Waziri Mkuu wa sasa, Mizengo Pinda akizungumza na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa.
RIPOTI ya tume iliyoundwa na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward
Lowassa mwaka 2006 kuchunguza ujenzi wa maghorofa katika Jiji la Dar es
Salaam, imemweka mahala pabaya na inaweza kumtoa kafara, Waziri Mkuu wa
sasa, Mizengo Pinda, Tanzania Daima Jumatano limedokezwa.
Pinda anatolewa kafara katika sakata la jengo la ghorofa 16
lililoporomoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam wiki iliyopita na
kusababisha vifo vya zaidi ya watu 40.
Kutokana na janga hilo, Pinda analalamikiwa kukalia ripoti ya Tume ya
Lowassa ambayo ilikuja na mapendekezo ya kukabiliana na maghorofa
yaliyojengwa chini ya kiwango.
Duru za siasa kutoka ndani ya Bunge zinasema kuwa tayari kuna baadhi
ya wabunge bila kujali itikadi zao, wameunganisha nguvu kutaka kumsulubu
Waziri Pinda katika mkutano ujao wa Bunge kupitia hoja binafsi au
maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu.
Mmoja wa mawaziri waandamizi wa serikali ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema: “Pinda anastahili kubeba mzigo, kwani
baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo alimwajibisha nani tangu 2008 hadi sasa?
“Kwa uzembe huu, Pinda ameshiriki kwa kuwa hakuwawajibisha waliojenga
kinyume na utaratibu hadi Watanzania wengine wakafa.
Zamu hii hata
akilia anahusika.” Mbunge wa Vunjo Augustino Mrema (TLP) alimshangaa
Waziri Pinda kwa kushindwa kuchukua hatua zilizopendekezwa na tume ya
Lowassa kwani ilipendekeza baadhi ya majengo yabomolewe na wahusika
wachukuliwe hatua.
Alisema athari ya ukimya huo ni kuendelea kuangamia kwa Watanzania kunakosababishwa na uzembe wa viongozi wa serikali.
“Hili tatizo la kushindwa kuchukua uamuzi mgumu litaendelea
kutugharimu kila siku, yale maghorofa yaliyotakiwa kubomolewa kipindi
kile hayajaguswa na hayataguswa kwa sababu ya kubebana, hili hatuwezi
kulinyamazia, lazima tukawashe moto bungeni,” alisema Mrema.
Alisema Watanzania hawapo tayari kuletewa danganya toto ya tume nyingine ikalete majibu ambayo tayari yako mezani kwa Pinda.
Mbunge wa CCM aliyeomba jina lake lihifadhiwe, alisema kitendo cha
Jeshi la Polisi kuwakamata watendaji wa Manispaa ya Ilala hakitoshi kama
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka
ataendelea kubaki ofisini.
Mrema ambaye amepata kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya
Ndani kwa nyakati tofauti, alisisitiza kuwa Waziri Tibaijuka anapaswa
aige mfano wa Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi na Lowassa walioamua
kuachia ngazi kutokana na uzembe wa watendaji wao.
“Kwa wenzetu leo inapotokea boti ikazama kwa uzembe na kupoteza
maisha ya watu watatu waziri mwenye dhamana anawajibika, iweje sisi leo
tuwachekee mawaziri wetu?” alihoji mbunge huyo.
Mbunge wa kuteuliwa na rais, James Mbatia, ameapa kuwasha moto katika Bunge lijalo hadi kieleweke.
Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, alisema lazima Waziri
Mkuu atoe majibu ya msingi kwa Watanzania kwanini hakutekeleza maazimio
ya tume ya Lowassa.
Alienda mbali na kuhoji utendaji wa kitengo cha maafa cha Waziri Mkuu
kwani kimekuwa kikishughulika kutoa vyakula vya misaada kwenye maafa
badala ya kudhibiti yasitokee.
“Tangu tume zianze kuundwa kuhusu maafa ni akina nani walichukuliwa
hatua? Kuanzia tume ya MV Bukoba hadi tume ya matokeo ya kidato cha nne,
Watanzania tumechoka
kuneemesha mifuko ya wajumbe wa tume na kufilisi rasilimali zetu,
hivyo Pinda, Tibaijuka lazima wajiuzulu,” alisema.
Wakati wabunge hao wakitaka Pinda na Tibaijuka waachie ngazi, habari
zaidi ndani ya serikali zinasema kuwa ripoti ya Tume ya Lowassa
haikufanyiwa kazi kwani baadhi ya majengo yaliyopendekezwa kubomolewa,
yanawahusu viongozi wa juu serikalini.
“Ile ripoti iliwasilishwa wakati Lowassa bado yuko madarakani.
Alishindwa kuifanyia kazi na haiwezi kufanyiwa kazi kwani baadhi ya
majengo yanawahusu viongozi au yanamilikiwa na watu wa karibu wa
viongozi, na ndio wachangiaji wakubwa wa fedha wakati wa kampeni,”
kilisema chanzo chetu cha habari.
Akifanya majumuisho katika hotuba ya matumizi ya ofisi yake bungeni
kwa mwaka 2008/09, Pinda alizungumzia jinsi Tume ya Lowassa ilivyofanya
kazi katika sakata la ghorofa kuanguka jijini Dar es Salaam.
Pinda alilithibitishia Bunge kuwa zaidi ya maghorofa 100 jijini Dar es
Salaam yalibainika kuwa yalijengwa kinyume na taratibu za ujenzi.
Kwa mujibu wa ripoti iliyoundwa na Lowassa, kati ya maghorofa 505 ambayo waliyakagua, 147 yalikutwa hayana nyaraka za ujenzi.
Lowassa aliunda tume baada ya jengo la hoteli ya Chang’ombe Village
Inn, Keko, Dar es Salaam kuanguka mwaka 2006 na kuua mtu mmoja na
kujeruhi wengine kadhaa. Ilidaiwa kwamba ulikuwapo ukiukwaji katika
ujenzi wake.
Pinda aliliambia Bunge kuwa tume hiyo ya Lowassa ilibaini pia
maghorofa 81 yalikutwa yamekiuka masharti ya ujenzi huku mengine 22
wenyewe hawakupatikana na yalikuwa yamejengwa bila kuzingatia sheria za
ujenzi pamoja na uzembe wa baadhi ya watendaji wakiwamo wahandisi wa
manispaa husika.
NHC yatoa kauli
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limesema kuwa mbia wao alikuwa na
vibali vya mamlaka zinazohusika kusimamia ujenzi wa majengo makubwa vya
kumruhusu kuongeza ghorofa 16 kutoka kumi za awali.
Kauli hiyo inakuja kukiwepo na mvutano kutoka mamlaka mbalimbali
ikiwemo Manispaa ya Ilala kwamba mbia wao huyo ambaye ni M/s Ladha
Construction alipewa kibali cha kujenga ghorofa kumi, lakini cha
kushangaza aliongeza nyingine sita bila taarifa na hivyo kusadikiwa kuwa
huenda ndiyo chanzo cha kuanguka kwa jengo hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa NHC, Nehemiah Mchechu akizungumza jana na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaa, alisema Agosti 22 mwaka jana
mbia wao huyo aliwataarifu kuwa ameshapata vibali kutoka mamlaka husika,
na kwamba angependa aingie nao mkataba mdogo kutambua ongezeko la
ghorofa hizo na mabadiliko ya tarehe ya kumaliza mradi.
“Shirika lilimjibu kuwa hakuna pingamizi kama mbia ataleta nakala ya
vibali kutoka mamlaka husika kwa ajili ya kumbukumbu za shirika na pia
ili kufikia hatua za maamuzi ya ndani na mawasiliano yote hayo yapo
kwenye rekodi zetu na endapo mamlaka husika itazihitaji tuzazipatia,”
alisema.
Kutokana na hali hiyo, aliutaka umma kutoliingiza shirika hilo katika
sakata hilo kwa madai kuwa zipo taasisi na vyombo vinavyokasimiwa
mamlaka ya kusimamia ubora wa ujenzi wa nyumba nchini, na NHC nayo
husimamiwa na taasisi na vyombo hivyo.
Chanzo: Tanzania Daima
Picha kwa hisani ya mtandao.
0 comments:
Post a Comment