Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
“Tunajua nia yao ni kufanya nchi
isitawalike lakini sisi tumesema hatukubali. Tumekubaliana na Waziri wa Mambo
ya Ndani, ulinzi uimarishwe kila mahali, mshingae kuona watu wanawahoji lakini
nia njema, ya kurudisha amani yetu,” alisema Waziri Mkuu.
Ametoa kauli hiyo juzi mchana (Ijumaa,
Mei 10, 2013) wakati akiwasilisha salamu za rambirambi kwa niaba ya Serikali
wakati wa ibada ya mazishi ya waumini watatu wa Kanisa la Mt. Joseph
Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti, jijini Arusha waliofariki dunia kutokana na
mlipuko wa mabomu uliotokea Jumapili iliyopita, Mei 5, mwaka huu kanisani hapo.
Waziri Mkuu amewaomba wanachi
kutoka ushirikiano kwa vyombo vya dola kwa kutoa taarifa zozote zitakazosaidia
kwenye upelelezi wa tukio hilo.
“Ninawaomba Watanzania tushirikiane
kuwafichua watu hawa waovu kwa sababu tunaishi nao, ni watu ambao wako miongoni
mwetu... Tusaidieni kutunong’oneza ili tuchukue hatua, alisema.
Waziri Mkuu alisema yeye ni
miongoni mwa watu wanaoamini kwamba ukristo au uislamu hauwezi kuondolewa kwa
kuwaua viongozi wa dini au waumini wao. “Ni kujidanganya tu mtu akiamini kuwa
akimuua Askofu, Mufti au Muumini
ataimaliza dini yoyote. Madhehebu haya mawili ni nguzo kubwa kwa Taifa letu,
tunatamani tuendelee kuwa na amani iliyokuwepo siku zote,” alisisistiza.
Alisema Serikali kupitia idara ya
maafa itatoa sh. milioni 100/- ili zisaidie kukabiliana na janga lililowakabili
wana Arusha.
Mapema, akiongoza ibada hiyo, Muadhama Polycarp Kardinali Pengo
aliwataka waumini wote kutolipa uovu kwa uovu bali watende wema ili kusahihisha
maovu. “Ishara ya uovu imetendwa na hawa watu dhidi ya waumini wenzetu kwa
madhumuni yanayojulikana na wao tu bila kuchokozwa na hawa marehemu ama wale
waliko hospitali (majeruhi),” alisema.
“Uovu umeshatendwa, je sisi tufanye
nini? Angekuja hapa kanisani yule aliyesababisha mauti haya, tungemfanya nini?”
Alihoji Kardinali Pengo na kujibiwa na mamia ya waumini waliohudhuria ibada
hiyo: “Tungemsamehe.”
Aliwasihi waumini wote kuendelea
kuliombea Taifa la Tanzania ili tukio hilo na lile la kuuawa kwa Padre Evarist
Mushi kule Zanzibar yasiwe sababu ya kusambaratika kwa amani ya Taifa hili.
“Tusilipe ubaya kwa ubaya,
tuendelee kuomba Mungu asikie sala yetu na awazindue wenye mamlaka watimize
wajibu wao,” alisema.
Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Alex Malasusa akitoa salamu za
rambirambi kwa niaba ya Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF), alilaani
waliosababisha mauaji hayo na kusema kitendo hicho kimelitia doa Taifa kwa vile
ni kitendo kinachoashiria kuchafua amani ya Tanzania.
Aliwasihi waumini wote kutokuwa
waona katika kazi ya kumtanga za Kristo. “Risasi zinapigwa, mioto inayowashwa
katika makanisa yetu na mabomu yanayolipuliwa yasiwe sababu ya kututia hofu.
Imani yetu haiko katika miili bali iko mioyoni mwetu,” alisema.
Askofu Mkuu Josephat Lebulu wa
Jimbo Kuu la Arusha akitoa shukrani kwa niaba ya Kanisa Katoliki aliwashukuru
wote waliofika kuwafariji kutokana na tukio hilo na kuwathibitishia kuwa kama
Kanisa wameguswa na moyo waliouonyesha.
“Tupige goti, ndiyo kazi
tuliyonayo. Tupige goti ili Mungu awafichue hawa watu, aufichue mfumo wao wa
kiovu, na awape nguvu viongozi wetu wao ni kama sisi na iko siku watatoa hesabu
mbele ya Mwenyezi Mungu,” alisema.
Aliwasihi waumini wote kutoogopa na
kuendelea kuomba ili waliohusika na uovu huo Mungu awafichue na kuwaonyesha
hadharani. “Ninaambiwa msiogope, hakuna kutishwa kwa namna yoyote tunaposimama
na Kristo... sisi hatupaswi kuogopa kwa sababu Kristo alishinda mauti,”
alisisitiza.
Watu 66 waliathirika kutokana na
mlipuko huo uliotokea Mei 5, mwaka huu ambapo watatu wamefariki dunia na kati
ya wagonjwa 63 waliobakia, wanane walihamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili,
wengine waliotibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani, na baadhi wanaendelea
kupatiwa matibabu mjini Arusha.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment