WAKATI Aprili 12 ilikuwa siku ya kumbukumbu ya kifo cha Waziri
Mkuu aliyeweka historia ya pekee nchini, Edward Moringe Sokoine, Bunge
la Jamhuri ya Muungano limeshindwa kumkumbuka hata kwa dakika moja.
Ingawa hakuna sheria inayolitaka Bunge kufanya kumbukumbu ya aina
yoyote ya kifo chake, lakini limekuwa na utamaduni wa kuitangaza siku
hiyo bungeni na wakati mwingine kusimama kwa dakika moja.
Ijumaa iliyopita siku ya maadhimisho ya kumbukumbu yake, Spika wa
Bunge Anne Makinda aliyekuwa akiongoza kikao cha Bunge, hakutangaza
wala kusema neno lolote juu ya siku hiyo.
Mmoja wa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliliambia gazeti hili
kuwa inawezekana spika na wabunge waliokuwepo ukumbini siku hiyo,
walipitiwa na ndiyo maana hakukuwa na neno lolote kutoka kwao.
"Bunge hili lina mambo mengi, mara ugaidi, mara kanuni, inawezekana kabisa spika amepitiwa," alisema mbunge huyo.
Wakati Bunge likisahau kumkumbuka Sokoine, mjini Monduli kulikuwa na
maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha kiongozi huyo ambaye hadi leo
anatajwa kama kiongozi jasiri mwenye uthubutu.
Baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa na wabunge, walipata fursa ya kuhudhuria kumbukumbu hiyo.
Hadi sasa ni miaka 29 tangu mtendaji huyo mkuu wa serikali na kiongozi wa shughuli za serikali bungeni alipofariki dunia.
Sokoine alifariki dunia Aprili 12 mwaka 1984 eneo la Wami-Dakawa akiwa njiani kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam.
Ilikuwa majira ya saa kumi jioni, Mwalimu Julius Nyerere alipotangaza kifo chake kwa sauti ya huzuni.
Sokoine alikuwa kiongozi wa kweli ambaye daima alisimama upande wa umma.
Wengi wanamuelezea kwamba alikuwa kiongozi wa mfano wa kuigwa kwani aliishi kama alivyohubiri.
Sokoine si tu kwamba hakujilimbikizia mali, bali pia alipunguza hata
mali zake ili apate nafasi zaidi ya kuwatumikia Watanzania.
Itakumbukwa kwenye kikao cha Bunge cha Aprili 1984, Sokoine
alikabiliana na hoja za wabunge kutaka kuongezewa posho na marupurupu
yao ambapo alitamka: “Ndugu Spika, niko tayari kuwaongezea wabunge
posho ya chakula chao, lakini kamwe sitakuwa tayari kuwaongezea
mishahara na marupurupu mengine."
Baada ya kikao kile cha Bunge, Sokoine badala ya kupanda ndege ya
serikali kumrudisha Dar es Salaam, aliamua kurudi kwa njia ya barabara,
apate nafasi ya kuona shughuli za maendeleo.
Wakati huo huo, mjadala wa hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, unaendelea tena leo na unatarajia kuhitimishwa kesho.
Tanzania Daima
Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment