VURUGU zilizofanyika hivi karibuni mkoani Mtwara zimechukua sura mpya, baada ya mambo mazito yenye sura ya kinyama ndani yake kuibuliwa. 

Utafiti uliofanywa na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’s), umebaini watu zaidi ya 12 wamepoteza maisha katika vurugu hizo tofauti na takwimu za watu watatu wanaotajwa na Serikali. 

Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kwa kushirikiana na Mtandao wa Haki za Binadamu Kusini Mwa Afrika (SAHRINGON).

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Harold Sungusia alisema utafiti huo wa muda mfupi umebaini kasoro katika takwimu za Serikali kuhusiana na vifo vya watu.

Sungusia alisema utafiti uliofanywa na shirika lake umebaini kuwapo kwa vitendo vya ubakaji wa wanafunzi wa vyuo, huku wazee wa kimila wakidaiwa kuchinja mbuzi za tambiko kupinga ujenzi wa bomba kwa ajili ya kusafirisha gesi.

Vifo
Sungusia alidai kuwa wamebaini vifo vilitokea katika vurugu hizo ni zaidi ya 12 na kwamba shirika lake linaendelea kuhakiki majina ya watu waliofariki dunia na taarifa zao nyingine.

Sungusia alitoa shutuma nzito kwa askari polisi kwamba ndio waliohusika na ongezeko la vifo hivyo.

“Hivi vifo ni kutokana na askari polisi kuvamia nyumba za wananchi, kuvamia maduka na kuingia ndani na kupiga mabomu ya machozi, huku wakiiba mali za raia zikiwamo televisheni, redio na fedha,” alisema.

Alisema timu ya watafiti hao inaendelea kuzungumza na wazazi na familia zilizopoteza ndugu zao ili kuwa na uhakika wa majina yao, umri na maeneo walipozikwa.

Sungusia alisema katika hali isiyo ya kawaida, taasisi za Serikali zikiwamo hospitali na polisi zimeshindwa kutoa ushirikiano wa karibu pale walipotakiwa kutoa taarifa halisi kuhusu madhara ya vurugu hizo.

“Tumezungumza na baadhi ya wakazi wa Mtwara juu ya mambo mbalimbali kuhusu gesi na athari zilizotokea katika vurugu za hivi karibuni.

“Walieleza ndugu zao waliokufa na baadhi tumepata majina yao, tutayaweka baada ya kukamilisha taarifa zote,” alisema.

Matambiko ya kimila
Alisema kuwa katika vurugu hizo zilizotokea, wamebaini kuwa tayari baadhi ya wazee maarufu wa kimila wamekwishafanya matambiko yao na kuwapa vijana imani ya kuapishwa juu ya kutetea na kulinda rasilimali za Mtwara zisitoke bila wao kuridhia.

“Tumezungumza na wazee wa kimila na wakakiri kwamba walikwishafanya matambiko yao na kutoa mbuzi wawili kama kafara, mbuzi mmoja alichinjwa wakanywa damu na wa pili alipelekwa eneo lenye gesi na kufanya matambiko yao.

“Katika matambiko yao walikubaliana kama mbuzi huyo akipiga magoti, basi gesi hiyo haitatoka Mtwara na kama angesimama ingeashiria inatoka. Wanasema mbuzi wao alipiga magoti.

“Pia tumeelezwa kwamba, vurugu hizo zilichochewa na taarifa zilizotolewa na wavuvi wanaovua kina kirefu cha bahari kwamba, kuna meli imetia nanga baharini na inavuna gesi na inaipeleka ng’ambo kupitia Nyambizi yaani Sub-marine.

“Kutokana na hali hiyo, wananchi wa Mtwara walianza kuhamasishana mjini hadi vijijini na kuwa na msimamo wao wa lugha ya kimakonde kama ‘AIYUKI’ yaani haitoki,” alisema.

  Ubakaji
Sungusia alisema wanafunzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma, Chuo cha Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na Chuo cha Mtakatifu Augostine ni miongoni mwa watu walioathiriwa.

Alisema wanafunzi hao walivamiwa na polisi wakiwa njiani wakienda mjini kujifunza kwa vitendo ‘field’ na kufanyiwa vitendo hivyo vibaya.

Alisema licha ya wananchi wa Mtwara kushukuru askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kurejesha amani, lakini wameendelea kuwa na hofu kubwa.

CUF kukutana na Wanamtwara
Wakati huo huo Chama cha Wananchi (CUF), kimeandaa kongamano kubwa kwa ajili ya wananchi wanaotoka Mtwara na Lindi waishio jijini Dar es Salaam, ili kujadili kwa uwazi tukio la Mtwara.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam na waandishi wa Habari Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alisema kongamano hilo litafanyika Juni 2, mwaka huu.

Alisema CUF imeamua kufanya kongamano hilo, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi wakilalamikia hatua ya Serikali kutosikiliza kilio chao.

“Baada ya majadiliano ya kina mawazo ya wananchi yatakusanywa kisha kupelekwa kwa Rais Jakaya Kikwete pamoja na Spika wa Bunge, Anne Makinda ili waweze kuyachambua nao kwa nafasi zao na kuyachukulia maamuzi,” alisema Mtatiro.

Alisema kuwa chama chake kinafanya hivyo kutokana na vyama vya siasa kuzuiwa kufanya mikutano katika mikoa ya kusini katika kipindi hiki.

“Sisi vyama vya siasa hatuna mtutu wa bunduki, ila tunatoa elimu kwa wananchi ni wapi tumeyumba kiuchumi na nini kifanyike katika kuiondoa CCM madarakani,” alisema.

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top