Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
1). Kwa ujumla kupata Sera mpya ya gesi asilia ni hatua
muafaka japo imechelewa sana. Hata hivyo ni bora kuchelewa kuliko kutofika
kabisa. Ni vema wananchi wachukue fursa hii kuisoma na kuijadili rasimu hii na
kuiboresha ili iwezeshe wananchi wenyewe kufaidika na utajiri ambao nchi yetu
imejaaliwa.
2). Sera ina jumla ya sura Sita. Sura ya kwanza inaweka sababu
na masuala ya jumla na utangulizi . Sura ya pili inaweka sababu za kuwepo kwa
sera mpya na madhumuni maalumu, Sura ya tatu ndio yenye matamko ya msingi ya
kisera (fundamental policy issues) ikiwemo masuala ya miundombinu ya gesi
kwa ajili ya soko la ndani, usimamizi wa mapato yatokanayo na gesi asilia na
masuala ya ‘’ local content’’. Sura hii pia imezungumzia masuala
ya uwazi na uwajibikaji. Sura ya nne ni masuala ya mfumo wa kisheria na
udhibiti na sura ya tano ni taasisi za usimamizi wa sera ya gesi asilia. Sura
ya sita ni hitimisho. Kila sura imeweka matamko ya kisera.
3). Rasimu ya sera imeshindwa kutofautisha suala la Mafuta na Gesi
kuwa ni suala la Muungano au sio suala la muungano katika muktadha wa Katiba
mpya inayojadiliwa sasa. Hii inadhihirisha umuhimu wa kuwianisha mchakato wa
katiba na michakato mingine inayoendelea nchini. Hivi sasa Zanzibar inajiandaa
kuwa na sera na sheria yao ya mafuta ya gesi, iweje sera hii itamke gesi asilia
ni mali ya Jamhuri ya Muungano wakati upande mmoja wa Muungano utakuwa unafaidi
utajiri wake peke yake? Rasimu ya sera imeshindwa kutambua kuwa kuna vitalu vya
mafuta na gesi ya (vitalu namba 9-12) vimesimamisha shughuli kwa sababu
Serikali ya Zanziabar haitambui mafuta na gesi kuwa suala la muungano. Rasimu
inapaswa kuzingatia jambo hili kabla ya kupata sera yenyewe.
4). Rasimu imetamka katika ukurasa wa 9 kwamba sera hii
haitambui shughuli za utafutaji (‘This policy document only covers
mid-and downstream segments’ ndio nukuu ya neno kwa neno ya Sera hii).
Hiki ni kichekesho cha milenia .
Taifa linawezaje kuandika sera ya gesi asilia kwa upande wa
uchuuzi tu (biashara) na kuacha kazi yenyewe haswa ya utafutaji na uchimbaji (exploration
and exploitation are upstream). Shughuli za utafutaji na uchimbaji ndio
msingi haswa wa sera ya gesi asilia.
Mikataba yote huamuliwa kwa kuzingatia kwanza utafutaji,
shughuli nyingine ni biashara tu ya kitakachogunduliwa . Rasimu kuacha kabisa
eneo la utafutaji na uendelezaji (upstream) ni sawa na kutokuwa na sera
kabisa.
Kwa namna eneo hili lilivyoachwa kuna harufu ya mkakati wa siri
wa kuwanyima wananchi msimamo wa kisera kuhusu utajiri wao unavyonyonywa .
Sentensi hii yenye maneno 10 katika uk. wa 9 wa kijitabu cha rasimu ya sera
unaondoa kabisa umuhimu wa sera yenyewe wakati dhumuni kuu la sera linatamkwa
uk.6 kwamba Gesi asilia ni mali ya wananchi wa ‘Jamhuri ya Muungano’ wa
Tanzania’’ kurasa tatu baadaye zinaiondoa sera kwenye eneo hilo la umiliki wa
mali hii ( Upstream). Tumeamua kuandika sera ya uchuuzi wa gesi asilia?
5). Rasimu katika 3.2.2(uk.24) imeweka matamko ya kisera
kuhusu uwazi na uwajibikaji . Uwazi ndio eneo ambalo watanzania wengi walikuwa
wanasubiri kwa hamu sana . Usiri wa mikataba katika sekta mbali mbali nchini ni
chanzo cha ufisadi na uporaji wa utajiri wa mali yetu. Sera hii imeJibu swala
hili? HAPANA. Sera haisemi ni namna gani mikataba itakuwa wazi kwa wananchi.
Sera haisemi ni namna gani wananchi wataiwajibisha Serikali na vyombo vyake
(Accountability) kwenye masuala ya mafuta na gesi. Sera imepiga porojo kuhusu
uwazi na uwajibikaji. Bila misingi imara ya Uwazi na Uwajibikaji katika
rasilimali ya gesi asilia, sera haina maana yoyote ile.
6). Serikali ni lazima ijue kwamba hivi sasa nchi yetu ni nchi
tajiri yenye watu masikini.[i] Sera
ya gesi inapaswa kutuondoa kuwa nchi yenye laana ya rasilimali. Sera hii haina
mwelekeo huo kabisa . Sera inapaswa kuwezesha wananchi kupata thamani ya
maliasili yetu na kuwezesha matumizi mazuri ya mapato yatokanayo na utajiri wa
nchi.
Sera yetu lazima ioneshe dhahiri kwamba gesi asilia ni mali ya
wananchi na uendelezaji na unyonyaji wa rasilimali hii utafaidisha wananchi
kwanza na kwa ruhusa yao (Prior informed Consent Principle) sera
ni lazima itamke hilo kinagaubaga.Sera ni lazima ionyeshe kuwa katika ushindani
wa soko makampuni ya mafuta na gesi asilia yatapata faida ya halali ( normal
retuns) ya uwekezaji wao na kwamba lolote linalozidi litabakia kuwa
mali ya wananchi wa Tanzania.
Mkakati wa makampuni ya mafuta na gesi asilia ni kuhakikisha
taifa linapata kiduchu na wanasaidia serikali kutoa majibu ya kipato hicho
kiduchu. Watanzania hawatakubali tena.
7). Ni lazima tuseme kuwa tunataka utajiri wetu uwe neema kwa
wananchi wetu, na siyo laana. Maendeleo yetu yatategemea ni namna gani
tunafaidika na utajiri wetu wa maliasili kama gesi asilia. Sera ya Gesi Asilia
itujengee imani hiyo. Hii Sera (Rasimu) inapaswa iangaliwe upya na hasa maeneo
ya uwazi na uwajibikaji.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment