Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Federick Werema.

SAKATA la Watanzania wanaodaiwa kuficha fedha nchini Uswisi, jana liliibuka tena bungeni mjini Dodoma, huku Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Federick Werema, akisema kazi ya uchunguzi bado ni ngumu.
Jaji Werema, alilazimika kujibu swali hilo, baada ya Naibu Waziri wa Fedha, Janeth Mbene, kushindwa kulitolea ufafanuzi swali lililoulizwa na Mbunge Kisesa, Luhaga Mpina (CCM).

Katika swali lake, Mpina alitaka kujua kama kamati iliyoundwa na Serikali kuchunguza utoroshaji wa fedha nchini Uswisi, itashughulikia pia utoroshaji wa fedha katika nchi nyingine.

Mpina, alisema katika kitabu cha awali cha Mpango wa Taifa wa Maendeleo kulikuwepo na kipengele kilichozungumzia utoroshaji wa fedha nje ya nchi, lakini anashangaa rasimu ya mwisho ya mpango wa suala hilo, limeondolewa kinyemela.

Katika maswali yake, Mpina pia aliungwa mkono na Mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM), ambaye alitaka kujua lini Kamati ya Serikali iliyoundwa kuchunguza utoroshaji huo, itapeleka majibu bungeni.

Jaji Werema, alisema kwa bahati mbaya kazi ya kuchunguza utoroshaji huo, imekuwa ngumu, lakini bado ahadi ya kupeleka majibu bungeni ipo palepale.

“Tutajitahidi tutaleta majibu bungeni, lakini kazi ni ngumu, kamati inafanya kazi na Waziri Mkuu ataleta taarifa kuhusu shughuli za Kamati,” alisema Werema.

Akisaidia kujibu maswali hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, alisema hana uhakika suala la utoroshaji wa fedha nje ya nchi kama lilikuwepo katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo.

“Namuahidi mheshimiwa mbunge, tutakaa pamoja na wataalamu wa Tume ya Mipango na kupitia vitabu vyote vya awali na cha sasa,” alisema Lukuvi.

Awali akijibu swali la msingi la Mpina, Naibu Waziri wa Fedha, Janeth Mbene, alisema swali alilouliza Mpina linatokana na hoja ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA) wakati wa Bunge la Novemba, mwaka jana.

Alisema hoja hiyo, inafanyiwa kazi na kamati maalum ya kitaifa iliyoundwa na Serikali.

“Kwa kuwa Azimio la Bunge, linaitaka Serikali kutoa taarifa kamili bungeni baada ya kulifanyia kazi, tunaahidi pindi kazi hiyo itakapokamilika, Serikali itatoa taarifa kamili kuhusiana na suala hilo,” alisema Mbene.

Katika swali lake la msingi, Mpina alitaka kujua Watanzania waliotorosha fedha nchini na hatua zilizochukuliwa.

Mpina alisema katika kipindi cha miaka 39, Tanzania imepoteza Sh trilioni 11.6 na kushika nafasi ya 13, kati ya nchi bora kwa utoroshaji wa fedha za umma kwenda katika mabenki ya dunia.

Itakumbukwa Novemba, mwaka jana mamlaka nchini Uswisi, zilitoa masharti magumu kwa Serikali ya Tanzania ambayo yalitakiwa yatekelezwe kabla ya kutoa ushirikiano wa kufichua fedha zinazodaiwa kuibwa na kufichwa katika benki kadhaa za nchini humo.

Serikali ya Uswisi, iliitaka Tanzania ikabidhi majina ya vigogo wote wanaotuhumiwa kukwapua mamilioni ya fedha.

Sharti la pili, mamlaka za Tanzania zilitakiwa ziwe na ushahidi usio na shaka kuwa mabilioni hayo yalipatikana kwa njia chafu au rushwa. Hiyo ni pamoja na mhongaji na mhongwaji (majina), namna rushwa ilivyotolewa na zaidi ya yote, ushahidi wa kuonyesha fedha hizo zimetokana na kampuni zinazotuhumiwa kuwa za mafuta.

Lakini Serikali ya Tanzania, ilikubali kulifanyia kazi suala hilo na kuwasilisha ripoti bungeni Aprili, 2013, kufuatia mjadala mkali kuhusu hoja binafsi iliyowasilishwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA).

Itakumbukwa Juni, mwaka huu, Benki ya Taifa ya Uswisi ilitoa taarifa kuhusu watu mbalimbali duniani wenye akaunti nchini humo ambapo raia wa Tanzania walielezwa kuweka jumla ya dola za Marekani milioni 196 (Sh bilioni 314).

Kwa muda mrefu sasa, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, amekuwa akisisitiza kuwa kuna Watanzania wameficha kiasi cha dola za Marekani milioni 196, ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 300 na Serikali imeshindwa kuwachukulia hatua.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top