WIZARA YA MAWASILIANO, SAYANSI NA TEKNOLOJIA TAMKO LA SERIKALI KUHUSU UHAMAJI KUTOKA MFUMO WA UTANGAZAJI WA ANALOJIA KWENDA DIJITALI
Mabadiliko katika mfumo wa utangazaji kutoka mfumo wa analojia kwenda
katika mfumo wa dijitali ni utaratibu ambao unaendelea ulimwenguni kote.
Mabadiliko haya yanatokana na makubaliano ya nchi wanachama wa Shirika
la Umoja wa Mataifa lenye dhamana ya masuala ya mawasiliano yaani
International Telecommucations Union yaliyofanyika mwaka 2005 huko
Geneva, Uswisi. Makubaliano ya nchi wanachama ni kuzima kabisa
matangazo katika mfumo wa analojia na kutumia mfumo wa utangazaji wa
dijitali ifikapo tarehe 17 Juni 2015. Ili kuhakikisha
mabadiliko haya yanafanyika kwa ufanisi, tija na pia kutoa muda wa
kutosha wa kutekeleza mabadiliko haya, mwaka 2005 Serikali ilianza
mchakato wa uhamaji kutoka mfumo wa utangazaji wa analojia kwenda
dijitali ambao ulihusisha wadau wote, wakiwemo wamiliki wa vyombo vya
habari na vituo vya utangazaji wa televisheni, hatua kwa hatua, hadi
kuridhia ratiba nzima ya uzimaji wa mitambo ya analojia. Kwa kifupi
mchakato wa uhamaji ulipitia hatua zifuatazo: Mwaka 2005:
Waraka wa kwanza wa mashauriano (consultative document) kuhusu umuhimu
na faida za kuhama kutoka mfumo wa utangazaji wa analojia kwenda
dijitali ulitayarishwa na kusambazwa kwa wadau wote; Mwaka
2006: Waraka wa pili wa mashauriano na mapendekezo ya muundo wa leseni
kwenye mfumo wa utangazaji wa teknolojia ya dijitali ulitayarishwa na
kusambazwa kwa wadau wote; Mwaka 2007: Kamati ya kiufundi inayoshughulikia uhamaji kutoka mfumo wa utangazaji wa analojia kwenda dijitali iliundwa;
Mwaka 2007: Mkutano mkuu uliojumuisha vituo vyote vya utangazaji nchini
ulifanyika Bagamoyo kupitisha maazimio ya mfumo wa leseni za utangazaji
utakaotumika kwenye mfumo wa dijitali; Mwaka 2010: Kampuni tatu (3) zilipewa leseni za ujenzi wa miundombinu ya utangazaji ya dijitali. Kampuni tatu zilizopewa leseni za kusambaza matangazo ya dijitali ni:- Agape Associates Limited, Basic Transmission Limited, na Star Media (T) Limited.
Kampuni hizo zilipewa leseni baada ya kuthibitisha kuwa zina uwezo wa
kujenga miundombinu ya kurushia matangazo katika mfumo wa dijitali; Mwaka 2010: Kamati ya Kitaifa ya Kuratibu Mabadiliko ya Utangazaji toka mfumo wa analojia kwenda dijitali iliundwa. Kamati hii hukutana kila baada ya miezi mitatu kutathmini maendeleo ya ubadilishaji wa mfumo wa utangazaji;
Mwaka 2011: Kampeni ya Kitaifa ya kuelimisha umma kuhusu mabadiliko ya
mfumo wa utangazaji ilizinduliwa rasmi na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Ili kuhakikisha kuwa ujenzi wa
miundombinu ya urushaji wa matangazo katika mfumo wa dijitali unaendana
na ratiba ya uhamiaji katika mfumo wa matangazo kutoka mfumo wa analojia
kwenda dijitali, taarifa za mara kwa mara zimekuwa zikiletwa na wajenzi
wa miundombinu hiyo katika Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania na
kujadiliwa na Kamati mbalimbali zinazohusiana na masuala ya uhamaji
katika mfumo wa utangazaji wa dijitali. Taarifa hizo zimekuwa
zikionyesha kuwa ujenzi wa miundombinu unaendelea vizuri na kwamba
ratiba ya uzimaji wa mitambo ya analojia nchini itakwenda kama
ilivyokubalika na wadau wa utangazaji. Kufuatia uzinduzi wa
Kampeni ya Kitaifa ya Kuelimisha umma kuhusu mabadiliko ya mfumo wa
utangazaji kutoka katika mfumo wa analojia na kwenda katika mfumo wa
dijitali uliofanywa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Serikali, kwa kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, iliandaa Mkakati
Maalum wa Mawasiliano ambao ulilenga katika kuhamasisha wananchi kuhusu
uhamaji katika mfumo wa utangazaji wa dijitali. Njia
mbalimbali zimetumika katika kuelimisha umma kuhusu mabadiliko ya mfumo
wa utangazaji ikiwa ni pamoja na kufanya mikutano ya hadhara sehemu
mbalimbali, kutoa vipeperushi na matangazo katika magazeti, redio na
televisheni, kufanya majadiliano katika televisheni na redio ambayo
yalihusisha pia maswali kutoka kwa wadau mbalimbali, kuweka taarifa
katika tovuti kuhusu masuala mbalimbali ya uhamaji katika mfumo wa
utangazaji. Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa uhamasishaji na
elimu kwa umma imetolewa kwa kiasi kikubwa na wananchi wamehamasika sana
katika kuingia katika mfumo wa utangazaji wa dijitali kutoka ule wa
analojia. Hii ni kutokana na wananchi wengi kujitokeza kununua
ving’amuzi (visimbuzi) kwa wingi katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo
mengine ambayo matangazo katika mfumo wa analojia yalitarajiwa kuzimwa.
