WATU wawili wamekufa na wengine 66 kujeruhiwa baada ya kutokea
mlipuko wa kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu wakiwa katika ibada ya
kutabaruku parokia mpya ya Olasiti, jijini Arusha jana.
Mlipuko huo umetokea huku kukiwa na vuguvugu la machafuko ya kidini
nchini pamoja na onyo la Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Said
Mwema, kuwataka Watanzania wawe macho na magaidi wa vikundi vya Al
Shabab na Al-Qaeda wanaoweza kufanya mashambulizi wakati wowote.
Miongoni mwa walionusurika ni balozi wa Baba Mtakatifu nchini Mhashamu
Askofu Mkuu Francisco Padila, Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Arusha
Josephat Lebulu, mapadri na waumini waliohudhuria ibada hiyo.
Kati ya watu waliojeruhiwa, wengine walikimbizwa katika hospitali ya rufaa ya KCMC, mkoani Kilimanjaro, kwa matibabu zaidi.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo ambao walifika kusali katika
kanisa hilo walisema lilikuwa la kushtukiza baada ya kitu ambacho
wanadai kilikuwa katika mfuko wa Rambo kilipodondoka nje ya jengo la
kanisa hilo na kulipuka.
“Kwa kweli tukio hili lilikuwa la ghafla sana ambalo hatukulitegemea
kwa kuwa waumini wote tulikuwa tukimuangalia Askofu Mkuu akikaribia
kukata utepe na ghafla ukatokea mlipuko huo na kuzua taharuki kubwa
kwetu,” alisema mmoja wa mashuhuda hao.
Mpaka wakati tunaelekea mitamboni jeshi la polisi lilikuwa
likimshikilia mtu mmoja kwa mahojiano kuhusiana na tukio hilo akidaiwa
ndiye aliyerusha kitu kilichosababisha mlipuko huo katika kanisa hilo.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, baada
ya kufika katika eneo la tukio aliwataka waumini kutulia na kutohusisha
tukio hilo na dini yoyote.
“Ndugu zangu tukio limeishatokea….., ni tukio kama mengine; tutulie
linafanyiwa uchunguzi na tusilihusishe tukio hilo na dini yoyote,”
alisema.
Mulongo alipata wakati mgumu wakati akitoka katika Hospitali ya Mount
Meru baada ya kikundi cha wananchi waliokuwepo hapo kuanza kumzomea.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabasi, alithibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kwamba jeshi hilo linamshikilia mtu mmoja kwa
uchunguzi kuhusiana na mlipuko huo.
Kamanda Sabasi alisema wanashirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ) kuchunguza sampuli za mchanga waliochukua katika eneo hilo la
tukio ili kujua mlipuko huo umetokana na kitu gani.
Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema, akiwa ameongozana na mbunge wa
Arumeru Mashariki, Joshua Nasari, walifika katika kanisa hilo na kuamsha
kelele za kushangiliwa na wananchi kujisahau kama kuna janga limetokea
katika eneo hilo.
Akizungumza katika eneo hilo, Lema aliwapa pole waliofikwa na maafa
hayo huku akilitaka Jeshi la Polisi kutumia nguvu ileile waliyoitumia
kumkamata yeye kufanikisha kukamatwa wahusika wa tukio hilo.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mount Meru, Frida Mokitu, alithibitisha
kupokea majeruhi 42 na kuelezea kifo cha watu wawili ambao
hawakulitambuliwa majina yao kwa wakati huo.
Majeruhi wengine 16 walipelekwa katika Hospitali ya Seliani iliyoko
katikati ya jiji la Arusha wakiendelea kupata matibabu na wagonjwa
wengine wawili wakikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC.
Baadhi ya majina ya majeruhi iliyopatikana jana walioko katika
Hospitali ya Mount Meru ni Concesta Julius Mbaga, Edith Ndowo,
Christopher Raymond, Frank Donatus, Deborah Joakim, Elizabeth Isidory,
Beather Cornel, Neema Daudi na Anold Alex.
Wengine ni Sophia Kimolo, Lightness Nelson, Theophilda Inocent,
Jackline John, Faustin Andrea, Regina Daud, Donald Swai, Restuta Alex,
Alfonce Nyakondi, Mathias Kiya, Anna Didas, Albert Njou, Flomena
Nyereza, Dereck Kessi, Mary Okeere na Joyce Okeele.
Aidha wengine ni Doreen Pankaras, Fatuma Tarimo, Faustin Andrea, Anna
Didas, Anastazia Regine, Anna Kessy, Elizabeth Masawe na Faustin
Shirima.
Utoaji damu
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Mbunge wa Arumeru Mashariki na
kada wa CHADEMA James Ole Millya waliwahamasisha wananchi wa Arusha
kujitokeza kujitolea damu kwa ajili ya kusaidia matibabu kwa majeruhi.
Akizungumza kwa simu na gazeti hili, Lema alisema, “Nimewahamasiha
wapigakura wangu wafike kujitolea damu, zoezi hili limeongozwa na
Nassari na Ole Millya nitafuatia mimi, na vijana wengi zaidi ya 200
wamefuatana nasi tuko hapa hospitali ya mkoa, maana tunajua katika hali
hii ndugu zetu wanaweza kuhitaji damu.”
Akizungumzia tukio hilo, Makamu Mkuu wa Chuo cha Mtakatifu Agustino,
Padri Charles Kitima, alisema kitendo hicho ni uhalifu uliotendwa ili
kuvuruga ibada.
“Kama ni bomu tujiulize nini kinaingia nchini, nyumba za ibada ni
tulivu, ni mahali ambapo tunapaswa kukimbilia hivyo hatutegemei vitu
kama hivi kutokea huko, ila tusubiri taarifa ya jeshi la polisi,
serikali inapaswa ijiulize ni kwa nini kwenye nyumba za ibada, ingawa
tunatoa tahadhari kuwa uhalifu huu usihusishwe na mapenzi ya Mungu, ni
maslahi ya waovu kwa maslahi ya kutesa watu.”
Wananchi wavunja geti
Wakati majeruhi wakiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya
Mount Meru, mgonjwa mmoja ambaye jina halikupatikana alizidiwa hali
iliyolazimu ahamishiwe KCMC lakini gari la wagonjwa lililombeba mgonjwa
huyo lilipofika getini halikufunguliwa kutokana na kutokuwapo kwa
walinzi.
Kutokuwapo kwa walinzi hao kuliamsha hasira za wananchi ambao waliamua
kusubiri kwa dakika 10 na baada ya hapo waliamua kuvunja geti la
hospitali hiyo ili kuruhusu gari liwahi KCMC.
Bilal, IGP Mwema wazuru
Wakati huohuo Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, na Inspekta
Jenerali wa Polisi (IGP), Saidi Mwema, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani,
Pereira Silima, na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele,
walifika eneo la tukio jana jioni kuwajulia hali majeruhi na kutoa pole
kwa waliofikwa na maafa hayo.
Dk. Bilal alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuwasaka wahusika wa
tukio hilo ili sheria ichukue mkondo wake huku akiwataka watu wa dini
mbalimbali kukaa kwa amani na kuepusha chokochoko ya aina yoyote ile.
Dk. Bilal aliamua kumchukua mtoto wa kiume Anorld Alex (10) aliyeumia
katika tukio hilo na kuahidi kumkimbiza katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili ili akapatiwe matibabu kutokana na hali yake kuwa mbaya.
Tukio la Arusha
Tukio la jana limetokea siku chache tu baada ya Mkuu wa Jeshi la
Polisi Nchini (IGP), Saidi Mwema, kusema zipo dalili za kuibuka makundi
ya kigaidi ndani ya nchi yakiratibiwa na makundi ya Al-Qaeda na
Al-Shabab.
Mwema alitoa kauli hiyo April 21 visiwani Zanzibar kwenye semina ya
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ambapo aliwakilishwa na Kamishna
Mwandamizi wa Polisi Hussein Nassor Laisseri, alipokuwa akiwasilisha
mada kuhusu hali ya uhalifu Tanzania Bara na visiwani Zanzibar.
Matukio ya kigaidi yamekuwa yakitokea mara kwa mara nchi jirani ya
Kenya ambapo inadaiwa kikundi cha Al Shabab kimekuwa kikiendesha matukio
hayo kupinga serikali ya Kenya kupeleka majeshi yake nchini Somalia.
0 comments:
Post a Comment