Absalom Kibanda
JUHUDI za Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam
kuwanasa watuhumiwa waliomtesa na kumuumiza vibaya Mwenyekiti wa Jukwa
la Wahariri Nchini (TEF), Absalom Kibanda, huenda zikagonga mwamba
kutokana na utata uliopo, Tanzania Daima limedokezwa.
Taarifa za ndani ya jeshi hilo zinadai kuwa suala hilo limeanza
kuumiza vichwa huku baadhi ya askari wa chini wakikerwa na tabia ya
wakubwa wao kusuasua kulimaliza.
Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New habari (2006)
Ltd, wachapishaji wa magazeti ya Rai, The African, Mtanzania, Bingwa na
Dimba, alivamiwa Machi 3, mwaka huu, nyumbani kwake kisha kupigwa nondo
kichwani, kutobolewa jicho, kunyofolewa ukucha, kung’olewa meno mawili
na kukatwa kidole.
Wakati Kibanda akiendelea kupata matibabu nchini Afrika Kusini,
mwenendo wa uchunguzi wa sakata lake umezua mashaka kutokana na mlolongo
wa matukio yanayoibuliwa ili kujaribu kuzima mjadala huo.
Vyanzo vyetu kutoka ndani ya jeshi la polisi ambalo linaendelea
kupeleleza tukio hilo, vilisema kuwa baadhi ya askari hawaridhishwi na
kasi ndogo inayoonyeshwa katika kulipatia ufumbuzi badala yake jamii
imekuwa ikidhani linahusika.
“Suala hili kwa sasa limekuwa gumu, tangu Kibanda atekwe hadi sasa,
makachero tunaumiza vichwa, ingawa hatuwezi kusema wazi kuwa tumeshindwa
kuwabaini watu hao.
“Lakini ukweli unajidhihirisha kuwa hicho kikundi kilichomtesa Kibanda
kina wataalamu wa kazi hiyo na wala si majambazi au vibaka wa kawaida.
“Haya ni mateso ya watu maalumu wanaojua kutesa na hayo hufunzwa kwa watu maalumu kwenye vyuo maalumu,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kiliongeza: “Inasikitisha kiasi fulani watu wanataka
kujaribu kuanza kuhusisha suala la Kibanda na suala la watuhumiwa
waliokamatwa kwa masuala mengine kabisa ya kisiasa.
“Hata sasa huyu ambaye tumemshikilia hapa, zote hizi ni siasa tu, watu
wangependa mabega yao yapendeze, hali kama hii ikiendelea kukua ndani
ya jeshi itasababisha tudharaulike.”
Baadhi ya vyombo vya habari navyo vinadaiwa kutumiwa kulififisha suala
la Kibanda kwa kuibua mijadala ya kushambuliana vyenyewe kwa vyenyewe
hatua inayoonekana kuwepo kwa ajenda ya siri ndani yake.
“Ni kama vile haiwezekani, kusema kuwa tangu Kibanda ateswe eti hakuna
hata mtuhumiwa mmoja aliyetiwa mbaroni, hata na viongozi wetu wa jeshi
la polisi ukiwauliza, wanaanza kusema timu iliyoundwa kupeleleza suala
la Lwakatare (Wilfred) na Ludovick (Joseph) litashughulikia pia suala la
Kibanda.
“Haya mambo mawili ya Kibanda na Dk. Stephen Ulimboka kweli
yanatufedhehesha sana, tunaonekana tunafanya siasa badala ya taaluma ya
ukachero, hapa kuna baadhi ya wakubwa wanalindwa; sisi tunapelekeshwa
tu,” kilisisitiza chanzo chetu.
Zikiwa zimetimia siku 26 tangu kuteswa kwa Kibanda, tume ya polisi ya
wataalamu iliyoundwa na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es salaam,
Suleiman Kova, haijamkamata mtuhumiwa hata mmoja huku kamanda huyo
akikataa kuzungumzia maendeleo ya uchunguzi.
Tukio la Kibanda limekuwa likifananishwa na lile la Dk. Ulimboka
kutokana na utaaalamu uliotumika kuwatesa kufafana ingawa yalitendeka
maeneo tofauti.
Dk. Ulimboka ambaye alitekwa na watu wasiojulikana usiku wa Juni 26,
mwaka jana, hadi leo ni mtu mmoja amefunguliwa mashtaka baada ya
kujisalimisha kanisani akidai kuhusika na tukio hilo.
Mshtakiwa huyo, Joshua Mulundi, awali ilidaiwa na uongozi wa kanisa
alikojisalimisha kuwa alikuwa na matatizo ya akili lakini jeshi la
polisi limekuwa likisema upelezi wa tukio zima pamoja na uchunguzi wa
afya yake unaendelea.
Dk. Ulimboka mwenyewe alimtaja mara kadhaa, mtu aliyedai ni Afisa
Usalama wa Ikulu, Ramadhan Ighondu, kuwa alihusika kumteka na kumtesa,
ingawa hadi leo hajawahi kuhojiwa na polisi kuthibitisha hilo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment