Watumishi
wa Serikali, kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, kuanzia Septemba
mwaka huu wataanza kunufaika na mikopo nafuu ya ujenzi wa nyumba za kuishi
chini ya utaratibu mpya ulioandaliwa na Serikali na unaojulikana kama Mpango
Maalum wa Nyumba za Kuishi za Watumishi wa Umma – Public Servant Housing Scheme.
Mpango
huo ulitangazwa , Ijumaa, Mei 17, 2013 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete wakati wa hotuba yake ya kufunga
Wiki ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwenye bustani ya Nyerere Square mjini Dodoma.
Hata
kabla ya kuutangaza Mradi huo hadharani mjini Dodoma, Rais Kikwete
alikwishakuambiwa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Profesa Beno Ndullu kuwa
chini ya Mpango huo, watumishi wa Serikali kuanzia Septemba mwaka huu wataweza
ama kukopa nyumba za gharama nafuu ama
kukopa mikopo ya gharama nafuu ambayo italipwa katika kipindi cha miaka 25.
Gavana
Ndullu alikuwa Mwenyekiti wa Kamati Maalum iliyoteuliwa na Rais Kikwete
kuangalia jinsi gani ya kuwasaidia watumishi wa Serikali katika Tanzania kuweza
kupata mikopo nafuu ama kukopa nyumba za bei nafuu ambayo iliwasilisha ripoti
yake kwake katika mkutano uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam katikati ya wiki
iliyopita.
Chini
ya mpango huo, ambao utaendeshwa na kampuni iitwayo Watumishi Housing Company
Limited iliyoandikishwa na kupewa usajili Februari mwaka huu, 2013, kiasi cha
nyumba 5,000 zitajengwa katika miaka ya kwanza mitano, mwaka wa kwanza zikiwa
zimejengwa nyumba 2,500.
Mpaka
sasa kiasi cha Sh. bilioni 68 zimekwishapatikana kati ya kiasi cha Sh.bilioni
358 zinazotarajiwa kuwekezwa katika Mradi huo katika miaka hiyo mitano ya
mwanzo na itakuwa ni kampuni hiyo ambayo itajenga nyumba za gharama nafuu na
kuwezesha kupatikana kwa mikopo nafuu kwa watumishi ambao watapendelea kukopa
fedha ili kujenga wenyewe nyumba za kuishi.
Taasisi
zitakazoshiriki katika kampuni hiyo ni pamoja na mifuko ya Hifadhi ya jamii ya
NSSF, PPF, PSPF, LAPF, GEPF, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) pamoja na Mfuko
wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Mbali
na taasisi hizo, pia benki 10 zimekubali kushiriki katika Mradi huo. Mabenki
hayo ambayo yatakuwa yanatoza riba ya kati ya asilimia 10 na 13 kwa miaka yote
25 ya mkopo ni NMB, CRDB, NBC, Bank of Africa, Azania Bank, EXIM Bank, Banc
ABC, NIC Bank, DCB Bank na KCB.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
1 comments:
Ni vema pia mkatuelekeza tufanyeje ili tupate mikopo hii kwa sababu tunasikia tu hatuelewi pakuanzia ni wapi
Post a Comment