Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi
 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema asilimia 80% ya mapato ya fedha za kigeni zinazoingia Nchini kupitia Sekta ya Utalii inaweza kubakia kuwa ndoto kama suala la amani na utulivu halitazingatiwa  na kupewa nafasi yake chini ya usimamizi wa Jamii kwa mashirikiano na Serikali Kuu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  amesema hakuna  mgeni wala Mtalii atakayekuwa na shauku ya kutaka kuingia nchini endapo amani na utulivu uliopo utachezewa na hatimaye kutoweka kabisa.

Balozi Seif Ali Iddi ameeleza hayo wakati akizindua rasmi safari za ndege za shirika la Mango Airlines kati ya Afrika Kusini na Zanzibar, katika  hafla iliyofanyika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar.

Balozi Seif Idd amesema Taasisi, Jumuiya na hata watu wanaohudumia wageni na watalii wanapaswa  kuendeleza zaidi ukarimu uliopo Nchini ambao ni miongoni mwa utamaduni unaoikuza Zanzibar Kiutalii katika Mataifa ya Nje.


Kiongozi huyo amesema  Serikali kwa upande wake  itajitahidi  kutunza na kuidumisha amani na wale  wanaotishia usalama wa wananchi na mali zao watachukuliwa hatua zinazostahiki kwa mujibu wa sheria bila ya kumuonea mtu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema  soko hilo la Afrika Kusini ni kubwa na ni lazima kwa makampuni yanayohusika na sekta hiyo kujiimarisha ili kupata watalii wengi zaidi.

Takwimu za mwaka 2012 zinaonesha kuwa  idadi ya watalii kutoka Afrika Kusini ni kubwa na ilifikia watalii elfu 11,145 na kuchukuwa nafasi ya Tano miongoni mwa Nchi zilizoleta watalii wengi hapa Zanzibar.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top