WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema makampuni yapatayo 22 yamejiunga na Mpango wa Kupambana na Malaria kupitia sekta binafsi na sekta ya michezo (Malaria Safe Companies) ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali za kushirikiana na sekta binafsi kumaliza kabisa ugonjwa huo.

Alitoa kauli hiyo jana usiku (Jumamosi, Februari 9, 2013) wakati akishiriki mjadala kuhusu juhudi za Serikali katika kupambana na ugonjwa wa malaria uliofanyika kwenye kituo cha mikutano cha Sandton, kilichopo jijini Johannesburg, Afrika Kusini.


Amesema si jambo rahisi kuiachia Serikali peke yake iendeshe mapambano dhidi ya ugonjwa huo, ndiyo maana Serikali ya Tanzania iliamua kutumia mfumo wa kushirikisha sekta binafsi ili kuongeza chachu katika kampeni hiyo.


“Ugonjwa wa Malaria hauna mipaka. Huwezi kusema mbu ataishia Tanzania, Zimbabwe, Malawi au Afrika Kusini tu. Tunapaswa kuungana pamoja, na mimi natamani kuona nchi zetu zikiungana kupambana na ugonjwa huu,” alisema.


Alisema mpango huo ulianza mitatu iliyopita lakini ulizinduliwa rasmi mwishoni mwa mwaka jana. Aliyataja baadhi ya makampuni hayo ni Bakhresa, Kampuni za Bia za SBL na TBL, SONGAS, NSSF, PPF na Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF). Tanzania ni nchi ya pili kati ya 12 barani Afrika zilizojiunga na Mpango huo. 


Alilitaka Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kutumia fursa ya mashindano hayo yanayofikia kilele chake leo, lichukulie mapambano haya kama changamoto ya kuziunganisha nchi wanachama wa SADC katika mapambano dhidi ya malaria kwani katika ngazi ya Umoja wa Afrika (AU) suala hilo limekwishapiga hatua.


Mjadala huo uliwashirikisha Waziri wa Afya wa Afrika Kusini, Dk. Aaron Motsoaledi na Naibu Waziri wa Afya wa Msumbiji, Dr. Nazira Vali Abdulla ambao walihojiwa na mtangazaji wa habari za michezo wa kituo cha televisheni cha SuperSport, Bi. Carol Tshabalala ikiwa imebakia siku moja tu kufanyika kwa fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2013).


Mjadala huo uliandaliwa ili kuzihimiza serikali za nchi za Afrika kuongeza juhudi katika kupambana na malaria ambao unaongoza kwa vifo vitokanavyo na ugonjwa huo. Mahojiano hayo yatarushwa leo usiku kwenye fainali za michuano hiyo itakayozikutanisha timu za Nigeria na BurkinaFaso.


Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, takwimu za mwaka 2011 zinaonyesha kuwa kati ya vifo 655,000 vinavyotokana na malaria kila mwaka, asilimia 91 ya vifo hivyo inatokea barani Afrika. Na asilimia 86 ya vifo hivyo, huwakumba watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.


Ili kupambana na ugonjwa huo, bara la Afrika linagharimika kutumia kiasi cha dola za marekani bilioni 12 kila mwaka zikiwa ni kwa ajili ya matibabu na muda ambao unapotea kwa wafanyakazi kukosa kufanya kazi au wananchi kushindwa kufanya shughuli za uzalishaji.


Naye mwanamuziki maarufu nchini Afrika Kusini, ambaye pia ni Balozi wa Kupambana na Malaria barani Afrika, Bi. Yvonne ChakaChaka ambaye alishiriki chakula cha jioni mara baada ya mjadala huo, alisema wadau wengi zaidi wanahitajika kushiriki kampeni hii ifike mahali idadi ya vifo vya watoto wachanga ipungue.


”Nilipoanza kufanya uhamasishaji wa kupambana na malaria ni Ethiopia pekee ambao walikubali kushirikiana nami. Wakati huo kila sekunde 30 mtoto mmoja alikuwa anakufa kutokana na ugonjwa huo, lakini sasa hivi imefikia kila baada ya dakika moja,” alisema.


”Zinatakiwa jitihada zaidi za wadau wote ili ifike mahali tuseme mtoto mmoja anapoteza maisha kwa ugonjwa huu kila baada ya saa moja, siku moja au kila baada ya wiki moja na pengine tufike mahali iwe hakuna kabisa vifo vya aina hiyo ,” alisema.


Alisema anaujua ubaya wa malaria kwa sababu mmoja wa wanamuziki wake alipoteza maisha kutokana na ugonjwa huo. “Ni lazima tuunganishe nguvu katika vita dhidi ya malaria la sivyo vizazi vijavyo vitatuhukumu. Tunaweza kumaliza ugonjwa huu, kila mmoja akitimiza wajibu wake,” alisisitiza.


Waziri Mkuu amerejea nchini mchana huu na kwenda moja moja Dodoma kuhudhuria vikao vya Chama cha Mapinduzi.


    

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, FEBRUARI 10, 2013.

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top