Bunge la Jamhuri ya Muungano limelazimika kuahirishwa mara mbili siku ya Alhamisi ya leo baada ya kutokea kwa mgongano wa kikanuni baina ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na chama cha wananchi (CUF).
Mgongano huo ulijitokeza mara baada ya msemaji wa kambi ya upinzani Ezekiel Wenje  wakati akiwasilisha bajeti ya wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa ambapo hotuba yake ilisitishwa kwa madai ya kutumia maneno ya kuwaudhi wabunge wa chama cha CUF.
Mbunge wa Mtambile wa CUF Mheshimiwa Masoud Abdallah Salim alilazimika kuomba mwongozo kwa Naibu Spika Job Ndugai kwa kumuomba mhusika ayafute maneno na kuomba radhi kwa chama chake.
Naibu Spika alilazimika kusitisha shughuli za bunge mchana na kuruhusu kamati ya maadili ya bunge kukaa kwa ajili ya kutatua mgogoro huo ambapo jioni Mheshimiwa  Wenje aliamrishwa kuomba radhi na kuondoa vifungu vyenye maneno yanayodaiwa kuwaudhi wabunge wa CUF bila mafanikio.
Hata hivyo Mheshimiwa Wenje ambaye ni Mbunge wa Nyamagana alikubali kuondoa maneno husika lakini amekataa kuomba radhi kwani anasema madai yalikuwa sahihi.
Baada ya majibu hayo  kwa mara nyingine Naibu Spika Job Ndugai akaahirisha kikao hicho mpaka Ijumaa saa tatu asubuhi.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top