Aidha, hapakuwa na mapendekezo yoyote kutoka kwa wajenzi wa
miundombinu ya urushaji wa matangazo ya dijitali kuwa watashindwa
kujenga miundombinu hiyo kwa wakati ifikapo tarehe 31 Desemba 2012, siku
ambayo ilikuwa imekubalika kuzima mitambo ya utangazaji ya mfumo wa
analojia na kuanza kutumia mfumo wa dijitali. Tarehe 31
Desemba 2012, Serikali ilianza kuzima matangazo hayo kwa awamu ili
kubaini na kushughulikia changamoto mbalimbali ambazo zingeweza
kujitokeza katika mabadiliko hayo. Uzimaji wa mitambo ya
utangazaji wa analojia kwenda katika mfumo wa utangazaji wa dijitali
ilianza kutekelezwa tarehe 31 Desemba 2012 kwa kuzima mitambo 14 ya
televisheni inayotumia utangazaji wa mfumo wa analojia katika jiji la
Dar es Salaam ambapo wananchi wengi walinunua ving’amuzi ili waweze
kujiunga na mfumo mpya wa utangazaji wa dijitali. Kadhalika,
uzimaji wa mitambo ya analojia kwenye miji ya Dodoma na Tanga ulifanyika
tarehe 31 Januari 2013. Uzimaji wa mitambo ya analojia kwa jiji la
Mwanza ulifanyika tarehe 28 Februari 2013. Uzimaji wa mitambo kwa miji
ya Arusha na Moshi umefanywa tarehe 31 Machi 2013. Kwa ujumla
wananchi wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kujiunga na mfumo huu mpya wa
utangazaji na hakuna matatizo yaliyojitokeza zaidi ya changamoto kadhaa
ambazo zimeendelea kupatiwa ufumbuzi. Ikumbukwe kuwa uzimaji wa
urushaji wa matangazo katika mfumo wa analojia na kuanza kutumika kwa
mfumo wa dijitali umefanywa mahali ambapo kuna mawimbi (signal) ya
televisheni ya dijitali tu. Pale ambapo hakuna mawimbi ya
televisheni ya dijitali, matangazo ya televisheni yameendelea kurushwa
katika mfumo wa analojia hadi wakati ambapo mawimbi ya televisheni ya
dijitali yatakapofikia mahali hapo. Hivyo, kwa mfano katika
Jiji la Mwanza ambapo urushaji wa matangazo katika mfumo wa dijitali
ulisitishwa tarehe 28 Februari 2013, maeneo yaliyoguswa na usitishaji wa
matangazo hayo ni Mwanza City, Sengerema, Ukerewe na Kisesa. Sehemu nyingine zote za Mkoa wa Mwanza bado zinaendelea kupokea matangazo ya televisheni katika mfumo uliokuwepo hapo awali.
Vivyo hivyo, uzimaji wa matangazo katika Jiji la Tanga umegusa maeneo
ya Jiji la Tanga, Muheza, Mkanyageni, Nguvu Mali, Mabokweni na Mkinga. Maeneo mengine kama vile Lushoto, Korogwe, Handeni yanaendelea kupokea matangazo katika mfumo uliokuwa unatumika hapo awali.
Hivyo, katika maeneo ambayo hakuna uzimaji wa mitambo ya analojia
umefanywa, wananchi wanaendelea kupata matangazo ya televisheni kwa
kutumia mfumo uliokuwepo hapo awali. Serikali inapenda
kuwakumbusha wananchi kuwa katika maeneo ambayo tayari kuna matanagzo ya
televisheni katika mfumo wa dijitali, watumiaji wa televisheni
wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanapata matangazo ya televisheni zote zenye
leseni za kitaifa bila gharama yoyote ile ya ziada mbali na gharama ya
kununua king’amuzi (kisimbuzi) ambacho kinawezesha kuona matangazo
katika mfumo mpya wa utangazaji wa dijitali. Stesheni hizo ni
TBC1, ITV, Star TV, Channel 10, na East African TV. Endapo matangazo ya
televisheni ya vituo hivyo hayapatikani, wananchi wawasiliane mara moja
na watoa huduma za ving’amuzi ili kuwasaidia kupatia ufumbuzi.
Serikali inatumia fursa hii, kuwashukuru na kuwapongeza wananchi kwa
kuitikia vyema wito wa kuhamia katika mfumo wa utangazaji wa dijitali
katika maeneo yote yaliyohusika na uzimaji wa mitambo ya utangazaji wa
analojia. Aidha, Serikali inavishukuru na kuvipongeza vyombo
vya habari ambavyo vimekuwa mstari wa mbele katika kuelimisha umma
kuhusu mabadiliko haya ya mfumo wa utangazaji. Serikali itaendelea kutoa
elimu na kuhamasisha wananchi kwa kutumia njia mbalimbali, ili Tanzania
iwe imekamilisha uhamiaji katika mfumo mpya wa utangazaji kabla ya
tarehe 17 Juni 2015. Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni,
Serikali imeshuhudia kauli mbalimbali zinazotolewa na baadhi ya wamiliki
wa vyombo vya habari na hasa wa utangazaji kupitia vyombo vya habari
wanavyovimiliki, wakiilaumu na kuishutumu Serikali kuhusu uamuzi halali
wa Serikali wa kuhamia katika mfumo wa dijitali. Kauli hizo
zilizotolewa kwa nguvu kupitia mikutano ya waandishi wa habari na pia
kuhusisha mijadala katika baadhi ya redio na televisheni zina nia ya
kufifisha mchakato wa uhamaji kutoka mfumo wa utangazaji wa analojia
kwenda mfumo wa dijitali. Kauli hizi sio za kweli, zinapotosha
ukweli na hali halisi na pia zinalenga kuchochea wananchi kutokubaliana
na maamuzi haya ya Serikali na pia kutounga mkono juhudi za Serikali
ilizokwishafanya katika kutekeleza azma ya uhamaji kutoka utangazaji wa
mfumo wa analojia kwenda dijitali. Kauli hizo si tu
zimewachanganya wananchi wanaoendelea kuhamia katika mfumo mpya
utangazaji wa dijitali, bali pia zimetia hofu vyombo vya fedha ambavyo
vimekuwa vikitoa mikopo kwa wajenzi wa miundombinu ya urushaji wa
matangazo katika mfumo wa dijitali. Madhara ya kauli hizo ni
kuwapotosha wananchi kuhusu suala zima la uhamiaji katika mfumo wa
utangazaji wa dijitali na pia kukwamisha juhudi za Serikali kuhakikisha
zoezi la kuhamia dijitali linafanikiwa kabla ya kufikia ukomo wa
matangazo ya analojia tarehe 17 Juni 2015. Serikali inapenda
kuwafahamisha wananchi kwa mara nyingine tena, Serikali ilifikia maamuzi
ya kuhamia dijitali kwa kuzingatia maslahi ya taifa wananchi msikubali
kupotoshwa kwa ajili ya maslahi binafsi. Upotoshaji huu
unaweza kusababisha wananchi kukosa taarifa muhimu ikiwa ni pamoja na
kupata taarifa mbalimbali za maendeleo au matukio ya ndani na nje ya
nchi; kufuatilia mijadala bungeni na pia kufuatilia mchakato wa kuandaa
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, upotoshaji
unaofanywa unaweza kusababisha hasara kubwa kwa wananchi ambao
wataendelea kununua televisheni zinazotumia mfumo wa analojia. Vile
vile, upotoshaji huo utachelewesha wananchi kutumia huduma nyingine
nyingi zinazoendana na teknolojia ya utangazaji ya dijitali ikiwa ni
pamoja na huduma za Intaneti, huduma za kifedha, ununuzi wa vitu kwa
njia ya mtandao na kupata chaneli nyingine za ziada. Baadhi ya
wamiliki hao wa vyombo vya habari wanatambua wazi kuwa walikuwa na fursa
kwa zaidi ya miaka 7 kuwasilisha maoni au malalamiko yao kwa vyombo
husika ili kama kuna changamoto katika uhamiaji huo ziweze kufanyiwa
kazi, badala ya kutumia muda mwingi wa matangazo katika vyombo vyao vya
habari kupotosha umma kuhusu dhana nzima na mchakato wa uhamaji kutoka
mfumo wa utangazaji wa analojia kwenda dijitali. Kwa kuwa
upotoshaji huu unaongozwa na wamiliki wa vyombo vya habari ambavyo kwa
namna moja au nyingine vinahusika na ujenzi wa miundombinu ya urushaji
wa matangazo katika mfumo wa dijitali, Serikali iko tayari kushirikiana
na wadau hao katika kutatua changamoto zinazowakabili ili kuhakikisha
kuwa utekelezaji wa uhamiaji katika mfumo wa utangazaji unaendelea kama
ilivyopangwa badala ya kutumia muda mwingi kuupotosha umma.
