JESHI la Polisi mkoani Arusha linamshikilia ofisa wa jeshi hilo, Inspekta Isaac Manoni, kwa tuhuma za kumtorosha mtuhumiwa wa usafirishaji wa magunia ya bangi, Koplo Edward.

Koplo Edward ni dereva wa gari la polisi lenye namba za usajili T 2025, aina ya Toyota Land Cruiser, linalodaiwa kutumika kubeba magunia 18 ya bangi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema jana kuwa katika sakata la usafishaji wa bangi kwenda Holili, mpakani Kenya, watuhumiwa walikuwa wawili, akiwamo askari namba G. 2434, PC George, ambao wote wamefukuzwa kazi.

Hata hivyo, habari zaidi zinasema kuwa kutoroka kwa askari huyo kunadaiwa kuwa ni mpango uliotengenezwa na askari wenzake ili kupoteza ushahidi katika kashfa hiyo.

Inaelezwa kuwa askari huyo aliwatoroka askari waliokuwa wakimlinda akiwa nyumbani kwake baada ya kuwahadaa kuwa anachukua pesa na ndipo alipotokea mlango wa nyuma.

Baadhi ya askari mjini Moshi waliozungumza kwa sharti la kutotaka majina yao yatajwe, walidai kuwa tukio hilo ni mpango uliosukwa na baadhi ya askari wenzake wa Arusha kwa lengo la kumwepusha na balaa mmoja wa vigogo wa jeshi hilo anayedaiwa kuwa kwenye mtandao wa kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi.

Askari huyo ndiye anayedaiwa kumpigia simu kigogo mmoja wa polisi mjini Arusha akimtaarifu kukamatwa kwao na akakaripiwa kwa kukamatwa kizembe huku mpango wa kuwapa rushwa askari wa doria waliowakamata ukikwama.

“Wakati wakiwa katika nyumba ya mtuhumiwa huyu kulikuwa na askari saba, akiwamo Inspekta Isaac ambaye alikuwa kiongozi, hivyo baada ya tukio lazima tumshikilie huyu kwa uzembe kazini,” alisema kamanda huyo.

Awali watuhumiwa hao walikamatwa Mei 18, mwaka huu, majira ya saa 5 usiku huko Himo na askari polisi wa Kilimanjaro wakiwa na gari la polisi lenye namba za usajili T 2025, Toyota Land Cruiser lililokuwa likiendeshwa na Koplo Edward huku likiwa na magunia 18 ya bangi yakipelekwa Holili, mpakani Kenya.

Hata hivyo jeshi hilo limetoa wito kwa mtu yeyote anayefahamu mahali alikotorokea mtuhumiwa huyo atoe taarifa polisi na kuwafichua watu wote wenye mtandao wa biashara haramu ya bangi.

Kamanda Sabas alisema kuwa tayari ameshatoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya kutoroka kwa askari huyo na hatua zilizochukuliwa kwa askari waliokuwa wakimlinda, hivyo hawezi kutoa taarifa nyingine kwa njia ya simu.

Katika hatua nyingine, askari PC George, mwenye namba za usajili G. 2434 amefikishwa mahakamani mkoani Kilimanjaro.

Mbali na askari huyo, pia mfanyabiashara mmoja, Livingstone Urassa, wa Usseri Wilaya ya Rombo alifikishwa mahakamani pamoja na askari huyo ambapo wote walisomewa shitaka la kula njama na kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi.

Washtakiwa hao walifikishwa mbele ya Hakimu Simon Kobelo, ambaye ni Hakimu Mkazi Mfawidhi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Moshi.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyosomwa na wakili wa serikali, Abdallah Chavula, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa siku, muda na mahali pasipofahamika walikula njama ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi.

Shitaka la pili lilimhusu PC George, ambaye anadaiwa kuwa Mei 18, mwaka huu huko Kilema, Wilaya ya Moshi, mshtakiwa alisafirisha dawa za kulevya aina ya bangi magunia 18, ikiwa na thamani ya sh milioni 81.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 5, mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakamana hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza shauri hilo.
Tanzania Daima 
Picha kwa hisani ya mitandao
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top