Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (Tef), Absalom
Kibanda ambaye amelazwa Hospitali ya Millpark, Johannesburg nchini
Afrika Kusini kutokana na kupata majeraha makubwa baada ya kushambuliwa
na watu wasiojulikana, ameng’olewa jicho.
Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Tef, Neville Meena inaeleza jana aliingizwa kwenye chumba cha upasuaji katika hospitali hiyo, kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji na kurekebishwa sura.
“Nachukua fursa hii kuwapa maendeleo ya tiba ya Mwenyekiti wa Tef Absalom Kibanda, ambaye amelazwa Hospitali ya Millpark, Johannesburg nchini Afrika Kusini, leo ameingizwa theater (chumba cha upasuaji) ili kuanza kufanyiwa upasuaji na kurekebishwa sura, baada ya kupungua kwa uvimbe katika majeraha aliyokuwa nayo sehemu mbalimbali za mwili wake, hususan kichwani na usoni,” alisema Meena katika taarifa yake hiyo.
Meena alifafanua kuwa upasuaji huo unazingatia matokeo ya uchunguzi uliofanywa kwa zaidi ya saa 48 na jopo la madaktari, ambao walibaini kwamba mbali na madhara ya awali, Kibanda pia aliumizwa taya lake la kushoto.
“Kuhusu jicho lake la kushoto ambalo pia lilijeruhiwa, madaktari walisema wangetoa uamuzi kuhusu aina ya upasuaji ambao wangeufanya baada ya kubaini hali halisi, wakati watakapokuwa wakirekebisha sura yake ambayo iliharibiwa kwa majeraha,” alisema.
Alisema Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd ambao ni wachapishaji wa magazeti ya Rai,
Mtanzania, Dimba na Bingwa, bado ana maumivu
makali kutokana na majeraha aliyopata, kwani hata wakati akipelekwa
kwenye upasuaji huo uliotarajiwa kuchukua saa zaidi ya nne, alikuwa
akilalamika kwa maumivu zaidi kwenye kidonda kilichopo kwenye mguu
wake wa kushoto.
“Tutaendelea kufahamishana kila hatua ya tiba ya mwenyekiti wetu, na tunaomba tuendelee kumwombea ili apone haraka,” alisema Meena.
Juzi jopo la madaktari wanaomtibu katika hospitali hiyo walibaini madhara zaidi aliyoyapata Kibanda, kutokana na unyama aliofanyiwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Jumatano wiki hii.
Madhara hayo ni pamoja na kukatika kwa
mshipa unaounganisha pua na mdomo, kulegea kwa meno sita, awali
ilibainika kuwa ametobolewa jicho lake la kushoto, kung’olewa meno
mawili, kunyofolewa kucha, kukatwa mara tatu kwenye kichwa chake.
Katika hatua nyingine, Rais Jakaya Kikwete jana alimtembelea Kibanda hospitalini alikolazwa akiongozana na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.
Meena alisema Rais Kikwete amesema Serikali itajitahidi kuwasaka waliohusika na tukio la utesaji wa Kibanda, ili wafikishwe mahakamani kwa mujibu wa sheria.
Rais Kikwete na Kinana wapo Afrika Kusini kwa ziara ya kikazi, ambapo waliamua kutumia fursa hiyo kwenda kumtembelea mhariri huyo.
Hadi Kibanda anasafirishwa kwenda Afrika Kusini Alhamisi wiki hii kwa matibabu zaidi, viongozi wa Serikali waliofika kumjulia hali ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi pamoja na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, wahariri na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Via Mwananchi
0 comments:
Post a Comment