtuhumu kuchochea vurugu za kupinga mradi wa bomba la gesi kutoka mkoani humo kwenda jijini Dar es Salaam.
 
Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Msemaji wa Jeshi la polisi nchini, Advera Senso zinaeleza kuwa Murji alikamatwa jana jioni nyumbani kwake maeneo ya Shangani mjini Mtwara.
Kukamatwa kwa mbunge huyo kunakuja ikiwa zimepita siku tano tangu viongozi wanne wa vyama vya upinzani mkoani Mtwara, kufikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara, Juni 4, mwaka huu wakikabiliwa na mashtaka matatu ikiwamo kula njama, kufanya uchochezi na kuamsha hisia mbaya kwa wakazi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Washtakiwa hao ni Katani Ahmed Katani (33) na Saidi Kulaga (45) wa CUF, Hassan Uledi (35) wa NCCR Mageuzi na Hamza Licheta (51) wa TLP, wote wakazi wa Mtwara. Taarifa zaidi zilieleza kuwa baada ya polisi kumkamata mbunge huyo, walifanya upekuzi katika nyumba yake kwa saa kadhaa na baada ya kujiridhisha walikwenda kupekua na ofisi yake.
“Amekamatwa kwenye saa 11:00 jioni, hata hati ya kukamatwa kwake imeeleza kuwa anatuhumiwa kuchochea vurugu za kupinga gesi inayopatikana mkoani Mtwara kwenda Dar es Salaam,” alisema Katibu wa Mbunge huyo, Meckland Millanzi.
Katika ufafanuzi wake Senso alisema kukamatwa kwa mbunge huyo ni jambo la kawaida na kwamba hivi sasa unaandaliwa utaratibu ili faili lake lipelekwe kwa Mwanasheria wa Serikali.
“Acheni polisi ifanye kazi yake kama kutakuwa na la ziada tutawaeleza ila kwa sasa tunaandaa utaratibu wa suala hili kwenda kwa mwanasheria wa Serikali,” alisema Senso. 

Murji amekamatwa ikiwa zimepita siku 16 tangu kutokea vurugu kubwa mkoani Mtwara zilizodumu kwa siku mbili, ambapo polisi walipambana na makundi ya vijana wanaopinga mradi wa bomba la gesi kujengwa.
Vurugu hizo zilizosababisha baadhi ya watu kupoteza maisha huku wengine wakiachwa majeruhi na mali nyingi kuharibiwa, ziliibuka baada ya hotuba ya bajeti ya wizara ya nishati na madini kusomwa bungeni .
Mvutano kuhusu mradi wa bomba la gesi ulianza Novemba 16, mwaka jana baada ya Serikali kutuma kamati inayoratibu maoni ya sera ya gesi “The Natural Gas Policy of Tanzania -2013” ambayo ilifika mkoani Mtwara kukusanya maoni ya wananchi.
Katika mikutano yake mjini Mtwara, wananchi wengi hawakukubaliana na wazo la kusafirishwa gesi nje ya Mtwara kwa njia ya bomba. Hali hiyo ndiyo iliyowasukuma viongozi wa vyama kuhamasisha wananchi kuhusu suala hilo.
Mwananchi 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top