Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh amemuweka kitanzini aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), William Mhando, baada ya kushauri ashtakiwe pamoja na mkewe, Clara, kutokana ukiukwaji wa sheria katika kutoa zabuni.
 
Mbali na Mhando, wengine ambao CAG amependekeza wachukuliwe hatua za kisheria ni Mkurugenzi wa Kampuni ya McDonald Live Line Technology, watu wote walioingia katika biashara na Tanesco kinyume cha sheria pamoja na wafanyakazi waliohusika kutoa zabuni hizo.
Mapendekezo hayo ya CAG, Utouh yamo katika ripoti yake ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma ya 2011/12, aliyoiwasilisha bungeni wiki iliyopita ikirejea ukaguzi maalumu uliofanyika katika shirika hilo kutokana na maombi ya bodi ya wakurugenzi ya shirika hilo.
CAG pia ameweka wazi kuwa Tanesco iligubikwa na ukiukwaji uliokithiri wa Sheria ya Ununuzi ya 2004 na kanuni zake za mwaka 2005, uliosababishwa na viongozi wake wa juu.
“Mkurugenzi Mkuu wa Shirika akiwa ndiye mwenye uamuzi wa kuhusu ununuzi, alishindwa kuzuia ukiukwaji huu wa sheria ya ununuzi na mara nyingi aliidhinisha ununuzi wa chanzo kimoja au usiozidi ushindani,” inasema ripoti hiyo na kuongeza:
“Bodi inatakiwa kuripoti kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DPP) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) yale yote yaliyogunduliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa kubaini kuwapo kwa rushwa na ubadhirifu.”
Katika ripoti hiyo, CAG amebainisha ukiukwaji mkubwa wa sheria uliofanywa na Mhando, huku akibainisha kuwa mkewe, ambaye ni Mtendaji wa Mkuu wa Kampuni za Santa Clara Supplies Company Limited, alipewa zabuni katika shirika hilo kwa kutumia taarifa za kughushi.
Pia CAG amebainisha kuwa kampuni hiyo haikuwasilisha katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), rejesho la kodi kiasi cha Sh4.854 milioni ilizolipwa na Tanesco.

Santa Clara.
CAG amebainisha kuwa kampuni hiyo iliyosajiliwa Aprili 18, 2011, ilipewa Leseni ya Biashara, Mei 2011 na kwamba wakurugenzi na wanahisa wa kampuni ni mke na watoto wawili wa Mhando.
Mke wa Mhando aliwahi kuwa mfanyakazi wa Tanesco, lakini aliacha kazi baada ya mumewe kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu.
CAG amebainisha kampuni hiyo iliingia mkataba na Tanesco na kupewa zabuni Namba PA/001/11/HQ/G/011 ya ugavi wa vifaa vya ofisi, vifaa vya matumizi ya kompyuta na mashine za kudurusu, kwa mwaka 2011 hadi 2012, mkataba ulianza Desemba 20, 2011.
Mwananchi 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top