Ikumbukwe kuwa mabadiliko haya hayaepukiki, hivyo basi wadau wote kwa
pamoja hawana budi kushirikiana katika mchakato mzima kama
ilivyokubalika kupitia vikao mbalimbali vilivyofanyika toka mwaka 2005
vikishirikisha wadau wote wa Sekta ya Utangazaji, wakiwemo wamiliki wote
wa vyombo vya habari vya utangazaji wa televisheni nchini.
Serikali imejiridhisha kuwa mchakato wote wa kuelekea mfumo wa
utangazaji ulifanywa kwa umakini mkubwa na kwa muda wa kutosha, elimu
imetolewa na inaendelea kutolewa. Aidha, ni dhahiri kuwa watoa
huduma za miundombinu ya dijitali waliopewa leseni tangu 2010
wameendelea na wajibu wa kuweka mitambo ya dijitali sehemu mbalimbali
nchini na zoezi linaendelea vizuri. Serikali haitavumilia
kikundi au mtu yeyote atakayeonekana kupotosha au kufifisha mchakato wa
kuhamia katika mfumo wa utangazaji wa dijitali. Aidha,
Serikali inaiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kuendelea na
utaratibu, ratiba ya zoezi zima la uzimaji wa mitambo ya analojia kama
ilivyotolewa na Serikali. Vile vile, Serikali inaiagiza
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kupitia Kamati ya Maudhui kuchunguza
endapo kauli zilizotolewa na baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari kwa
kutumia muda mrefu kuelezea kauli zao katika vyombo vyao vya habari
kama hawakukiuka sheria na kanuni za Utangazaji kwa nia ya kupotosha
umma kwa kusudio la kudhoofisha maamuzi haya ya Serikali.
Pamoja na tathmini ya awali ambayo Serikali, kupitia Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania imefanya na kuonyesha kuwa mchakato wa uhamaji
unaendelea vizuri, Serikali itafanya tathmini ya kina baada ya kumaliza
awamu ya kwanza ya uzimaji wa mitambo ya kurushia matangazo ya analojia
kwenye miji 7 ambayo kwa sasa inapata matangazo kupitia mfumo wa
utangazaji wa dijitali. Tathmini hiyo itaendana na kufanya
mkutano wa wadau wote wa utangazaji nchini ili kuweza kupata maoni yao
kabla ya kuanza awamu ya pili ya uzimaji kwenye miji 14 ambayo itapata
huduma za matangazo ya dijitali hivi karibuni. Serikali inaomba
wananchi kupuuza upotoshaji unafanywa kuhusu ukweli wa mabadiliko ya
mfumo wa utangazaji wa kutoka analojia kwenda dijitali. Aidha,
tunaomba vyombo vya habari kuendelea kutoa ushirikiano na kuendelea
kuunga mkono juhudi hizi muhimu kwa kuelimisha umma kuhusu ukweli katika
mchakato wa uhamiaji katika mfumo wa utangazji wa dijitali.
Serikali itaendelea kupokea maoni kutoka kwa wadau ili kuhakikisha kuwa
uhamiaji unakamilika mapema kabla ya ukomo wa matangazo ya analojia
tarehe 17 Juni 2015. Imetolewa na: Prof. Makame M. Mbarawa (Mb.) Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia DAR ES SALAAM 2 Aprili 2013
0 comments:
Post a Comment