WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amekutana na wakuu wa taasisi za kimataifa za
WFP, IFAD na FAO na kufanya nao mazungumzo kuhusu namna ya kuendeleza kilimo
nchini Tanzania.
Waziri Mkuu amekutana na viongozi hao Alhamisi (Machi 21, 2013)
alipowatembelea kwenye ofisi zao jijini Roma, Italia kila mmoja kwa nyakati
tofauti.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa
Mtaifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Bi. Ertharin Cousin, alimweleza
Waziri Mkuu kwamba shirika lake litaendelea kutumia bandari ya Dar es Salaam
kusafirishia vyakula kwenda nchi zenye uhitaji wa chakula ikiwa ni utekelezaji
wa mpango wa ununuzi wa bidhaa kwa maendeleo (Purchase for Progress Programme).
“Tumekubaliana na wadau tunaoshirikiana nao, tuendelee kutumia bandari ya
Dar es Salaam kupeleka mizigo Sudan ya Kusini na Uganda kwa sababu ya amani
iliyopo nchini Tanzania. Kwa hiyo muamini kwamba sisi ni wadau wenu wa karibu
na wa kuaminika,” alisema Bi. Cousin.
Akitoa mfano, Bi. Cousin alisema:
“Kuna wakati kulikuwa na njaa kubwa kule Somalia na Zambia wakawa na hifadhi
kubwa ya mahindi, lakini tulishindwa kusafirisha mahindi kutoka huko na
kuyapeleka yanakohitajika kwa sababu ya hali mbaya ya usalama kwenye ukanda wa
magharibi,” alisema.
Akizungumzia kuhusu ukuaji wa miji na kasi ya watu kuhamia mijini, Bi.
Cousin alionya kwamba kuna haja ya kuwianisha uendelezaji wa miundombinu kwenye
maeneo ya mijini na yale ya vijijini ili kuepuka tatizo la msongamano mkubwa wa
watu mijini linalozikabili nchi nyingi zinazoendelea.
Alisema shirika lake limefanya utafiti nchini India na kubaini kuwa kadri
kiwango cha ukuaji wa miji kinavyoendelea ndivyo kasi ya wakazi kuongezeka
inavyozidi. “Tumeziainisha nchi za Kenya, Tanzania na Ethiopia na kuziweka
kwenye mpango maalum ili zijipime jinsi zitakavyokuwa katika miaka 20 ijayo ili
zisije kuwa na hali kama ya India hivi sasa,” aliongeza.
Naye, Rais wa Shirika la Kimataifa Kuendeleza Kilimo na Chakula
(IFAD), Dk. Kanayo Nwanze alimweleza Waziri Mkuu kwamba shirika lake limeandaa
mpando wa miaka mitatu ambao utazihusisha nchi 30 ikiwemo Tanzania ambazo
zitafanyiwa impact evaluation kulingana na misaada ambayo zimekuwa
zikipatiwa na shirika hilo.
“Tunataka tuangalie hali halisi kule Vijijini, je maisha ya wananchi
yamebadilika kulingana na misaada ambayo tumekuwa tukiitoa? Je, wakulima
wameongeza uzalishaji? Je wakulima wameunganishwa na masoko? Je, taasisi za
kifedha zinawajali wakulima wadogo?” alifafanua Rais huyo wa IFAD.
Alisema hivi sasa wameanza kukusanya takwimu za awali (baseline data)
katika nchi husika kabla ya kuanza kufanya tathmini itakayoanza mwaka huu hadi
mwaka 2016.
Mapema, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula
na Kilimo (FAO), Bw. Jose Graziano da Silva alimweleza Waziri Mkuu kwamba
shirika lake limetiliana saini makubaliano na benki ya Rabo (Rabobank) ili
iweze kuwasaidia wakulima waliojiunga kwenye vyama vya ushirika.
“RaboBank imekubali kufanya kazi
hiyo na imeichagua Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zitakazokuwa waanzilishi wa
mpango huo (pilot project)… watawasiliana nanyi muda si mrefu kuhusiana
na suala hili,” alisema.
Aliomba wakati mpango huo
utakapoanza, wakulima wa Tanzania wawe tayari kushiriki kwenye mpango huo.
Waziri Mkuu Pinda kwa upande wake, katika
nyakati tofauti aliwaarifu wakuu wa taasisi hizo za kimataifa juu ya hali ya
uchumi wa Tanzania, Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP), Ukanda wa
Kilimo wa Nyanda za Juu Kusini (SAGCOT) na mchakato wa kuandaa Katiba mpya.
Alisema ili kuendeleza kilimo, ipo haja ya kushirikiana na wadau kutoka
sekta binafsi kama njia ya kuleta maendeleo ya haraka nchini Tanzania. Bado
tunayo changamoto ya kukabiliana na umaskini, lakini tunaamini kuwa kilimo
ndiyo jawabu la tatizo hili,” alisema.
Waziri Mkuu alikwenda Roma, Italia kumwakilisha Rais Jakaya Kikwete kwenye
ibada maalum ya kumsimika Papa Francis iliyofanyika Jumanne, (Machi 19, 2013)
kwenye viwanja vya Kanisa Kuu la Mt. Petro mjini Vatican, kisha akaamua
kukutana na viongozi wa taasisi hizo.
Waziri Mkuu alirejea nchini siku ya Ijumaa, Machi 22, 2013).
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment