WATU wenye ulemavu
mkoani Ruvuma wamependekeza madaraka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ni vyema yapunguzwe kwani kwa muda mwingi inaonekana Rais amekuwa akielemewa na
kazi nyingi sana ambazo zingeweza kufanywa na waziri mkuu wa nchi.
Watu hao wenye ulemavu
walitoa mapendekezo yao kwenye semina
iliyoendeshwa kwa muda wa siku mbili chini ya mradi wa kuhamasisha watu wenye ulemavu katika mchakato wa
kukusanya maoni ya katiba mpya uliofadhiliwa na shirika lisilo la kiserikali la
“Foundation for Civil Society” la jijini Dar es Salaam iliyofanyika kwenye
ukumbi wa mikutano wa SACCOS ya wafanyakazi wa Halmashauri ya manispaa ya
Songea.
Mjumbe wa Chama cha
Viziwi Tanzania (CHAVITA) mkoani Ruvuma Henry Chaima alisema kuwa katiba mpya
ni lazima iweke bayana kuona kazi anazozifanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ili aweze kupunguziwa madaraka ambayo yatamwezesha kufanya kazi kwa
ufanisi zaidi tofauti na ilivyo sasa ambapo amekuwa akielemewa na kazi nyingi
sana.
Alipendekeza kuwa Rais
awe na madaraka ambayo hayamsababishii usumbufu zaidi mfano, uteuzi wa wakuu wa
wilaya na wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya, Maspaa na Majiji ufanywe na
Waziri Mkuu ambaye ni mtendaji mkuu wa serikali na kwamba mawaziri wasiwe
wabunge.
Asia Abdallah ambaye ni
katibu wa CHAVITA mkoa wa Ruvuma ameomba katiba mpya iweke bayana lugha kwa
watu wenye ulemavu wa kutosikia kwani lugha ya wasiosikia ni ngumu kuielewa
hasa kwa watu wenye ulemavu wa kutosikia kutokana na uhaba wa shule maalumu kwa
watu wasiosikia.
Naye Kelvin Vicent
ambaye ni Mwenyekiti wa CHAVITA mkoa wa Ruvuma amependekeza kuwa kwenye katiba
mpya ijayo kuoneshe wazi uwepo wa mgombea binafsi wa nafasi ya urais kwani kuna
watu wengine ambao ni watanzania wenye sifa nzuri za kuiongoza nchi lakini si
wanachama wa chama chochote cha siasa jambo linalowafanya wakose sifa ya
kugombea.
Amebanisha zaidi kuwa
vilevile mikataba ya nchi iwe wazi kwa wananchi mfano ardhi na mikataba ya
biashara mbalimbali ya kimataifa na pale inapogundulika kuwa mahali fulani pana
madini wananchi wa maeneo hayo ni vema wakashirikishwa ili kujua namna zoezi la
uchimbaji wa madini hayo litavyondeshwa na wao wakafahamu faida watakayoipata
kutokana na uchimbaji huo.
Aidha, wameitaka katiba
mpya iseme wazi juu ya miundombinu ya walemavu wa aina zote na kwamba vyama vya
walemevu vipatiwe ruzuku na kuwepo na uwakilishi mzuri Bungeni kwa asilimia
therathini kama inavyofanywa kwenye jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania
(UWT), Vijana, uwakilishi wa vyuo vikuu na wabunge wa viti maalumu.
Wamesema muungano wa
nchi ya Tanzania uvunjwe na badala yake uwe wa serikali tatu yaani serikali ya
Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na serikali ya Jamhuri ya Muungano kwani kwa
muungano tulionao kwa hivi sasa watanzania wengi bado hawajauelewa
kinachoshangaza Zanzibar wana serikali yao yenye maamuzi kamili tofauti na serikali ya
Muungano.
Iko haja kwa sasa
katiba mpya itamke kuwa spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
asitokane na chama chochote cha siasa na badala yake nafasi hiyo itangazwe ili
watu wagombee kama wanavyogombea ubunge kuondoa utata unaojitokeza kwenye vikao
vya Bunge.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment