Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa
Ujumbe wa amani na tahadhari ya umakini kwenye utoaji maoni
kwenye Katiba ndiyo vilitawala wakati wa misa za Sikukuu ya Pasaka
zilizofanyika sehemu mbalimbali nchini jana na juzi.
Miongoni mwa waliotoa hotuba wakati wa sikukuu
hiyo ni pamoja na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, ambaye
alikuwa mkoani Mtwara; na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aliyekuwa
jijini Dar es Salaam.
Mkapa akataa udini
Rais mstaafu Mkapa alitumia fursa ya kutoa salamu
katika Kanisa Katoliki mjini Masasi kuliasa taifa kujiepusha na utoaji
wa maoni ya Katiba kwa misingi ya dini.
Mkapa alisema katiba ijayo haipaswi kuwa na itikadi za kidini kwa kuwa zinaweza kuliangamiza taifa.
“Wapo watakaopata uwakilishi kupitia rasimu ya
Katiba ya nchi. Namwomba Mwenyezi Mungu awape mwanga, muhakikishe jambo
moja tu ambalo litakuwa msingi mkubwa wa amani na maendeleo na umoja wa
taifa letu.
Watupatie Katiba ambayo inatoa fursa kamilifu ya kila mtu kuwa na imani yake.
“Katiba inayoheshimu imani ya kikatiba na imani
zote zinazofanywa na wananchi wa Kitanzania…Vilevile ihakikishe kwamba
dola au nchi yetu haina imani rasmi kama vile nchi yetu isivyo ya kabila
moja, hivyo haiwezekani kuwa na Katiba ambayo inatambua kwa dhana au
maandalizi ya vipengele mbalimbali kwamba kuna udini, haiwezekani.”
Askofu na Muungano
Watanzania wametakiwa kuwapuuza watu wanaohubiri
kuuvunja Muungano kwani watu hao wana agenda binafsi ambazo si kwa faida
au masilahi ya nchi, bali wao na baadhi ya mataifa yanawafanya vibaraka
wa kuvuruga amani na utulivu uliodumu kwa miaka mingi.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mhashamu Askofu
Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki la Dodoma wakati wa misa ya Pasaka
ambayo ilifanyika kitaifa katika Kanisa Kuu la Kiaskofu la Mt. Paulo
wa Msalaba mjini humo.
Askofu Nyaisonga alisema hata kama kuna baadhi ya
matatizo katika Muungano, yanapaswa kuboreshwa badala ya kuuvunja kabisa
Muungano ambao kimantiki umeijengea nchi heshima.
Chanzo: Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment