Latest News

TENGA AMWAGA MIPIRA 1283 KUIMARISHA SOKA MIKOANI.
Rais wa TFF, Leodgar Tenga
 Watanzania wametakiwa kutoa msaada wa vifaa vya mpira wa miguu katika shule za msingi na sekondari kwa ajili ya kujenga na kuimarisha mchezo huo hapa nchini.
 
Akizungumza wakati wa akikabidhi mipira 1283 yenye thamani ya dola elfu 30 kwa vyama 32 vya mpira wa miguu hapa nchini,Rais wa TFF Leodgar Tenga amesema maendeleo ya mchezo huo yataletwa na watanzania wenyewe.Kila mkoa utapata mipira 25.

Mbali na mikoa hiyo pia taasisi za kukuza vipaji kama Azam
Academy,Lord Burden ni miongoni mwa taasisi zilizonufaika na msaada huo.
Rais huyo anayemaliza muda wake amesema msaada huo unatokana na fedha dola elfu 30 ambazo alizawadiwa na FIFA kwa kuweza kusuluhisha migogoro ya vyama vya soka katika nchi za Kenya,Sudan,Uganda na Kenya hivyo akaamua kuzikabidhi kwa TFF.
Tenga amesema maendeleo ya mpira yanataka kuhusisha wadau wengi na vipaji haviwezi kupatikana bila kuwa na vifaa kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo wazazi,walezi na jamii kwa ujumla.

Mkurugenzi mkuu wa ufundi wa TFF Sunday Kayuni amesema mchango uliotolewa na Leodgar tenga ni muhimu kwa maendeleo ya soka kwani vifaa kwa hivi sasa ni ghali na wazazi hawawezi kununua vifaa kwa ajili ya watoto.

 Nao makatibu Riziki Majala na Nassib Mabruki wa vyama vya soka mikoa Mwanza na Pwani  na mwenyekiti wa DRFA Almas Kasongo wamesema msaada huo ni muhimu kwa hivi kutokana na uhaba mkubwa wa vifaa unaotokana ukata wa fedha.

Soka la vijana ndiyo msingi wa maendeleo ya mpira wa miguu lakini changamoto kubwa imekuwa ni namna ya kuvumbua vipaji,kuendeleza na kupata vifaaa.

Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) lilimpa Rais Tenga fedha hizo ikiwa ni shukrani kwake kwa kushughulikia mgogoro wa uongozi wa mpira wa miguu nchini Kenya uliodumu kwa miaka miwili; ambapo nchi hiyo kutokana na mgogoro huo ilikuwa na vyama viwili (KFF na FKL).

 “Dhamira yangi si kushukuru kwa hafla hii, bali kutoa sababu kwa nini nimefanya hivi. Ninaamini kwa kuanzia mipira ndiyo muhimu, pili kwa kufanya hivi itaonekana kweli mipira imegawiwa,” amesema Rais Tenga.

Amesema moja ya ndoto zake wakati anaingia kuongoza TFF mwaka 2004 ameshindwa kutimiza ni kusaidia mipira, kwani uwezo wa kununua mipira kwa wanaocheza katika ngazi ya chini hasa watoto haupo.

“Hizi kelele zote za maendeleo ya mpira wa miguu ni kwa sababu shuleni hakuna vifaa. Nia yangu ilikuwa shule zote zipate mipira, lakini hiyo ni moja ya ndoto nilizoshindwa kutekeleza. Vipaji haziwezi kupatikana kama watoto hawachezi.

“Tunashukuru sana kwa Serikali kurejesha mpira shuleni. Hata
nitakapoondoka madarakani nikipata nafasi nitaendelea kuomba mipira kwa ajili ya shule,” amesema Rais Tenga.

Vyama vya mikoa ambavyo jumla ni 32 (Tanzania Bara na Zanzibar) kila kimoja kimekabidhiwa mipira 25 (kumi saizi namba tano, 15 saizi namba nne kwa ajili ya vijana). Kwa academies ambazo ni 21 kila moja imepewa mipira 25 (minane saizi namba tano, na 15 saizi namba nne).


KIPINGU AMPIGIA CHAPUO TENGA.
 
                                            Iddi Kipingu          

Lakini kwa upande mwingine Watanzania wametakiwa kuthamini michango ya wadau nchini kwani wamewezesha uthabiti na kuendelea kwa mpira wa miguu nchini badala ya kuwasema kwa maneno mabaya kila uchao.

Mwenyekiti  mstaafu wa Baraza la Michezo Tanzania BMT Kanali mstaafu Iddi Kipingu amesema katika uongozi wa Leodgar Tenga TFF iliweza kusimama na kuimarisha uhusiano na taasisi nyingine kiwemo serikali.

Kipingu amesema tenga kama binadamu anaweza kuwa na upungufu wake lakini mchango wake uthaminiwe na Watanzania.
Leodgar Chilla Tenga aliingia madarakani mwaka 2004 huku akitaraji kung’atuka mara baada ya uchaguzi mkuu kufanyika kuwapata viongozi wapya baadaye mwaka huu.

COASTAL, AZAM KUCHEZA SIKU YA MUUNGANO
 
Timu za Coastal Union ya Tanga na Azam zitapambana Aprili 26 mwaka huu katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) itakayofanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Awali mechi hiyo namba 168 ilikuwa ichezwe Aprili 27 mwaka huu, lakini imerudishwa nyuma kwa siku moja ili kuipa fursa Azam kujiandaa kwa mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco.

