Jeshi la Polisi nchini limewataka wananchi kutokuwa na hofu juu ya taarifa za kutoaminika na  ambazo hazijafanyiwa uchunguzi zinazotolewa na baadhi ya watu kuhusu idadi ya watu waliofariki katika vurugu zilizotokea mkoani Mtwara.
Akizungumza na Waandishi wa habari mkoani Mtwara Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi hilo Paul Chagonja alisema idadi ya watu waliofariki ni watu watatu mpaka hivi sasa na waliojeruhiwa ni watu kumi na nane tofauti na taarifa ambazo zimekuwa zikisambazwa na baadhi ya watu.
Aliwataja waliofariki kuwa ni Fatuma Mohamed (22), Karimu Shaibu (22) na Mussa Mohamed (28) ambapo mpaka hivi sasa mtu mmoja ndiye aliyebakia katika hospitali ya rufaa ya Ligula akipatiwa matibabu.
Chagonja alisema watu 91 walishafikishwa mahakamani kujibu makosa mbalimbali ikiwemo ikiwemo kuharibu miundominu, kufanya mikusanyiko isiyo halali na kuchoma nyumba moto.
Alisema zaidi ya watu mia moja wameshajitokeza mbele ya tume iliyoundwa kwa ajili ya kukusanya malalamiko kwa yeyote ambaye anaona hakutendewa haki wakati wa kudhibiti vurugu hizo na endapo upelelezi utabaini kuwepo kwa vitendo viovu sheria itafuata mkondo wake.
Hata hivyo alibainisha kuwa Jeshi hilo litahakikisha linamkamata kila mmoja ambaye amehusika katika vurugu hizo na kumfikisha katika vyombo vya sheria.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top