TFF YAWATULIZA WADAU SAKATA LA KATIBA
RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) amewataka wadau wa mchezo huo kuwa watulivu kwa vile tofauti zilizojitokeza kati ya Shirikisho na Serikali zitamalizwa kwa taratibu za mpira wa miguu.
 
Amesema nia ya TFF ni kuhakikisha Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) haliifungii Tanzania kwani tayari Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara alishaahidi kuwepo kikao kati yake na viongozi wa TFF kitakachofanyika Jumanne (Machi 19 mwaka huu).
“Suluhu itapatikana kwa mazungumzo kati ya Wizara na TFF. Naamini suala hili tutalimaliza baada ya kikao cha Machi 19 ambacho kimepangwa na Waziri kutokana na maombi ya TFF,” amesema Rais Tenga na kuongeza kuwa tatizo lilianzia kwenye mchakato wa uchaguzi ambao umesimamishwana FIFA.
FIFA ilisimamisha Mkutano Mkuu wa uchaguzi baada ya baadhi ya wagombea walioenguliwa kulalamika, na yenyewe kuahidi kutuma ujumbe wa kushughulikia suala hilo.
Rais Tenga amesema lisingetokea tatizo hilo, TFF tayari ilishaitisha Mkutano Mkuu ambao ungefuatiwa na uchaguzi. Lakini kwa vile FIFA ndiyo iliyosimamisha mkutano huo, TFF inalazimika kusubiri hadi FIFA itakaposhughulikia suala hilo na kutoa maelekezo ikiwemo lini mkutano ufanyike.
Amesema kwa kuamini tatizo hilo litamalizwa ndani ndiyo maana TFF hadi sasa haijapeleka FIFA maagizo ya Waziri Dk. Fenella ya kutengua marekebisho ya Katiba ya TFF ya mwaka 2012, kuitisha Mkutano Mkuu wa marekebisho ya Katiba na Mkutano Mkuu wa Uchaguzi, kwani ingefanya hivyo Tanzania ingefungiwa mara moja.
TFF inasisitiza kuwa FIFA ilijua tatizo la Serikali kutoa maagizo kwake kupitia vyombo vya habari, hivyo kumuandikia Rais Tenga na kueleza msimamo wake iwapo itabainika kuwa Serikali imekuwa ikiingilia uendeshaji wa shughuli za mpira wa miguu.

Uhalali wa kuwepo kwa barua ya FIFA kwenda kwa Rais Tenga juu ya suala hilo ulihojiwa pia na mwandishi wa Reuters, Brian Homewood baada ya kusoma kupitia vyombo vya habari nchini kuwa Shirikisho hilo huenda likaifungia Tanzania ikibainika Serikali inaingilia shughuli za TFF.
 

Mawasiliano kati ya FIFA na mwandishi huyo ambapo majibu yake pia TFF ilipewa nakala yameambatanishwa katika taarifa hii.


TFF YAONDOA ‘FREE PASS’ MPIRANI  
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeondoa utaratibu wa wadau wake kuingia bure kwenye mechi kwa kutumia tiketi maalum (free pass).
Kutokana na uamuzi huo hakutakuwa tena na pasi za bure kwa ajili ya kushuhudia mechi zilizo chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa TFF katika viwanja mbalimbali nchini.

Uamuzi huo umetokana na ukweli kuwa free pass zimekuwa zikipunguza au kuchukua mgawo wote wa TFF kwenye mechi, na wakati mwingine Shirikisho hulazimika kutoa fedha za ziada kugharamia pasi hizo.

Pasi zote ambazo imekuwa ikitoa kwa wadau wake hukatwa katika mgawo wa TFF katika mechi husika. Shirikisho hivi sasa linapata asilimia nne tu ya mapato katika mechi za Ligi Kuu, ligi ambayo hivi sasa inaendeshwa na Kamati yake ya Ligi.

RUVU SHOOTING KUIKABILI YANGA VPL
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho (Machi 16 mwaka huu) kwa mechi tatu ambapo Yanga itakuwa mgeni wa Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mwamuzi Jacob Adongo kutoka Musoma mkoani Mara ndiye aliyepewa jukumu la kuchezesha mechi hiyo namba 146. Adongo atasaidiwa na Anold Bugado wa Singida na Milambo Tshikungu kutoka Mbeya wakati mwamuzi wa mezani ni Hashim Abdallah wa Dar es Salaam.
Mtathmini wa waamuzi ni Army Sentimea wakati Kamishna wa mechi hiyo inayokutanisha vinara Yanga na Ruvu Shooting inayoshika nafasi ya saba ikiwa na pointi 29 chini ya ukufunzi wa Charles Boniface Mkwasa na Msaidizi wake Selemani Mtungwe ni Emmanuel Kavenga kutoka Mbeya.
Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 5,000 kwa viti vya bluu na kijani, sh. 8,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 kwa viti vya VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh. 20,000.

