Sura ya Mbele ya Uwanja wa Ndege Songwe Mbeya
MBUNGE wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (CHADEMA) amesema haungi
mkono pendekezo la Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Mbeya kutaka kuuita
Uwanja wa Ndege wa Songwe jina la Rais Jakaya Kikwete.
Akizungumza na Tanzania Daima jana jijini Dar es Salaam, Mbilinyi
maarufu kama Sugu alisema mapendekezo hayo yametolewa na watu wenye
kutaka kujipendekeza kwa mkuu wa nchi badala ya kufikiria kuutangaza
Mkoa wa Mbeya katika nyanja ya kimataifa.
Alisema Mbeya ina historia ya kutaka kujitangaza kimataifa na uwanja
huo ni fursa pekee ya kufikia malengo hayo aliyoeleza kuwa yanataka
kufifishwa na wateule wa rais.
“Siungi mkono uwanja kuitwa kwa jina la JK, tunataka jina
litakaloasisi uhalisia wa Mbeya nasi tufahamike kimataifa, kamati ya
ushauri ya mkoa chini ya Mkuu wa Wilaya ya Mbeya mjini, Norman Sigala
ilikurupuka kuleta wazo hilo kabla ya kuwasiliana na wabunge,” alisema.
Alisema hatua hiyo ya Sigala haiwakilishi mawazo ya wananchi bali
inawakilisha mawazo ya mtu aliyeteuliwa na kwamba wao wakiwa
wawakilishi wa Mkoa wa Mbeya kwa ridhaa ya wananchi hawawezi
kukubaliana na suala hilo.
Kauli ya Sugu iliungwa mkono na wabunge wengine wa Mkoa wa Mbeya,
ambapo Mchungaji Lukson Mwanjale wa Mbeya Vijijini (CCM) alisema
anasikitishwa na hatua hiyo ya kuliwasilisha wazo hilo bila ya
kuwashirikisha wabunge.
Alisema wakati wa kikao cha kamati ya ushauri wabunge wengi
hawakuwepo na taarifa hizo walizisikia baada ya kusoma kwenye vyombo
vya habari.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo ambaye pia
ni mbunge wa Songwe, aliomba apewe muda wa kutaka kujua sababu
zilizoibua wazo hilo.
Wazo la kuuita Uwanja wa Ndege wa Songwe jina la Rais Jakaya Kikwete
linazidi kupata upinzani ambapo awali chama cha NCCR-Mageuzi na kile
cha PPT Maendeleo kupitia kwa viongozi wa Mkoa wa Mbeya vilipinga wazo
hilo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment