Rais Kikwete akifafanua jambo
Rais Jakaya Kikwete amebainisha kuwa vurugu za kidini na kisiasa zinazotokea nchini, zina uhusiano na watu wa nchi za nje.
Alitoa kauli hiyo jana kwenye ibada maalumu ya
kuwekwa wakfu kwa Askofu Mkuu wa Sita wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dk
Jacob Chimeledya.
Rais Kikwete alikuwa mgeni rasmi kwenye ibada hiyo iliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu.
“Wanaohamasisha vurugu hizo ni watu wenye uhusiano
ya karibu na watu wa nje ambao mambo yakiharibika nchini watakuwa wa
kwanza kupanda ndege, ilhali wakiendelea kutoa matamko ya uchochezi
wakiwa nje ya nchi wakati wengine wakiendelea kuumia,” alisema Kikwete.
Ibada hiyo ilifanyika chini ya ulinzi wa polisi na
askari wa usalama, na ilihudhuriwa na Askofu Mkuu wa Anglikana duniani,
Justin Welby.
Rais Kikwete alisema amekuwa akichukizwa na vurugu
za kidini zinazofanywa na baadhi ya watu wasioitakia mema Tanzania,
huku wakijua kuwa amani ikitoweka ni gharama kubwa kuipata.
“Halafu lazima watu wajue kuwa nchi hii ni yetu
sote, kama ni kubanana lazima tubanane humuhumu, lakini kwa idadi ya
wingi wa watu isiwe mbanano wa mapanga,” aliongeza Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisema vurugu zinazotokea zinafanywa
na watu wachache ambao hawana mamlaka katika taasisi za kidini, na
aliwataka viongozi wa dini zote kukemea vurugu, kuihubiri amani na
kuwakumbusha waumini wao kuipenda nchi yao.
Alirudia kauli yake kuwa Serikali haitawavumilia watu wanaoendelea kuvuruga amani ya nchi kwa kisingizio cha masuala ya dini.
“Dini zote zinahimiza upendo, hakuna dini
inayohubiri kuuana, ukiona dini inayohubiri kuuana hiyo itakuwa ni ya
shetani, dini ya kweli inahimiza upendo kwa kila mtu,” alisema Rais
Kikwete.
Awali Askofu Mkuu aliyewekwa wakfu, Dk Chimeledya
aliiomba Serikali kushughulikia changamoto za nchi ikiwamo suala la
umaskini, maradhi, ujinga na hatari ya kuporomoka amani.
Dk Chimeledya alisema kuwa rushwa, dawa za
kulevya, ufisadi na mauaji ya vikongwe ni miongoni mwa mambo
yanayoiondolea sifa Tanzania ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikijulikana
kama kisiwa cha amani.
Via Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Via Mwananchi
0 comments:
Post a Comment