TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
HALMASHAURI ZILENGE KUSAIDIA WATOTO WANAOISHI KWENYE
MAZINGIRA HATARISHI - PINDA
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema kila Halmashauri hapa nchini ina wajibu wa
kuhakikisha kuwa mipango inayowekwa inalenga kusadia watoto walio katika
mazingira hatarishi.
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Februari mosi, 2013) wakati mamia ya wazazi na
wanafunzi walioshiriki uzinduzi wa Mpango Kazi wa Pili wa Taifa wa Watoto walio
katika Mazingira Hatarishi uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Mpango
Amesema
wadau wakuu katika kutekeleza mpango kazi huo wa miaka mitano (2013 -2017) ambao
ni Halmashauri zote nchini, Serikali Kuu, Bunge, Mahakama, washirika wa
maendeleo, asasi zisizo za kiserikali na madhehebu ya dini wana mchango mkubwa
wa kuhakikisha hali za watoto hao zinabadilika.
“Kila Halmashauri itekeleze wajibu
inavyotakiwa. Wenyeviti wa Serikali za Vijiji, Madiwani ni lazima tuhakikishe
mipango yetu inalenga kusaidia watoto walio katika mazingira hatarishi,”
alisema.
Waziri Mkuu alisema wadau wengine
wakuu katika kutekeleza mpango kazi huo ni Serikali Kuu ambapo alizitaka Wizara
Mtambuka zinahusika na suala hili zijipange kuhakikisha mpango huo unatekelezwa
na kusaidia kubadilisha maisha ya watoto hao.
Alisema Bunge
kwa upande wake, ambalo liliwakilishwa kwenye uzinduzi huo na wajumbe wa Kamati
ya Bunge ya Huduma za Jamii, litasaidia kuhakikisha fedha inayopangwa inapatikana
kwa wakati na inatumika vizuri.
Akisisitiza
kuhusu jukumu la kulea na kutunza watoto ni la kila mmoja, Waziri Mkuu alisema:
”Watanzania mmoja mmoja ni lazima tuonyeshe upendo kwa watoto kwa sababu mtoto
wa mweinzi ni mtoto wako. Usimuone mtoto wa mwenzio anafanyiwa ukatili au ana
hali mbaya ukasema shauri yake, huyu si wa kwangu”.
Alizitaka pia
Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii zikae pamoja na
kuwaita wadau wake ili ziweze kujadiliana njia bora ya kutoa huduma vizuri
zaidi kwa jamii wanazozihudumia kwenye mikoa mbalimbali badala ya kuachia asasi
nyingi kuwa zimejirundika katika mikoa michache tu.
Mapema
wakisoma risala yao, watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu walisema tangu
mpango huo uanze mwaka 2007, wamenufaika kwa kupatiwa vifaa vya shule, sare za
shule, mablanketi na ada.
Walisema
mpango huo umewasaidia kuwafanya wajiamni wawapo shuleni tofauti na hapo awali
ambapo wenzao walikuwa wakiwadhihaki na kuwatenga kwa kukosa sare au kuwa
wachafu wawapo shuleni kwani hawakuwa na nguo za kubadilisha.
Walitumia fursa
hiyo kuomba wanapofaulu, wapatiwe nafasi za bweni ili wawe na uhakika wa
kumaliza shule, wasidaiwe michango mbalimbali shuleni na wakipata nafasi ya
kwenda elimu ya juu, wapatiwe ufadhili na serikali kwa asilimia 100.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
IJUMAA,FEBRUARI MOSI, 2013.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment