Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare.

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imewafutia mashtaka matatu ya ugaidi, Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare na mwenzake Joseph Ludovick Rwezaura.

Mashtaka yaliyofutwa ni ya pili, tatu na nne. Shtaka la kwanza ambalo ni la kawaida la jinai limebaki. Yaliyofutwa ni kupanga njama za utekaji nyara dhidi ya Dennis Msacky kinyume na Kifungu cha 21 cha sheria inayopinga ugaidi. Shtaka la tatu ni walipanga na kushiriki katika mkutano wa kupanga kitendo cha ugaidi cha utekaji nyara dhidi ya Msacky na la nne ni lilikuwa likimkabili Lwakatare la kuhamasisha vitendo vya kigaidi.

Katika shtaka la kwanza ambalo ndilo lililobaki, washtakiwa hao wanadaiwa kula njama kumdhuru Msacky kwa kutumia sumu kinyume na Kifungu cha 227 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Kwa uamuzi huo, washtakiwa hao wanaweza kuomba dhamana wakati kesi yao itakapotajwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mei 13, mwaka huu.

Katika uamuzi wake, Jaji Lawrence Kaduri wa Mahakama Kuu alikubaliana na hoja za mawakili wa Lwakatare kuwa mashtaka hayo hayana maelezo ya kutosha kuonyesha kuwa ni ya ugaidi akisema yalipaswa yawe na maelezo yanayoelezea uhalisia wa ugaidi.

Hata hivyo, mahakama hiyo ilitupilia mbali maombi ya mawakili wa watuhumiwa hao kupinga uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) wa kuwafutia kesi na kisha kuwakamata na kuwafungulia tena kesi yenye mashtaka hayohayo kwenye Mahakama ya Kisutu, Machi 20, mwaka huu.

Jaji Kaduri alikubaliana na hoja za Wakili wa Serikali, Prudence Rweyongeza alizozitoa wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo kuwa uamuzi wa DPP ulikuwa sahihi.

Lwakatare na Rwezaura walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Machi 18 na kusomewa mashtaka hayo manne katika kesi namba 37 ya mwaka 2013.

Zombe aachiwa huru
Aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Zombe akizungumza na waandishi wa habari kwenye Viwanja vya Mahakama ya Rufani Dar es Salaam jana mara baada ya rufaa dhidi yake kutupiliwa mbali.

Mahakama ya Rufani imetupilia mbali rufaa ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Dar es Salaam (RCO), Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Abdallah Zombe na wenzake wanane.

Hata hivyo, mahakama hiyo imetoa fursa nyingine kwa DPP kukata rufaa nje ya muda kwa kuzingatia Sheria ya Ukomo wa Muda.

DPP alikata rufaa akipinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyomwachia huru Zombe na wenzake katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge, Morogoro na dereva teksi mmoja wa Manzese, Dar es Salaam.

Mahakama hiyo iliitupilia mbali kutokana na kasoro za kisheria zilizobainika katika taarifa ya kusudio la kukata rufaa.

Kasoro hiyo ni kuandika kuwa hukumu inayopingwa ilitolewa na Jaji Salumu Massati wa Mahakama ya Rufani, badala Jaji wa Mahakama Kuu.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top