Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein.
Serikali
ya Falme za Kiarabu (UAE) iko tayari kusaidia kuimarisha hospitali kuu
ya Mnazi Mmoja ili iweze kutoa huduma bora na za kisasa kwa wananchi.
Balozi
mpya wa nchi hiyo Abdulla Ibrahim Al-Suwaidi ametoa kauli hiyo Ikulu jana wakati alipokuwa akizungumza na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Katika
mazungumzo hayo Balozi Abdulla alisema nchi yake inajivunia uhusiano
wake wa kihistoria na Zanzibar na kwamba iko tayari mbali ya sekta ya
afya kuisaidia sekta nyingine ikiwemo elimu.
Amesema
wakati wa kipindi cha kuitumika nchi yake katika Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania atahakikisha uhusiano huo unaimarika kwa kuangalia maeneo
zaidi ya ushirikiano ikiwemo biashara na uwekezaji.
Alimueleza
Rais kuwa ujumbe wa wafanyabiashara kati ya 40 na 50 unatarajiwa kuzuru
Tanzania mwezi Juni mwaka huu ili kujionea fursa za biashara na
uwekezaji na hiyo itakuwa fursa nyingine ya kuimarisha mahusiano kati ya
serikali na watu wa Falme za Kiarabu na Tanzania.
Akimkaribisha
Balozi huyo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein alimueleza balozi Abdulla kuwa Zanzibar imetiwa moyo
na ushirikiano mzuri uliopo kati yake na nchi za Falme za Kiarabu na
kuzishukuru kwa misaada mbalimbali ambayo Zanzibar imekuwa ikipata
kutoka nchi hizo.
Alieleza
miongoni mwa sekta zilizofaidika ni maji na afya ambapo hospitali kuu
ya Mnazi Mmoja ilifanyiwa ukarabati mkubwa miaka ya nyuma.
Dk.
Shein alitumia fursa hiyo kumueleza balozi huyo mipango ya serikali ya
kuifanya hospitali hiyo kuwa ya rufaa kwa kuweka vifaa vya kisasa na
kuiwezesha kutoa huduma zote muhimu kwa wagonjwa.
Rais
alikubaliana na rai iliyotolewa na Balozi Abdulla ya kuongeza ziara za
viongozi hasa mawaziri na watendaji wakuu wa serikali za nchi zao ikiwa
ni njia mojawapo ya kuimarisha uhusiano wa Serikali na watu wa nchi
mbili hizo.
Alisema
ziara hizo ni muhimu katika kujenga msingi imara wa ushirikiano ambao
alisema serikali na watu wa nchi mbili hizo wana kila sababu kufanya
hivyo kuendeleza maslahi ya pamoja.
Dk. Shein alipendekeza ujumbe wa kibiashara kutoka Falme za Kiarabu utakaotembelea Tanzania mwezi
Juni upangiwe ratiba ya kuzuru Zanzibar ili kutoa fursa ya kuiona
Zanzibar na kukutana na viongozi wa Serikali na kufanya mazungumzo na
Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wenye viwanda na Wakulima wa Zanzibar.
Dk.
Shein alielezea pia umuhimu na kuhimiza uanzishwaji wa safari za moja
kwa moja za ndege za mashirika ya nchi hizo kama vile shirika la ndege
la Emirates na Al –Arabiya ili kuimarisha biashara na utalii Zanzibar.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment