Hayati Edward Moringe Sokoine.

MTOTO mkubwa wa Waziri Mkuu wa zamani Hayati Edward Moringe Sokoine, Lazaro Sokoine, ameibuka na kutoa madai mazito ya kutaka mwili wa baba yake ufanyiwe uchunguzi, kubaini chanzo cha kifo chake.

Mbali na kutaka uchunguzi huo, Lazaro pia amemuandikia barua Rais Jakaya Kikwete akielezea mlolongo wa matukio mengi, likiwemo mgogoro wa familia hiyo na kuporwa kwa ardhi na mali zake zingine alizoachiwa na Hayati Sokoine.

Lazaro alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam katika mahojiano maalumu na Tanzania Daima Jumatano, huku akishusha madai mazito dhidi ya Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Namelock Sokoine, ambaye ni mdogo wake.

Kwa nini mwili wa Sokoine uchunguzwe?
Akielezea sababu za kutaka mwili wa Sokoine uchunguzwe, Lazaro alisema miezi minne kabla ya kifo chake mwaka 1984 baba yake alienda nchini Cuba wakati Lazaro akiwa masomoni nchini humo; Sokoine alimwambia mwanaye huyo kuwa asishangae kusikia amekufa kwa njia yoyote ile ikiwamo kupigwa risasi kwani kuna watu wanamuwinda.

Alisema baada ya baba yake kumueleza hivyo alihoji sababu ya kuwa na hofu hiyo ambapo Sokoine alijibu kuwa hali ya nchi wakati huo chini ya Mwalimu Julius Nyerere, ilikuwa mbaya kutokana na vita dhidi ya wahujumu uchumi.

Mtoto huyo ambaye ana hali mbaya kiuchumi, alisema baba yake aliendelea kumwambia kuwa kutokana na hali hiyo, Mwalimu Nyerere alimuongezea ulinzi kutoka askari wanne hadi 14.

“Baba alikuja Cuba kwa ajili ya sherehe za uhuru wa nchi hiyo na akaniambia maneno hayo mazito nami nikaenda kuongea na walinzi wake ambao ni Mashaka, Kimaro na Kalbert juu ya hofu hiyo ya baba,” alisema Lazaro.

Alisema miezi minne baadaye alipata taarifa ya kifo cha baba yake kupitia Ikulu ya Cuba hali iliyomfanya ayakumbuke maneno ya tahadhari aliyoambiwa juu ya hofu ya kuuawa.

Akieleza sababu nyingine iliyomfanya atake mwili wa baba yake uchunguzwe upya, Lazaro alisema agizo la Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa wa wakati huo Imran Kombe, kuwataka walinzi wa Sokoine waliokuwa Dodoma watangulie Arusha badala ya kuandamana naye kwenda jijini Dar es Salaam, linatia shaka kwamba kulikuwa na mpango wa kutaka kumuua.

Alisema kutokana na mazingira hayo, amekuwa akitamani sana kuanzisha harakati za kutaka mwili wa kiongozi huyo maarufu uchunguzwe, lakini hali yake kiuchumi ndiyo inayomkwamisha.

“Kwa sasa sina uwezo ila nikipata pesa nitaanzisha mchakato wa kuchunguza kifo cha baba yangu; nimekuwa nikiuliza hili kwa muda mrefu, watu wamenichukia na sasa wananipiga vita hadi ndani ya familia kwa kuhoji suala hilo, mdogo wangu anayeitwa Joseph Sokoine aliyeko ubalozi wa Tanzania nchini Canada aliniambia nisiulizeulize hili suala, wala nisiliingilie kwani siku moja wataning’oa macho au kuniondoa duniani,” anaongeza Lazaro.

Alisema hivi karibuni wakati mwili wa Sokoine ulipozikwa kwenye kaburi jipya kutoka lile la awali, aliiambia familia yake kwamba isifunge milango ya kaburi ili uchunguzi wa mwili wa baba ufanyike.

Hivi karibuni gazeti hili lilipata kuandika taarifa ya mwili wa Sokoine kuzikwa kwenye kaburi jipya baada ya lile la awali kuharibika na kwamba familia ina mpango wa kutaka kuufanyia uchunguzi mwili huo.

Ikumbukwe kuwa wakati wa kifo chake kulikuwa na mjadala mzito, wengi wakidai aliuawa na kwamba kifo chake kilipangwa na mahasimu wake ndani na nje ya serikali ambao walikerwa na operesheni yake ya kupambana na wahujumu uchumi na mali za taifa.

Kwa mujibu wa sheria, mwili ukishazikwa unaruhusiwa kufanyiwa uchunguzi baada ya miaka 30 na mwakani mwili wa Sokoine utafikisha umri wa miaka 30 tangu ulipozikwa na huo utakuwa muda muafaka kwa wana ndugu hao kutaka kujua ukweli wa kifo cha ndugu yao.

Madai ya kuporwa mali
Akizungumzia suala la kuporwa mali na ardhi, Lazaro alisema ameamua kumuandikia barua Rais Kikwete ili aingilie kati kupata haki zake.

Alisema mwaka 1983, akiwa nchini Cuba Sokoine alimkabidhi kiwanja katika eneo la Kunduchi na hati ya kusaini umiliki wa kiwanja hicho ilipelekwa nchini humo na Paraseko Kone, ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Singida.

Alisema baada ya kumaliza kusaini, Kone alizirejesha hati hizo na kumkabidhi aliyekuwa Mkurugenzi wa Katapila Tanzania kwa wakati huo, Victor Ole Kimesera, ambaye kwa sasa ni Katibu Mtendaji ofisi ya Katibu Mkuu CHADEMA.

Aliongeza kuwa mwaka 1984 alipokuwa kwenye msiba wa baba yake, aliulizia mahala zilipo nyaraka hizo na mama yake alimueleza zilikokuwa na kwamba alipomaliza masomo nchini Cuba alirejea nchini na kukuta kiwanja hicho kimemilikishwa kwa mdogo wake Kilimbe Edward Sokoine.

Alisema baadaye kiwanja hicho kwa kushirikiana na mdogo wake, walikiuza kwa kampuni moja (jina linahifadhiwa), bila ridhaa yake.
“Kwa sasa mimi nina matatizo makubwa hata msaada unaotolewa na serikali kwa familia yetu mimi sijawahi kuupata nakuapia hata gari wananikataza nisisogelee na anayefanya hivi ni mdogo wangu, Namelock,” alisema Lazaro na kuongeza.

“Baba aliniambia kiwanja nimekupatia na pia kuna ng’ombe dume 600 wa kutumia kujengea hicho kiwanja.”

Lazaro alisema kutokana na hali hiyo aliamua kumuandika barua Rais Kikwete Mei 13 mwaka huu na kulazimika kuja jijini Dar es Salaam kujua hatma ya barua yake kama ilishafika mikononi mwa Rais Kikwete.

“Nina mke na watoto wawili hadi hivi sasa mke wangu amerudi kwao kwa kukosa matunzo, maisha ya kulala chini na kukosa chakula yananikabili; ninaleta matatizo haya kwako ili uweze kunisaidia kupata haki zangu zilizotaifishwa ili niondokane na maisha magumu niliyonayo ya kukosa sehemu ya kulala huku nikiwa na watoto wadogo chini ya miaka mitano na kukosa pesa ya kujikimu kimaisha,” inasomeka sehemu ya barua hiyo.

Kutokana na madai hayo Tanzania Daima Jumatano iliwasiliana na Mkuu wa Mkoa wa Singida kwa simu kujua ukweli wa madai hayo.
Mkuu wa mkoa huyo alisema hakumbuki kupeleka fomu kwa Lazaro akiwa masomoni Cuba, lakini alikiri kukutana naye nchini homo.

“Nakumbuka nilikutana na kijana huyo wakati huo akiwa masomoni Cuba ila sikumbuki hilo la kumpelekea fomu ya umiliki wa kiwanja,” alisema Kone.

Kwa upande wake Namelock ambaye ni mbunge wa viti maalumu (CCM) alikiri kuwa kiwanja anachoeleza kaka yake ni haki yake na kwamba kwa sasa kinamilikiwa na watu watatu kwa njia ya ujanja.

“Tumefuatilia bila mafanikio na juzi alipoenda Ikulu nilimwambia afadhali amwandikie barua Rais, na aliandika imefika kwa kuwa msaidizi wa Rais alinipigia, tena ramani ya hicho kiwanja ninayo hadi sasa,” alisema Namelock.”

Sokoine alifariki Aprili 12, 1984 eneo la Wami-Dakawa akiwa njiani kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top