Pia TFF inawaasa washabiki wa mpira wa miguu kuacha kununua tiketi mikononi mwa watu kwa vile wanaweza kuuziwa tiketi bandia. Tiketi zote zitauzwa katika vituo vinavyotangazwa katika magari maalumu, na uwanjani pia katika magari hayo.

Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wenye uwezo wa kuchukua washabiki 25,000 utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Toto Africans na Mgambo Shooting kutoka Tanga. Ugumu wa mechi hiyo unatokana na ukweli kuwa timu zote mbili zinapigana kuepuka kurudi zilikotoka (daraja la kwanza).

Mgambo Shooting inayonolewa na Mohamed Kampira inashika nafasi ya tisa ikiwa na pointi 24 katika ligi hiyo yenye timu 14. Toto Africans ambayo iko nyumbani itaingia uwanjani ikiwa na pointi 14 katika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi.

Baada ya kulala 2-1 mbele ya Simba katika mechi iliyopita, Coastal Union itakuwa mgeni wa Mtibwa Sugar katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro.


Ligi hiyo itaendelea tena keshokutwa (Machi 17 mwaka huu) kwa mechi moja itakayozikutanisha JKT Ruvu na Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Azam Complex.


RAMBIRAMBI MSIBA WA OFISA HABARI CECAFA

Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha aliyekuwa Ofisa Habari wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Finny Muyeshi
kilichotokea juzi (Machi 13 mwaka huu) jijini Nairobi, Kenya baada ya kuugua kwa muda mrefu.


Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani Muyeshi aliitumikia CECAFA kwa muda mrefu, hasa katika kuhakikisha waandishi wa habari wanapata mazingira mazuri ya kufanyia kazi wakati
wanaporipoti matukio mbalimbali ya Baraza hilo.

Alitoa mchango mkubwa katika eneo la habari za mpira wa miguu, tangu akiwa gazeti la East African Standard la Kenya akiwa mwandishi, na baadaye Mhariri wa Michezo kabla ya kujiunga na CECAFA, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.

TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Muyeshi, CECAFA, Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya (FKF) na tasnia ya habari kwa ujumla, na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Mungu aiweke roho ya marehemu Muyeshi mahali pema peponi. Amina

FDL KUKAMILISHA MSIMU WIKIENDI
Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu wa 2012/2013 unamalizika wikiendi hii huku timu za Mbeya City ya Mbeya, Ashanti United ya Dar es Salaam na Rhino Rangers ya Tabora zikiwa tayari zimepata tiketi ya kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao.
Kundi A mechi zote zitachezwa Jumapili (Machi 17 mwaka huu) ambapo Majimaji vs Mbeya City kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea, Kurugenzi vs Mkamba Rangers (Mafinga) na Burkina Faso vs JKT Mlale (Jamhuri, Morogoro).

Kesho (Machi 16 mwaka huu) katika kundi B itakuwa Green Warriors vs Polisi Dar (Karume, Dar es Salaam) na Ndanda vs Villa Squad (Nangwanda Sijaona, Mtwara). Keshokutwa (Machi 17 mwaka huu) ni Moro United vs Ashanti United (Karume, Dar es Salaam) na Tranist Camp vs Tessema (Mabatini, Mlandizi).


Kundi C ni kesho (Machi 16 mwaka huu) Polisi Tabora vs Pamba (Ali Hassan Mwinyi, Tabora). Keshokutwa (Machi 17 mwaka huu) ni Polisi Mara vs JKT Kanembwa (Karume, Musoma), Polisi Dodoma vs Mwadui (Jamhuri, Dodoma) na Rhino Rangers vs Morani (Ali Hassan Mwinyi, Tabora).


KILA LA KHERI AZAM KOMBE LA SHIRIKISHO

Kikosi cha Timu ya Azam
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaitakia kila la kheri timu ya Azam kwenye mechi yake ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Barrack Y.C. II itakayochezwa Jumapili (Machi 17 mwaka huu) nchini Liberia.

Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza itachezwa jijini Monravia na timu hizo kurudiana wiki mbili baadaye jijini Dar es Salaam. 

Ofisa Habari wa Azam yuko na timu hiyo Monrovia na anapatikana kwa namba +231888386655.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top