KIM, RENARD KUWAKABILI WAANDISHI KESHO
Kocha wa Taifa Stars -Kim
Kocha wa Zambia -RENARD

Makocha wa Tanzania (Taifa Stars), Kim Poulsen na Zambia (Chipolopolo) watakuwa na mkutano na waandishi wa habari utakaofanyika kesho (Desemba 21 mwaka huu) kuzungumzia pambano lao litakalochezwa Jumamosi (Desemba 22 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mkutano huo utafanyika saa 5 asubuhi kwenye ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Makocha hao watazungumzia maandalizi yao ya mwisho kabla ya pambano hilo litakalochezeshwa na mwamuzi Sylvester Kirwa kuanzia saa 10 kamili jioni.

Pia makocha hao watajibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari kuhusu pambano hilo litakalokutanisha timu hizo ambazo zimefanya vizuri kwenye orodha ya viwango vya ubora vya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) vilivyotolewa jana (Desemba 19 mwaka huu).

Wakati Zambia ambao ni mabingwa wa Afrika wamepanda juu kwa viwango vya ubora kwa nafasi nne, Taifa Stars ambayo katika mchezo uliopita iliifunga Kenya (Harambee Stars) bao 1-0 imepanda kwa nafasi nne.

Taifa Stars ambayo inadhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager iko kambini tangu Desemba 12 mwaka huu kujiandaa kwa mechi hiyo kubwa ya kirafiki inayotarajiwa kuwa ya kuvutia.


  
TENGA ATOA NOTISI YA MKUTANO MKUU TFF
Rais wa TFF Leordgar Tenga

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga ambaye ndiye Mwenyekiti wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho hilo tayari ametoa notisi ya mkutano huo utakaofanyika Februari 23 na 24 mwakani jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo utafanyika Februari 23 mwakani na kufuatiwa na ajenda ya uchaguzi siku inayofuata. Ajenda ya uchaguzi iko chini ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF.

Notisi hiyo imetumwa kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu ambao ni kutoka vyama vya mpira wa miguu vya mikoa, vyama shiriki, klabu za Ligi Kuu ya Vodacom na wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF.

Ajenda za Mkutano Mkuu zitatumwa kwa wajumbe siku 15 kabla ya mkutano huo wenye wajumbe zaidi ya 100.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top