Mechi hiyo itachezeshwa na Andrew Shamba kutoka mkoani Pwani
akisaidiwa na Abdallah Mkomwa (Pwani), Vicent Mlabu (Morogoro) wakati mwamuzi wa mezani atakuwa Mohamed Mkono wa Tanga. Charles Komba wa Dodoma ndiye atakayekuwa Kamishna wa mechi hiyo ya raundi ya 24.

Baada ya mechi ya Tanga, Azam itarejea Dar es Salaam siku inayofuatatayari kwa safari ya kwenda Rabat itakayofanyika Aprili 28 mwaka huu.
 

Mechi hiyo itachezwa wikiendi ya Mei 3, 4 au 5 mwaka huu.
Keshokutwa (Aprili 24 mwaka huu) kutakuwa na mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya African Lyon na JKT Ruvu itakayochezwa Uwanja wa Azam Chamazi, Dar es Salaam.

Iwapo Azam itafanikiwa kusonga mbele katika michuano ya Kombe la Shirikisho kutakuwa na marekebisho ya ratiba ya VPL. Hiyo ni kutokana na raundi inayofuata ya Kombe la Shrikisho kuchezwa wikiendi ya Mei 17, 18 na 19 mwaka huu ambapo bado haijajulikana Azam itaanzia wapi (nyumbani au ugenini) iwapo itavuka.

Mechi nyingine za VPL mwezi ni Aprili 25 (Ruvu Shooting vs Simba- Uwanja wa Taifa), na Aprili 28 (Simba vs Polisi Morogoro- Uwanja wa Taifa).

WAMOROCCO WA AZAM WAINGIZA MIL 50/-

Mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho kati ya Azam na AS FAR Rabat ya Morocco iliyochezwa juzi (Aprili 20 mwaka huu) imeingiza sh. 50,850,000.
Fedha hizo katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam na kumalizika kwa timu hizo kutoka suluhu zimetokana na
watazamaji 8,268 waliokata tiketi.

Viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 10,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh.
20,000 na sh. 30,000 ambacho kilikuwa kiingilio cha juu kwa jukwaa la VIP A. Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo walikuwa 7,354.

Mgawo ulikuwa kama ifuatavyo; gharama za tiketi sh. 5,575,500, asilimia 15 ya uwanja sh. 6,791,175, asilimia 10 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 4,527,450 na asilimia 75 iliyokwenda kwa klabu ya Azam ni sh. 33,955,875.

Mechi iliyopita ya Azam katika michuano hiyo dhidi  ya Barrack Young Controllers II ya Liberia iliingiza sh. 44,229,000 kutokana na watazamaji 17,128 waliokata tiketi. Viingilio vilikuwa sh. 2,000, sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 20,000 ambacho kilikuwa kiingilio cha juu kwa jukwaa la VIP A.

MECHI YA JKT RUVU, YANGA YAINGIZA MIL 66/-

Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya JKT Ruvu na Yanga iliyochezwa jana (Aprili 21 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 66,568,000 kutokana na watazamaji 11,864.
Viingilio katika mechi hiyo namba 106 iliyomalizika kwa Yanga kutoa dozi ya 3-0 kwa wenyeji wao vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 15,702,752.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 10,154,440.68.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh.
7,984,450.40, tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 4,790,670.24, Kamati ya Ligi sh. 4,790,670.24, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,395,335.12, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) sh. 931,519.21 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 931,519.21.


MTANDAO WA WASANII TANZANIA (SHIWATA)
Peter Mwenda
WASANII chipukizi 300 kutoka vikundi 15 jijini Dar es Salaam wamejitokeza kushiriki maonesho ya kukuza vipaji yaliyoandaliwa na Mtandao wa Wasanii Tanzania (SHIWATA) Jumamosi ya Aprili 27 katika ukumbi wa hoteli ya StarLight ,Mnazi Mmoja Dar es Salaam.

Vikundi ambavyo vimethibitisha kushiriki pamoja na Kaole Sanaa
Group,Splendid,Uyoga Boga na vingine katika fani ya Bongo Flava, Taarab, Maigizo, Ngoma ,Mazingaombwe, Sanaa za Ufundi,Kung Fu,Sarakasi,Kusheki,Kwaya,na Ngonjera.
Maonesho kama haya yatafanyika kila mwezi na kiingilio ni bure na
vikundi vingine ni Super Shine Morden Taarab,Zijiu,Edeneza Brass
Band,Asili Africa, Mege Arts,Kintu,Army Kwanza, Wachapakazi, Tanhope,
Tanz Arts,Mshikamano,Big House,Lutenga Boys, Kilimasta, Manuary.
 
Madhumuni makubwa ya tamasha hilo ni kuibua vipaji vya wasanii
chipukizi ili kazi zao ziweze kupata soko hivyo mapromota, Majd, Maproducer wa filamu wasikoke kufika katika maonesho hayo ili kuona mastaa chipukizi ambao ambavyo vipaji vyao bado havijaonekana.

Vijana wa sanaa mbalimbali wanatakiwa kufika katika ofisi za SHIWATA zilizopo Bungoni Ilala ili kujisajili kwa ajili ya maonesho mengine yanayofuata .

Tanzania kuna wasanii wengi wenye vipaji lakini kazi zao hazisikiki
wala kuonekana kwenye vyombo vya habari hivyo hiyo ni fursa kutumia maonesho hayo kama soko la kazi zao katika jiji la Dar es Salaam.

Wasanii mbalimbali ambao vipaji vyao vitakubalika sokoni watanufaika kupata ajira ya kuuza kazi zao pamoja na kushiriki katika matamasha mbalimbali ndani na nje ya nchi.

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top