WANANCHI wa Chwaka Zanzibar wameeleza kufarajika kwao baada ya kukamilika mradi wa maji safi na salama katika kijiji chao na kuondosha tatizo lililokuwa likiwakabili la ukosefu wa huduma hiyo kwa kipindi kisichopungua miaka saba.
 
Wakisoma risala yao mbele ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein mara baada ya kuuzindua mradi wa maji safi na salama kijijini hapo akiwa katika ziara yake katika Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

Katika maelezo yao kwenye risala yao waliyoisoma, wananchi wa Chwaka walitoa shukurani kwa Rais Dk. Shein pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa msaaada mkubwa wa fedha zilizotumika kuunulia mambomba yaliotumika katika kumalizia mradi huo.

Wananchi hao wa Chwaka walieleza kuwa walijitolea kwa hali na mali katika kufanikisa mradi huo na kuweza kuchangia Tsh. Milioni 37 pamoja na nguvu kazi na kuchimba mtaro pamoja na kufukia mabomba kutoka kisimani hadi Chwaka eneo lenye kilomita 7.

Wananchi hao wa Chwaka walitoa shukurani kwa wale wote waliochangia katika mradi huo akiwemo Mwakilishi wa Jimbo hilo Issa Haji Gavu aliyechangia Tsh. Milioni 41 zilizotumika kununulia mabomba na pambu ya kusukumia maji.

Aidha, katika risala yao hiyo wananchi wa Chwaka walitumia fursa hiyo kutoa shukurani kutoka kwa wavuvi wa kijiji hicho kwa kuthamini kilio chao cha muda mrefu.

Katika kuufanya mradi huo uwe endelevu wananchi hao wa Chwaka waliahidi kuwa wako tayari kushirikiana na Mamlaka ya Maji (ZAWA) katika kutoa ada ya matumizi ya maji kama ilivyopangwa na serikali.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top