Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kujihusisha na wizi wa mtandao katika maduka yanayotoa huduma za M-PESA,Tigo Pesa na Airtel Money katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Dodoma. Kamanda wa polisi mkoani humo David Misime amesema Watu hao ambao
wanadaiwa kujipatia zaidi ya shilingi milioni moja na laki saba  kwa Mawakala wanne tofauti wanaotoa huduma hizo wamekamatwa jana..

Amewataja watuhumiwa hao ambao wanatokea Jijini Dar es Salaam kuwa ni Mohamed  Dotto maarufu kwa jina la Sefu, mkazi wa Kigogo, Mohamed Pazi na  Ally  Mohamed wote  wakiwa ni wakazi wa Ilala.

Amefafanua kuwa Wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali kufanikisha wizi huo, ikiwemo kwenda kwenye maduka yanayotoa huduma hizo na  kumwambia wakala kuwa wanaharaka na kutaka kuweka Pesa kiasi fulani ambacho wanakuwa nazo mkononi na kuanza  kuzihesabu. Mara ujumbe toka kwa wakala unapoingia katika simu zao, simu zao huita wakati huo huo na   kujifanya wanapokea  huku wakisogea pembeni na kisha huondoka jumla kwenda kuzitoa mahala pengine kwa haraka.

Kamanda Misime ametoa wito kwa wamiliki na mawakala wote wanatoa huduma hizo kuwa makini wanapoendesha shuguli zao, kwa kutoa taarifa za watu wanaowatilia shaka wanaofika kutaka huduma katika maduka yao ili wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top